February 9, 2020

MBWANA Samatta ni mzawa kutoka Mbagala iliyopo Tanzania anayetoa somo kwa wachezaji wengi wenye shauku ya kufikia mafanikio kupambania ndoto zao.

Kwa sasa anakipiga kwenye moja ya timu kubwa ambayo inashiriki Ligi Kuu England ligi ambayo ni namba moja kwa ubora na inafuatiliwa na watu wengi duniani.

Mashabiki wa Tanzania nao tayari wameonyesha kwamba wapo pamoja naye kwenye kila hatua ambayo anaipitia kwa kumuombea dua pamoja na Baraka kutoka kwa Mungu.

Yote ni mema na ikumbukwe kwamba Samatta hakuibukia ghafla hapo ndani ya Aston Villa bali alipambana kwa moyo mmoja kutafuta mafanikio yalipojificha.

Stori yake akikusimulia kutoka mwanzo unaweza usiamini ila mwisho wa siku aliamini kile anachokifanya na mwisho wa siku yupo hapo alipo.

Alianza kupambania ndoto zake peke yake na ulimwengu wake mwenyewe achana na Thomas Ulimwengu.

Kwa sasa ameonekana na marafiki wengi ambao wanamfuatilia ni asili yetu na haiwezi kupotea kusapoti yale ambayo yamekamilika bila kujua kwamba yametokea wapi hakuna namna ni lazima tuendelee na utamaduni wetu.

Mapito yake alipokuwa Mbagala Market yeye mwenyewe anatambua kipi alikuwa anakifikiria na mwisho wa siku amefanikiwa kutimiza ndoto zake.

Samatta akiwa Mbagala Market ambayo kwa sasa ni African Lyon mwalimu wake anaeleza kuwa alikuwa na ndoto ya kufikia mafanikio na kucheza mbali.

Hata yeye mwenyewe alieleza kuwa miongoni mwa ndoto kubwa ya muda mrefu ilikuwa ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Akiwa Simba pia alipambana licha ya kutokuwa na jina kubwa aliamini kwenye uwezo wake na aliweza kuigomea timu yake kucheza mpaka apewe yale ambayo aliambiwa atapewa kabla ya kujiunga na timu hiyo.

Mpaka alipokamilishiwa mahitaji yake ndipo akaendelea kucheza jambo ambalo kwa wachezaji wa sasa ni gumu kidogo kufanyika na hatujaskia habari hiyo kwa wazawa zaidi ya wageni.

Alipotua Congo kuitumikia timu ya TP  Mazembe hakuonyesha uzembe aliendelea kukipiga kwa moyo mmoja akiamini kuna kitu ambacho anakitafuta na leo ameshafikia hatua ya kuwa mfano.

Genk ya Ubelgiji hawakuwa na hiyana walimvutia kasi na kumpa nafasi mwisho wa siku akatwaa ubingwa na aliweza kuifunga timu bora ya Liverpool Uwanja wa Anfield.

Yote haya anayofanya nyuma yake mashabiki wa Tanzania walikuwa nyuma yake wakimpa sapoti wakiamini kwamba kijana wao anaiva na anaendelea kuwa bora.

Kwa sasa amesajiliwa na Aston Villa timu ambayo inashiriki Ligi Kuu England na ameshacheza mechi mbili na kuweka rekodi zake za mwanzo kabisa.

Samatta ameingia kwenye kikosi cha kwanza jumlajumla na alianza kuonyesha uwezo wake mbele ya Leicester City mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Carabao ambapo ilishinda kwa mabao 2-1.

Pia ikumbukwe kuwa Samatta alitumia dakika 65 kucheza mchezo wake wa kwanza kabla ya kuomba kutoka kutokana na kuchoka.

Kocha wake Dean Smith alisema kuwa anahitaji muda kidogo ili awe bora na anapaswa kuongeza juhudi kwani ligi ya England si ya mchezo.

Kocha anaamini uwezo wa mchezaji wake Samatta ndio maana anampa nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake kinachopambana kisishuke daraja na kinahitaji kutwaa Kombe la Carabao.

Tukiachana na yote sasa kumekuwa na wimbi la mashabiki ambao wanaongea na mabosi wa timu ya Aston Villa wakionyesha ubaguzi.
Jambo hili sio sawa kwani linamjengea taswira ya tofauti Mbwana kwenye maskani yake mpya.

Na kwa namna ilivyo hawa jamaa wanavyofuatilia mambo kwa ukaribu itakuwa ngumu kwa wengine kupata nafasi kutokana na kosa hili la mashabiki.

Mashabiki wanapenda kumuona Samatta anafunga hata yeye anapenda kufunga ila huwa haiwi mara zote ukiwa uwanjani unafunga.

Ikumbukwe kuwa kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England Samatta alifunga bao lake la kwanza na kuingia kwenye rekodi ya mtu kutoka nchi ya 99 kufunga bao ndani ya ligi.

Hapa inaonyesha kwamba hawa jamaa zetu wanafuatilia kila jambo hebu fikiria kwenye ligi yetu ya Bongo kuna rekodi za mataifa ambayo yamefunga ndani ya ligi yetu?

Jibu ni moja tu taarifa hizo na mabao ya mataifa hayo hayapo na ukianza kuyafuatilia utapasuka tu kichwa kwa kuwa bado hatujaingia kwenye mfumo huo.

Hivyo kila kitu kwa wenzentu ni rekodi tunachotakiwa ni kumpa sapoti na kutomchafulia kijana wetu hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Leo hii ukiingia kwenye ukurasa wa Instagram wa Aston Villa kuna utawala wa watu kutoka Bongo nguvu yenu inaonekana na uwezo upo ila kile mnachokifanya sasa ni hatari kwa Samatta.

Lugha ambayo inaandikwa ni moja kwa moja kwamba Samatta anabaniwa na wachezaji wenzake jambo ambalo halina hoja na hakuna data.

Unapozungumzia mpira ni mchezo wa data ndio maana kwenye kila kinachofanyika wenzetu wanarekodi kisha wanakuja na tathimini.

Kwetu sisi ni nani ambaye ana rekodi za Samatta kunyimwa pasi na wachezaji wenzake? Jambo hili tulichukue kwa utofauti na kuamua kumpa sapoti kijana wetu bila kushusha matamko mabaya kwenye ukurasa wa Villa.

Kila mmoja ana Uhuru wa kutoa maoni yake kupitia kurasa za mitandao ya kijamii na viongozi wakafanyia kazi kwa umakini endapo kutakuwa na tija la kama hakuna tija basi ni suala la kuachana na hayo mambo.


Jack Grealish nyota wa Aston Villa amekuwa midomoni mwa mashabiki wa Tanzania wakimtaja kwamba ni mchoyo na ana roho mbaya kwa Samatta kwa kuwa hampi pasi.

Sina imani kama hili linawezekana kwa timu ambayo inatafuta matokeo na inajua kwamba mchezaji fulani ana nafasi ya kufunga akanyimwa pasi hakuna kitu kama hicho duniani kote.

Tunapaswa kutumia busara na kuangalia ni kwa namna gani Samatta anapaswa azidi kuimarika taratibu hasa ikiwa ni maisha yake mapya ndani ya Aston Villa na kazi yake ni kubwa kuinyanyua timu.

Kulaumu sio jambo jema kutokana na ukweli kwamba Engaland sio sawa na Bongo kwamba kila shabiki ana nafasi ya kushauri na akakubalika.

Tusisahau kwamba Grealish anahusika katika kupiga pasi iliyoleta bao la kwanza kwa Samatta ndani ya Ligi Kuu England, anahusika kwa kumpa Samatta pasi  ambayo alikosa bao la wazi dhidi ya Leicester City.

Kwa hapa pia bado mnamshushia lawama Grealish kutokana na pasi anazotoa na uwezo wake ambao anao hilo bado halipo sawa.

Rekodi zinaonyesha kuwa Grealish kapiga jumla ya pasi 800 zilizofika ana asisti 5 na mabao 7. Si kweli anamyima pasi Samatta na vizuri tuwe na takwimu wakati tunalaumu.

Basi tumuache Samatta afanye kazi lawama kwa Aston Villa tuzipuuze na kuendela kumuombea dua kwa sasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic