January 4, 2020






Na Saleh Ally
MKONGWE Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, ndiye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika mechi moja ya derby ya Kariakoo.


Kibadeni ndiye mtu pekee mwenye mabao matatu ‘hat trick’ katika mechi moja. Ilibaki kidogo mshambuliaji kipenzi cha Wanasimba aifikie rekodi hiyo mwaka 2012.


Ilikuwa Mei 6, 2012 wakati Simba iliposhinda kwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga. Katika mechi hiyo, Okwi raia wa Uganda alifunga mabao mawili na angeweza kufunga matatu lakini mkwaju wa penalti ambao wengi waliamini angepiga yeye, kipa mkongwe Juma Kaseja akaomba aupige, akapewa na kuanzika bao la nne katika dakika ya 66. Marehemu Patrick Mutesa Mafisango ndiye alihitimisha bao la tano katika dakika ya 71.


Ukiangalia hata mechi hiyo, utaona katika mabao matano ni moja tu lilifungwa na mzalendo, yaani Kaseja, mengine manne yalifungwa na Okwi mawili, Felix Sunzu na Mafisango.


Hapo ndipo ninaanzia kwamba wachezaji wa kigeni bila ya kujali wako Yanga au Simba, ndiyo wamekuwa na mabao mengi zaidi katika mechi za watani hao wa jadi na nimeamua kuanzia karibuni kwa maana ya mwaka 2011 nikitumia kizazi hiki.


Miaka mingi ya nyuma, hakukuwa na idadi kubwa sana ya wageni. Inawezekana kuanzia mwaka 2005 kuja juu, idadi ya wageni ikaanza kuongezeka na kuanzia 2011 nahesabu na kuona katika mechi 16 za misimu nane, wageni ndio wametawala kwa kutupia kambani.


Wageni wanaonekana kuwa washambuliaji au wachezaji wanaong’ara zaidi kinapofikia kipindi cha mechi za watani.

Inawezekana ni kutokuwa na hofu kuu kuliko wenyeji ambao wanaweza kuwa wanajua ugumu au hisia za historia ya mechi hiyo inawafanya kutokuwa “waliochangamka” kama inavyotakiwa.


Unaona zimechezwa mechi 16 kwa miaka hiyo nane, wageni wamefanikiwa kufunga mabao 19 dhidi ya yale 13 ambayo yamefungwa na wenyeji.


Wageni wakiwemo akina Sunzu, Donald Ngoma, Davies Mwape kutoka Zambia, Okwi na Hamisi Kiiza (Uganda) au Didier Kavumbagu na Amissi Tambwe kutoka Burundi na sasa Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere ni sehemu ya wageni ambao wamekuwa wakiongeza maksi nyingi kwa wageni wanaosumbua katika mechi ya watani wa jadi.

Mfano msimu huo wa 2011/12, wageni walitamba zaidi kwa kuwa katika mechi mbili za Simba na Yanga, yaani ile ya mzunguko wa kwanza na wa pili, wageni walifunga jumla ya mabao matano na wenyeji akawa mmoja, Juma Kaseja ambaye alifunga bao moja.


Msimu wa 2012/ 13, mechi mbili za mizunguko miwili ya Ligi Kuu Bara, wenyeji na wageni wakafungana na ikawa mabao 2 kwa 2 kama ilivyokuwa msimu uliofuata wageni wakawa na 4 sawa na wenyeji.


Msimu wa 201/15, wageni wakafunga moja, wenyeji hakuna kitu, msimu wa 2015/16, wageni wakawa na mabao matatu na wenyeji moja. Msimu wa 2016, mechi mbili zikazaa mabao 1 kwa 2.

Msimu pekee ambao wenyeji wanaweza kujitamba katika misimu nane ni ule wa 2017/18 ambao wenyeji walifunga mabao mawili na wageni mmoja. 


Hii ilitokana na mechi ya kwanza kuisha kwa sare ya 1-1, upande wa Yanga akifunga Obrey Chirwa na Shiza Kichuya upande wa Simba. Mechi ya pili, Simba wakashinda kwa bao 1-0, Erasto Nyoni akifunga bao pekee.


Msimu uliofuata yaani wa 2018/19, wenyeji wameendeleza ubabe tena baada ya kuongoza kwa mabao mawili kwa moja. Hii ni baada ya mechi ya kwanza kuisha sare ya bila bao na ile ya pili, Simba wakashinda bao 1-0 lililofungwa na Kagere.


Hii inaweza kuwa na somo kwa kiasi fulani, kwamba Yanga na Simba zaidi zimeamini wageni na si wachezaji wa nyumbani. Au wenyeji wamesahaulika sana au wanatakiwa wajikomboe kwa kujituma sana.



Dalili za wenyeji kuendelea kutamba, zinaonekana zitaendelea na kuthibitisha hilo angalia safu ya ushambulizi ya Yanga, pia ile ya Simba. Acha tuone mechi hii, kama ni mabao watakaofunga zaidi watakuwa wageni au wenyeji. Unaandika?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic