LIGI Daraja
la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) misimu yake kwa mwaka huu
inaelekea ukingoni.
Ukitazama SDL zimebaki raundi mbili kumaliza msimu, wakati
FDL raundi tano zimebaki msimu kumalizika.
Kuna baadhi
ya timu tayari zimejiweka karibu sana na kupanda daraja, hapa nazungumzia FDL
ambapo Kundi B, Gwambina FC inaongoza, katika mechi tano inahitaji pointi sita
tu kupanda moja kwa moja.
Huko chini
vita bado ipo, timu zinapambana kuepuka janga la kushuka daraja. Tusubiri hadi
mwisho itakuwaje.
Wakati FDL
na SDL mambo yakiwa hivyo, Ligi Kuu Bara nayo inazidi kushika kasi. Tumeona
juzi Yanga iliyotoka kuifunga Simba bao 1-0, nayo imekuja kukubali kichapo kama
hicho kutoka kwa KMC.
Ukiangalia
matokeo hayo ni kama ya kushtua kwani haikutarajiwa KMC ambayo ilikuwa nafasi
ya 18 kabla ya mchezo huo, itakuja kuibuka na ushindi mbele ya Yanga
inayopambana kuikimbiza Simba kileleni.
Lakini kwa
wanaofahamu vizuri soka, wanatambua kwamba kuna matokeo ya aina tatu. Kushinda,
kufungwa na sare.
KMC
inapambana kujinasua kutoshuka daraja, hivyo ilikuwa na namna ya kufanya ili
kushinda mchezo huu ikiwemo na michezo mingine ili tu isikumbane na janga hilo.
Kwa wakati
huu ambao msimu wa ligi hiyo upo mzunguko wa pili kuelekea kuumaliza, tunaweza
kushuhudia mengi kwa timu mbalimbali.
Hakuna timu
ambayo inataka kushuka daraja, hivyo kila moja inapambana kuona inajinasua na
hayo matatizo.
Timu
zinafahamu kwamba kushuka daraja ni hatari kwani kuja kurudi inaweza kukuchukua
muda mrefu sana.
Itazame Toto
Africans, tangu iliposhuka daraja msimu wa 2016/17, hadi leo haijapanda na
inazidi kushuka tu.
Hivi sasa ipo Ligi Daraja la Pili na huko kuna hatari
ikaenda na maji tena.
African
Sports ya Tanga nayo ipo Ligi Daraja la Pili. Kama utakuwa unakumbuka nayo
ilikuwa ligi kuu na katika msimu wa 2015/16, zilishuka timu zote tatu kutoka
Tanga. Coastal Union, Mgambo Shooting na African Sports.
Katika timu
hizo, Coastal Union pekee ndiyo imeweza kuirudi Ligi Kuu Bara, zilizobaki zipo
madaraja ya chini zikiendelea kupambana.
Hata ukiiangalia
Stand United ambayo msimu uliopita ilishuka daraja, inapambana pia huko FDL
ambapo inaonekana inaweza kushuka tena.
Hivyo kwa mifano hiyo, ndiyo maana
tunaona hivi sasa timu zikipambana kweli, hazitaki kushuka daraja.
Wito wangu
kwa wahusika kwa maana ya wanaosimamia ligi, kuisimamia kwa ukaribu hasa dakika
hizi za mwisho kwani kuna malalamiko kwa baadhi ya timu kwamba kuna timu
zinapendelewa.
Niliwasikia
Ihefu wakilalamika kwamba mechi zao na zile za Dodoma Jiji FC zimekuwa
zikichezwa siku tofauti wakiomba zichezwe siku moja ili kukwepa upangaji
matokeo.
Timu hizo
ambazo zipo kileleni mwa msimamo wa Kundi A katika FDL. Hivyo wadau wanataka
kuona kinara akipatikana si kwa kuandaliwa.
Cha
kupendeza zaidi ni kwamba mechi zao za wikiendi hii zinachezwa siku moja. Leo
Jumamosi Dodoma Jiji inacheza na Njombe Mji, wakati Ihefu ikipambana na Boma.
Nadhani hapa hakutakuwa na vilio tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment