NA MWANDISHI WETU
TIMU ya soka ya waandishi wa habari, Taswa FC, inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Benki ya Stanbic Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
Mchezo huo utaambatana na hafla fupi ya kufahamiana na kuimarisha uhusiano baina ya wanahabari na wafanyakazi wa Benki ya Stanbic.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Stanbic, Desideria Mwegelo, alisema wamefikia uamuzi wa kucheza mchezo huo na Taswa FC kutokana na kufahamu uhusiano wao mzuri na wanahabari.
“Wanahabari ni sehemu muhimu mno katika jamii hivyo sisi kama Stanbic Bank, tumeona kuna umuhimu wa kukutana na hawa wenzatu kupitia tukio hili la mechi ya soka ya kirafiki ili kufahamiana zaidi, kubadilishana mawazo na kuimarisha uhusiano baina yetu,” alisema.
Alisema timu yao ya soka ipo fiti ikiwa inafanya mazoezi ya nguvu kujiandaa na mchezo huo, wakiamini pia utasaidia kuimarisha afya za wachezaji wa pande zote mbili.
Alisema baada ya mchezo huo, wachezaji wa timu zote, wafanyakazi wa Stanbic Bank na wanahabari watakaojitokeza kuishangilia timu yao, watakusanyika pamoja katika hafla ya kuukaribisha mwaka 2020.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omari, aliishukuru Stanbic Bank kwa kuwakumbuka, akiahidi soka maridadi katika mchezo huo.
“Tunawashukuru sana Stanbic Bank kwa kutufikiria sisi Taswa FC kucheza nao mechi ya kirafiki, tukiamini ushirikiano huu utakuwa endelevu kwa manufaa ya pande zote mbili,” alisema.
“Niwaombe wanahabari kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam siku hiyo ya Jumamosi ili kuipa sapoti timu yetu ya Taswa FC, tukiwaahidi hatutawaangusha, lazima tutawafunga Stanbic FC,” alisema Majuto.
Naye nahodha wa Taswa FC, Wilbert Molandi, alisema kikosi chao kimekuwa kikifanya mazoezi makali kwenye Uwanja wa Bora uliopo Sinza, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo, hivyo Stanbic FC wajiandae kupokea kipigo kitakatifu.
“Hii mechi tumeisubiri kwa muda mrefu na sasa wakati umefika wa kuwathibitishia Stanbic Bank kuwa Taswa FC ni moto wa kuotea mbali, hivyo wanahabari wote wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Gymkhana Jumamosi ili kupata burudani ya nguvu,” alisema.
Tayari Benki ya Stanbic imeshaikabidhi Taswa FC jezi kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa aina yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment