SAFARI moja huanzisha safari nyingine hivyo ni wakati mwingine
wa kutazama ni namna gani tutaweza kuendelea vizuri pale ambapo tumeanza kwa
upande wa Wanawake.
Timu yetu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 imeanza kwa mguu mzuri ndani ya mwaka huu 2020 kwa ushindi wa mabao 5-1 mbele ya timu ya Taifa ya Burundi hili ni jambo la kujivunia kwetu.
Tunaona kwamba michuano ya kuwania tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya miaka 17 inaushindani mkubwa kutokana na kasi ambayo imeanza nayo.
Imani yangu ni kwamba bado kuna kazi ambayo inatakiwa kufanywa kwa benchi la ufundi na wachezaji ili kuona namna gani watapata tena matokeo chanya huko nchini Burundi.
Januari 25, mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa tena safari hii itakuwa nchini Burundi wao watakuwa wenyeji wetu kazi ipo tena kubwa tu.
Tukibweteka na kuona kazi imemalizika hapo ndipo ambapo tutakuwa tumekosea kwani tutatoa nafasi kwa wapinzani wetu kutupa kichapo ambacho hatutasahau na kuacha wao wakipenya sisi tukibaki kuwa watazamaji.
Itakuwa ni maumivu kwa mashabiki pamoja na benchi la ufundi kwani licha ya kuwa mpira una matokeo matatu kuna wakati tunapaswa nasi tuwe na chaguo la aina ya matokeo kutokana na mwanzo ambao tumeanza nao.
Ndio ninamaanisha kwamba inawezekana kupata matokeo mazuri hata ugenini kwani ushindi wa mabao 5-1 unatupa picha kwamba tunaweza kupata hata zaidi ya hayo tukiwa ugenini.
Tukumbuke kwamba wao wenyewe Burundi wametuambia kwamba walizoea kufanya mazoezi kwenye uwanja wa nyasi bandia na kucheza kwenye uwanja mdogo wa nyasi zao za bandia.
Basi hapo ndipo tunapotakiwa kuanza kuangalia ni namna gani tutawashinda wapinzani wetu kwani silaha zao za kazi wametuachia tunachotakiwa ni kuzimiliki huku wao wakiamini ni zao.
Kwenye soka mbinu ya kwanza ambayo inatumika kutoa ushindi kwa timu ni kujua aina ya mbinu ambazo wanazo wapinzani kisha mazoezi na kujituma kazi inakuwa imeisha.
Kwa kuwa wao wenyewe wamesema kwamba uwanja wao ni mdogo na tena ni wa nyasi bandia basi tuanze kufanya mazoezi kwenye uwanja mdogo wenye nyasi za bandia na utatawafanya wachezaji wetu wawe kwenye wakati mzuri wa kupata matokeo.
Uzuri ni kwamba tuna viwanja vingi vya michezo ambavyo ni vya nyasi bandia kwa sasa hilo tunajivunia ni jambo jema kuwa navyo basi vitumike katika matumizi sahihi.
Hapo jambo la msingi ni kutazama na kutafuta mazingira ya Burundi yanafanana na wapi ili kambi iwekwe tena haina matatizo popote kambi inaishi bila matatizo.
Ikiwa labda ipo kama ile ya kanda ya ziwa basi watoto wapelekwe kule Mwanza wakarukeruke Nyamagana pale pana uwanja mzuri wa nyasi bandia, mambo yakiwa magumu sana wapelekwe hata pale Kaitaba.
Bukoba kule wakale na ndizi maana pana uwanja pale wa Kaitaba nao ni nyasi bandia tena safi kabisa watapata muda wa kujipanga ikibidi wapelekwe mpaka Sobibo ilipo kambi ya Kagera Sugar wajifunze ujasiri.
Ikiwa ngumu sana basi wabaki Bongo wakafanye mazoezi pale Chamazi kwenye uwanja bora ambao hata Caf inautambua kwani mechi nyingi huwa zinachezwa pale.
Karume pia pana uwanja wa nyasi bandia ila hapa sishauri sana maana huu uwanja bado haujafanyiwa ukarabati tusije kuwaumiza watoto wetu bure bora waende hata Uhuru pale watakuwa huru kujifunza na kupata uzoefu kidogo.
Labda ratiba zinaweza kuwa ngumu basi itapendeza wakipelekwa Bunju nje kidogo ya jiji la Dar pale kuna uwanja wa Mo Simba nao una nyasi bandia. Kwa namna hali ilivyo inaitwa tushindwe sisi tu kushinda.
Maandalizi yakiwa mazuri na wachezaji wakajitambua wanahitaji nini basi kazi ya kwanza inakuwa imekwisha zinabaki dakika tisini tu za mwamuzi kujua ataita kati mipira mingapi ambayo itapachikwa kimiani
Wito wangu kwa mashabiki mwendo ambao wameuanza mwaka 2020 uwe wa kila siku kwani kuna tofauti kidogo ambayo inaonekana hasa kwa wao kujitokeza uwanjani kutoa sapoti kwenye timu ambazo zinakuwa zinacheza.
Naona kwamba ari inarudi taratibu na wengi wanaanza kujitokeza uwanjani basi ni wakati sahihi kwa Shirikisho la Soka Tannzania (TFF) kuboresha namna na mitindo ya watazamaji kuendelea kuwa wengi uwanjani.
Tatizo ni kwamba wengi wa watanzania wanapenda mpira na kwenda uwanjani ila muda mwingine mazingira yanakuwa si rafiki kwao kuingia ndani ya uwanja.
Unakuta kuanzia nje mpaka ndani ugumu tu unatawala kuanzia kupatikana tiketi za kuingilia uwanjani, ulinzi wao nao unakuwa mashakani kwani wale wanaopewa jukumu la kuwalinda wanakuwa wababe yaani shabiki hana amani anakuwa mtumwa tena.
Mpaka ataingia uwanjani amepitia mechi nyingi za shida ambazo zinamfanya akimaliza kushangilia asifikirie tena kurudi uwanjani kwani anajua ni tatizo tu akiwa ndani ya uwanja.
Endapo maboresho yatafanyika itakuwa vizuri na itaongeza morali ya mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani jambo ambalo litafanya mwaka huu uwe tofauti na ule uliopita.
Kila la kheri U 17 kwenye maandalizi ya kuelekea mechi yenu ya marudio nina imani hamtatuangusha watanzania nasi tunawaombea kila lililo jema.







0 COMMENTS:
Post a Comment