March 3, 2020


FEBRUARI ndo imeshameguka kwa kasi kisha mwezi Machi upo kwa hewa ndipo tutaukaribisha mwezi Aprili ambao unatarajiwa kuwa na tukio kubwa kwenye ulimwengu wa soka ndani ya Bara la Afrika.
Michuano hii ni muhimu pia kwetu kwani inatuhusu kwa asilimia kubwa kutokana na timu yetu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kukata tiketi ya kushirki michuano hiyo.
Hapa nazungumzia michuano ya CHAN inayotarajiwa kufanyika nchini Cameroon na Tanzania pia tutakuwepo ndani ya michuano hiyo tukiipeperusha bendera yetu.
Tumepangwa kundi D lenye timu za Guinea, Zambia na Namibia sio kundi jepesi kwa kulitazama ila kwa kupambana inawezekana na timu ikapata matokeo mazuri kwenye mechi itakazocheza.
Ninawaamini vijana wetu wana uwezo mkubwa wakiwa ndani ya uwanja hasa linapokuja suala la kutumikia Taifa lazima utawapenda kila mmoja anaonyesha juhudi na kufanya kile anachokipenda kwa moyo wake wote.
Ningependa iwe hivyo hata kwa mashabiki nao waendelee kuipa sapoti timu ya Taifa kwa watakaoweza wajiunge pia nchini Cameroon kuishangilia timu yao.
Sasa kinachotakiwa kufanyika kabla ya hiyo Aprili ni maandalizi mapema kabla ya kwenda kushiriki kwani kila kitu kinahitaji maandalizi ikishindakana kwenye maandalizi itashindikana pia kwenye matokeo.
Shirikisho la Soka Tanzania hapa lina kazi kubwa na ya msingi kutazama ni namna gani Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ambaye ni Ettiene Ndayiragije atapata muda wa kukaa na wachezaji wake atakaowachagua.
Ukweli upo wazi kwa sasa kumekuwa na mashindano mengi ambayo yanawafanya wachezaji wengi kuwa bize kutimiza majukumu yao na wana kazi pia ya kutimiza majukumu ya taifa jambo ambalo linaleta ugumu kidogo.
Ukitazama mwezi wa Februari kuna timu ambazo zilicheza mechi zao za ligi pia kuna nyingine zilicheza mechi za Kombe la Shirikisho na kwa sasa mchakamchaka unaendelea mwezi Machi..
Stand United ilifungashiwa virago na Simba kwenye hatua ya 16 bora na ushindani ulikuwa mkubwa hata Yanga pia walipenya mbele ya Gwambina kwa ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru.
Kwa namna ratiba ilivyo inaonesha ni namna gani kwamba muda umekuwa mdogo na maandalizi yanahitaji muda.
Ratiba ya Ligi Kuu Bara nayo inazidi kukata mbunga kwa kasi ikiwa ni mzunguko wa pili tunaona timu zinapambana kutafuta matokeo ni jambo la msingi.
Wito wangu kwa TFF kufanya uchunguzi na kufanyia kazi namna ratiba ilivyo kwa kutoa wiki mbili  za maandalizi kwa timu ya Taifa ambayo ina kibarua kikubwa mwezi Aprili.
Kuna namna ambayo inapaswa ifanyike kwa sasa ili kuwe na maadalizi mazuri kwa timu ya Taifa  ya Tanzania na itafanya tuwe na uwezo wa kupata matokeo kwenye mechi zetu za kimataifa tutakazocheza.
Timu inahitaji wiki mbili hata zaidi kwa ajili ya kufanya maandalizi na hii itasaidia kupata timu yenye muunganiko mzuri ambao hautasumbua wachezaji kutafuta matokeo kwenye mechi watakazocheza.
Maandalizi yasipokuwa imara itasababisha timu ishindwe kufikia malengo na kuwafanya wachezaji kucheza wakiwa hawana maelewano.
Kwa kuwahi kambini kutatoa nafasi kwa wachezaji kupata muda wa kuzoeana na kutambua aina za uchezaji ambazo zitawasaidia kupata matokeo kwenye mechi watakazocheza.
Imani yangu nafasi ikiwa kubwa kwa mwalimu kukaa na wachezaji wake ambao atawateua timu italeta ushindani na itakuwa kwenye ubora ambao wengi hawataamini kuona wanachokiona uwanjani.
Tuna timu nzuri hilo lipo wazi kutokana na kuwa na aina ya wachezaji wengi wanaobebwa na juhudi zao binafsi pamoja na usikivu ndani ya uwanja.
Miongoni mwa ligi ndani ya Bara la Afrika ambazo ni ngumu huwezi kuacha kuitaja ligi ya Bongo kutokana na mfumo wake ulivyo kwa sasa na namna ambavyo kila timu inapambana kupata matokeo.
Tumekuwa tukipata tabu tunapocheza na timu jirani za Afrika Mashariki kama Kenya, Uganda kwa kuwa kuwatumia wachezaji wao ndani ya timu zetu ni kitu kinachofanya tujione kwamba hatuna ligi ngumu ila ukweli ni kwamba tuna ligi ngumu.
Timu nyingine za Kenya zinaiba mbinu zetu kwa kuwa wana uzoefu nasi na wale ambao wamecheza kwa muda mrefu wanatambua falsafa ya timu zetu.
Ukitazama timu zile za nje ya Afrika Mashariki tukikutana nazo zimekuwa zikipata ushindani mkubwa kwani wachezaji wetu walikuwa wanawasumbua wachezaji wa kigeni bila mashaka.
Hii yote inatokana na wachezaji wetu kushiriki ligi ngumu na kupenda kujifunza kila siku ni jambo ambalo linavutia na inawezekana kuwa bora muda wote.
Imani yangu mwalimu akipewa wiki mbili zitamfanya awe na muda wa kutosha kujua falsafa za kikosi chake na wachezaji atakaokuwa nao kitu hicho kitampa nguvu ya kuandaa kikosi kazi kitakachofanya vizuri ndani ya CHAN.
Ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi na kila kundi lina ugumu wake ila mwisho wa siku ni kwamba timu inahitaji matokeo ambayo yatawapa nafasi ya kusonga mbele.
Kila timu ina nafasi iwapo itajipanga vema kwenye hatua ya mwanzo kabla ya mashindano kwani inapofika kushiriki hakuna muda wa kujiaandaa tena.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic