January 4, 2020





Na SALEH ALLY
TANGU msimu wa 2011/12 watani wa jadi Yanga na Simba wamefungana jumla ya mabao 32 tu. Hivyo kwa yule anayeamini ushindi wa timu moja leo utakuwa mkubwa wa kutisha, asahau.

Usiende na matokeo yako mfukoni Uwanja wa Taifa ukiamini timu moja itakuwa dhaifu sana na kufungwa mabao mengi sana, sahau.

Mechi hii ya watani wa jadi, imekuwa ngumu sana tofauti na watu wengi ambavyo wamekuwa wakiichukulia na ugumu wake umekuwa hautabiriki na haujali hata kama timu moja inaongoza ligi na nyingine katika nafasi ya 10 katika msimamo, Simba na Yanga inajitegemea, ni mechi iliyo katika “kisiwa” chake.

Ukiangalia ndani ya misimu nane, yaani mechi 16 za Ligi Kuu Bara, Simba na Yanga zimefungana mabao 32 tu na huu ni wastani wa bao moja tu katika kila mechi na hii inadhihirisha kuwa mabao hayaji kirahisi hivyo katika mechi za watani. Hii inatokana na mambo mengi sana ikiwemo presha.


Baada ya mechi ya pili ya msimu wa 2011/12 ambayo Simba iliishinda Yanga kwa mabao 5-0, Kocha Mkuu wakati huo, Milovan Cirkovic aliniambia hivi: “Saleh, matokeo kama haya, yatachukua miaka mingi sana kutokea tena na mara nyingi hupatikana kwa timu ambayo tayari ina nafasi kubwa ya kuwa bingwa kwa kuwa inacheza bila presha lakini si mzunguko wa kwanza.”

Kama unakumbuka, mechi ya kwanza msimu huo, Simba ililala kwa bao 1-0, mfungaji akiwa Davis Mwape raia wa Zambia. Lakini mzunguko wa pili, Simba ambayo ilikuwa na uhakika wa ubingwa ikaishindilia Yanga idadi hiyo kubwa ya mabao ambayo sasa ni miaka saba, hakujawahi kuwa na matokeo hata yanayokaribiana na hayo.

Angalia msimu wa 2013/14, mzunguko wa kwanza, Simba ikiwa haina hali nzuri ikionekana kuna nafasi kubwa ya kufungwa, ilianza kutangulia kufunga kwa bao la Haruna Chanongo dakika ya 75, zikiwa zimebaki dakika nne mpira kwisha, Simon Msuva akaisawazishia Yanga na mechi hiyo ya kwanza ikaisha kwa sare ya 1-1.

Mechi ya pili, mambo yalikuwa yameshabadilika, Yanga ilikuwa imejihakikishia ubingwa na timu yao ilikuwa ina kiwango cha juu na wachezaji wakongwe waliozoeana, wakati Simba katika kiungo iliowategemea kama akina Humud Abdulkarim wakionekana kama wamechoka sana.

Mechi hiyo ya mzunguko wa pili, hadi dakika 45 za kwanza, Yanga walikuwa wanaongoza kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa (Dk 15), Hamis Kizza (Dk 35 & 45). Wakati timu zinakwenda mapumziko, mashabiki Yanga wakaanza kuimba, “siku ya kisasi imefika”. Wakimaanisha siku hiyo walikuwa wanaifunga Simba mabao 5-0 na kulipa kisasi.

Kipindi cha pili, benchi la ufundi la Simba lilifanya mabadiliko na kuwatoa wachezaji nyota na wakongwe kama Humud na kuwaingiza Said Ndemla na William Lucian maarufu kama Gallas, hawa walikuwa makinda kabisa.

Kwa baadhi ya mashabiki wa Simba waliona zile tano zilikuwa zimetimia hasa kutokana na waliokuwa wakiingia, yaani wachezaji makinda kabisa.

Dakika 53, Betram Mwombeki akaifungia Simba bao moja, dakika ya 60, Joseph Owino akaifungia Simba bao la pili na beki mwingine Mrundi, Gilbert Kaze akaifungia Simba bao la kusawazisha dakika ya 84. Dakika ya 88, Simba wakakosa bao la wazi ambao wangekuwa makini lingekuwa la nne. Mechi iliisha kwa sare ya mabao 3-3.
Mechi hii hadi sasa ndio sare bora “come back” bora zaidi katika mechi ya watani katika kizazi hiki. Imeendelea kubaki katika rekodi na historia kwa muda mrefu zaidi kama gumzo lakini ina mafunzo mengi yanayoendelea kuonyesha utofauti wa mechi ya watani tofauti na wengine ambavyo wamekuwa wakiyachukulia mambo kishabiki au kitaalamu sana.
Hivyo mechi ya watani Yanga na Simba, si ya kuichukulia kiulaini hivyo kwa kuona itakuwa nyepesi na timu fulani kwa kuwa ni kali basi itaiangusha nyingine kirahisi.

Kawaida wakati wa mechi hii, kunakuwa na mambo mengi sana, huduma tofauti katika kila timu. Morali inakuwa juu, ahadi ya zawadi, kambi bora, chakula kizuri zaidi na wachezaji wanahamasika na kucheza tofauti na wakati mwingine timu inayotarajiwa kufanya vizuri inaweza kupoteza.

Ugumu wa mechi hizi unaonekana wazi, kwamba katika mechi 16, misimu nane, timu zimefungana mabao 32, hii ukijumlisha na hayo 5-0 ya Simba dhidi ya Yanga. Mwisho yanaandika wastani wa bao moja kwa kila timu kila mechi.


Katika mechi hizo 16, Simba ndio wanaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi kwani wamefunga 17 na Yanga wamefunga 15. Hii ni sehemu nyingine ya kudhihirisha kuna ugumu kwa kuwa tofauti ndani ya mechi 16 ni mabao mawili tu, maana yake hakuna mbabe sana kupita mwingine kwa kiwango cha juu sana katika mechi zote 16 ambazo si chache.
Angalia kuhusiana na ushindi, unaona pia hakuna tofauti kubwa katika mechi hizo 16 maana Simba wanaongoza wakiwa wameshinda mechi tano, Yanga wameshinda nne na sare saba.

Idadi kubwa ya sare inadhihirisha pia ugumu wa mechi za watani wa jadi, ndio maana naweka msisitizo, hii si mechi ya kwenda na matokeo uwanjani.

Ukibahatika kuingia uwanjani, basi tulia katika siti yako, furahia dakika 90 na matokeo yatajulikana hapo. Hali kadhalika kama utaangalia katika runinga ya Azam TV, basi mechi hii, inahitaji uburudike kwanza na matokeo yatafuatia ukiwa unaangalia.

 TAKWIMU TOKEA MSIMU WA 2011/12
USHINDI
Simba 5
Yanga 4
Sare 7

 MABAO
Yamefungwa 32
Simba  17
Yanga  15

Misimu 8
Mechi 16
Dakika 1,440





2 COMMENTS:

  1. Kisha hiyo mechi ya 3-3 dk ya mwisho kuna goli alikosa kavumbangu mbona ujaiandika weye Jembe usio na mpini

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic