JONAS Mkude
kiungo mkali wa Simba wiki iliyopita aliendelea kugonga vichwa vya habari
kuhusiana na nidhamu yake.
Inawezekana
wengi wamesahau lakini ukweli ni kwamba kiungo huyu amekuwa na mwendelezo wa
utovu wa nidhamu kwa baada ya hivi karibuni kushindwa kuungana na wenzake
kwenye kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars.
Jina la
kiungo huyo lilikuwa kati ya wachezaji 35 walioitwa Stars na kocha wa kikosi
hicho, Etienne Ndayiragije lakini wenzake walijiunga na baadhi walitoa taarifa
kutokana na kuzuiwa kutoka sehemu waliyopo kutokana na mlipuko wa Virusi vya
Corona, hao wengi ni wale wa kimataifa.
Nakumbuka
pia wakati fulani aliitwa timu ya taifa na Kocha Emmanuel Amunike, yeye pia
alionekana kulalamikia nidhamu za baadhi ya wachezaji kuwa hawakwenda kambini
huku wakishindwa kutoa sababu za msingi akiwemo Mkude japokuwa kocha hakumtaja
hadharani.
Lakini
kumbuka kiungo huyo, miezi iliyopita hakusafiri na timu yake ya Simba akiwa sambamba
na wachezaji wenzake, Clatous Chama, Erasto Nyoni na Gadiel Michael kwenda
kucheza mechi za Kanda ya Ziwa ambazo ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar na Biashara
United.
Lakini akiwa
bado anahojiwa juu ya suala hilo, timu iliporudi Dar es Salaam kuendelea na
maandalizi ya mechi kuna siku akachelewa kwenye mazoezi ambayo yalikuwa
yanafanyika Viwanja vya Gymkhana, Posta jijini Dar.
Hii si mara
ya kwanza kwa kiungo huyo kukumbwa na matukio ya utovu wa nidhamu, licha ya
kuwa amekuwa na mchango mkubwa kikosini humo na ndiye mchezaji mkongwe Simba,
nafikiri anahitaji msaada wa kuwekwa sawa.
Mkude ambaye
amewahi kuwa nahodha wa Simba kabla ya kupokwa na kupewa John Bocco, ni role
model wa vijana wengi mtaani ambao wanachipukia sasa kwa hiki anachokifanya
sasa hivi siyo sawa kabisa, anapaswa kubadilika.
Ifikie
wakati wachezaji wanapaswa kujulishwa umuhimu wa kuitumia timu ya taifa hasa
kwa wale wenye ndoto za kucheza soka la kulipwa nje.
Ni ngumu
kama malengo yako ni kucheza nje kupuuzia kuichezea timu yako ya taifa kwani moja
kati ya vipengele wanavyoangalia ni nafasi yako kwenye timu ya taifa sasa kama
wewe unaona sasa hivi huna mpango na taifa lako andika umeumia.
Hii siyo kwa
Mkude tu ni kwa wachezaji wote Tanzania, hili ni somo inawezekana wengi
hawajui, lakini ukweli ndiyo huu.
Sasa matukio
kama haya ukiangalia yanaripotiwa kwenye vyombo vya habari hivyo inapotokea
anahitajika kwenda kucheza soka la kulipwa inaweza kumpa shida kidogo kwani
klabu nyingi Ulaya zimekuwa zikizingatia nidhamu ya hali ya juu.
Mkude bado
ni kijana mdogo, taifa na klabu yake ya Simba bado zinahitaji huduma yake
katika kuhakikisha soka letu linapiga hatua.
Hii kwa
wote; Nidhamu ni muhimu sana kazini. Starehe zipo, fanya kwa wakati wako lakini
linapokuja suala la kazi basi fuata misingi ili usipotee.
Kama leo
ligi zimesimama kutokana na mlipuko wa Virusi vya Corona basi wachezaji
mzingatie suala la mazoezi ili kudumisha viwango vyenu, uzuri mchezo wa soka
unachezwa wazi hivyo ni vyema mkaendelea na mazoezi sehemu ambazo hazina hatari
ya kupata maambukizi hayo.
Kila mmoja
akili kichwani mwake, najua wapo ambao wanaendelea na matizi na wapo ambao
wanakaa tu wakisubiri ligi zirudi, siyo sawa linda kipaji chako kwa kufanya
mazoezi.
0 COMMENTS:
Post a Comment