March 2, 2020





Na Saleh Ally
MWANADAMU huwa ni lazima akosee na unapopunguza idadi
ya makosa hadi kuwa machache sana, utapewa jina moja, mtu makini.

Kujikita na kuhakikisha makosa katika jambo unalolifanya
hayawi makubwa sana nako kunahitaji muda wa kutosha,
kusimamia kwa ukaribu, kukagua kitu husika na kadhalika.

Suala hili la usimamizi wa karibu, limetushinda wanadamu wengi. Hadi imefikia baadhi wamekuwa wakifanya makosa kama ndiyo jambo la kawaida kabisa na kukosea wanataka kuweka uthibitisho kuwa wanadamu wanatakiwa wafanye hivyo.

Kama nilivyoandika makala kuhusiana na kuwaeleza Yanga
kwamba tuwaambie ukweli kwa kuwa tunataka wabadilike.
Tusiwafiche na tusione haya au aibu kusema kikosi cha Yanga bado hakipo vizuri sana.

Kikosi cha Yanga bado kinataka kuboreshwa lakini waliopo, nao wanatakiwa kucheza kwa juhudi zaidi ili kuipa haki klabu yao kwa kuwa ina mashabiki wengi wanaoumia wakitamani kuiona inafanya vizuri.

Kama Yanga haifanyi vizuri, basi kuna sehemu kunaweza kukawa na nafuu kwa wachezaji wake kuonyesha juhudi zaidi na maarifa ya juu ili kuwa sehemu ya msaada. Haya niliyaeleza

katika makala yaliyopita. Leo napigilia msumari, nataka kuwakumbusha Yanga kuwa wamesajili wachezaji wa kigeni zaidi ya 10 katika msimu huu na unaona wengi wao wakaonekana hawafai.

Hawafai kutokana na mambo mawili, inawezekana haraka za viongozi kwa hofu ya mashabiki wakaamua kuachana nao au wako waliosajiliwa kwa ajili ya maslahi ya baadhi ya watu ndani ya klabu, leo wamekuwa mzigo katika kikosi.

Baada ya msimu wa 2018/19 kwisha, maandalizi ya msimu wa 2019/20 yalianza na sehemu kubwa huwa ni usajili. Umeona Yanga imepoteza mamilioni kusajili wachezaji wengi ambao lilipofika dirisha dogo wakaachwa na tayari ikaonekana hawana msaada au hawafai na kuachwa.

Baada ya dirisha dogo, usajili mpya wa Yanga nao umeonekana haukuwa na tija, maana yake hakukuwa na
majuto au kujifunza kutokana na makosa ya mwanzo wa msimu. 

Tujiulize, nani anashughulikia usajili wa Yanga hadi asajili na kusababisha makosa yanayofanana ndani ya vipindi viwili vya usajili katika msimu mmoja.

Kama unakumbuka, Issa Bgirimana kutoka Rwanda aliachwa wakati wa dirisha dogo akifuatana na Juma Balinya, Mganda aliyekuwa mfungaji bora Uganda. Alikuwepo Sadney Urikobh, Mnamibia huyu, naye akaondoka lakini Mzambia Maybin
Kalengo naye akaachwa.

Wachezaji wa kigeni wanne ndani ya miezi minne wanaonekana hawafai, si kitu kizuri. Kama watu wako makini hii ni kashfa ya matumizi mabaya ya fedha. Na katika hali ya kawaida unategemea kuiona Yanga iliyojifunza. Wakati hao wanaachwa, unategemea kupata makali ya uhakika kuonyesha Yanga ilijuta kutokana na makossa iliyopitia. 

Lakini inakuwa ni kazi bure kabisa kwa kuwa usajili uliokwenda kufanyika, umekuwa hauna tofauti kubwa na ule ulionekana ni tatizo.

David Molinga, sasa anaongoza kwa kufunga mabao saba lakini unaona amekuwa akikaa jukwaani kabisa na kocha Luc Eymael anamuona hawezi. Ukiachana na Mkongo huyo, Yikpe Gnamien raia wa Ivory Coast pamoja na kukubalika na kocha huyo, bado anaonekana kuwa hana faida sana na bado hata yeye mara nyingi anamuweka benchi, anaingia ‘usiku’. 

Usajili wenye faida ambao bila shaka kila mmoja anaweza
kusema “yes” ni Bernard Morrison, raia wa Ghana ambaye
ameonyesha kweli ni msaada hasa Yanga na Haruna Niyonzima ambaye amerejea na hakuna anayeweza kujisifia kwa sasa aliona kipaji chake.

Tukubaliane usajili wa wachezaji wa kigeni unahusisha fedha nyingi haaa wakati wa usajili. Bila ya ubishi, wako wamekuwa wakichuma wakati huo wa usajili, ikiwezekana kwa kuongeza bei.

Klabu inakuwa inaingia gharama kubwa ambazo baadaye zinakuwa mzigo, hata kama ilikopwa, baadaye ndiyo inahangaika kwa madeni. Kuwa na madeni bila faida ni kutokuwa makini ni kuwa mtu unayerudia makosa mara kwa mara maana yake ni uzembe.


Hivyo Yanga inapaswa kulisimamia hili na kumaliza uzembe huu kwa faida na manufaa mapana ya klabu yenyewe. Kwenye sehemu yenye watu wengi, kuna mengi na kama uongozi utashindwa, basi utatutia hofu wadau kwamba kuna walakini.

Lazima kuwe na wataalamu sahihi, washirikiane na benchi la ufundi na wao pia wanapaswa kuhojiwa ili anaposajiliwa mchezaji, kuna na uhakika wa mambo angalau kwa asilimia 90, hata akitokea amefeli, basi kuwe na sababu ya msingi ya
kiuanamichezo na si hafai tu, klabu inasajili mwingine naye anaingia anakuwa hana msaada.


Klabu kubwa kama Yanga, haiwezi ikawa inaendeshwa kwa bahati mbaya “mlima”. Umakini wa kufanya mambo kwenda sahihi unahitajika, lazima kuwe na umakini katika utekelezaji la sivyo Yanga itaendelea kuumia kwa hasara na matumbo ya
wachache yakifaidika wakati wengi wakiwa wanaumia mioyo

kutokana na mapenzi na klabu hiyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic