UKIUTAZAMA msimamo wa Ligi Kuu Bara, timu nyingi zimecheza mechi 24, huku chache zikicheza 23 katika kuelekea kuumaliza msimu huu wa 2019/20 ulioanza Agosti, mwaka huu kwa kuzishirikisha timu 20.
Hivi sasa timu zinapambana kwa namna yoyote ile kufikia malengo yao ambayo walijiwekea mwanzoni mwa msimu huu.
Kila timu imekuwa na malengo ya kuwa bingwa katika mashindano inayoshiriki, hakuna hata siku moja ukamsikia kiongozi au mchezaji wa timu fulani akisema kwamba wanashiriki kwa ajili ya kuwasindikiza wenzao, lazima waweke malengo yao.
Katika malengo makubwa, ni kutwaa ubingwa ingawa kuna timu zingine zinasema kwamba katika msimu wake wa kwanza wa ligi kama ndiyo imepanda, inataka kwanza kuhakikisha haishuki, kisha msimu unaofuata ndiyo kuwania ubingwa.
Huwezi kufanya jambo kama hauna malengo, weka malengo kwanza, ndipo anza jambo lako kuhakikisha unafikia malengo yako, ukifeli utakuwa na sehemu pa kuangalia ili kutatua tatizo.
Nikiwa naizungumzia Ligi Kuu Bara ambayo inakwenda kwa kasi huku mzunguko wa pili ndiyo ukielekea ukingoni katika kukamilisha msimu, nazikumbusha timu cha kufaya kipindi hiki.
Ukiangali ni wazi kuna baadhi ya timu kama zimekata tama ya kuwepo tena msimu ujao wa ligi hiyo.
Hiyo inakuja kwa sababu msimu ujao zinatakiwa timu 18 kutoka 20 zilizopo hivi sasa. Ili kuzipata timu hizo 18, msimu huu zitashuka daraja timu nne.
Timu hizo nne zinashuka moja kwa moja ambazo ni zile zitakazoshika nafasi ya 17, 18, 19 na 20. Kisha zile zitakazoshika nafasi ya 15 na 16, zitacheza mechi za mtoano na timu mbili kutoka Ligi Daraja la Kwanza katika kulinda nafasi zao, zikipoteza nazo zinashuka, kisha zile zilizoshinda zinaopanda.
Kumbuka hapo kuna timu mbili kutoka Ligi Daraja la Kwanza zilizoongoza makundi yao kati ya yale makundi mawili zitakuwa zimepanda daraja moja kwa moja na kuziacha zitakazoshika nafasi ya pili na tatu kucheza mechi za mtoano.
Kushuka timu nne ndiyo kumekuwa kukiwaumiza wengi hasa makocha na wachezaji wa timu ambazo hivi sasa zipo kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Leo Jumamosi ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kwa kuchezwa mechi tisa katika viwanja tofauti, mwendelezo wa ligi hiyo utazidi kutoa picha halisi ya timu gani zitashuka daraja.
Msimamo unaonyesha timu zinazoshika zile nafasi nne za kushuka daraja moja kwa moja ni Mwadui, Mbao, KMC na Singida United, wakati Mtibwa na Mbeya City zikiwa kwenye mstari wa timu zitakazocheza mechi za mtoano.
Bado kuna takribani mechi 14 kabla ya msimu kumalizika, hivyo mechi hizo zenye jumla ya pointi 42, zinaweza kubadilisha kila kitu.
Usishangae timu ambayo hivi sasa inaburuza mkia ya Singida United, ikafanya mapinduzi ya kweli na kutoka huko ilipo, ikapanda juu zaidi na kujinasua na hili janga la kushuka daraja.
Lakini hilo haliwezi kutokea kama miujiza, ni lazima wachezaji, benchi la ufundi, viongozi wa timu na mashabiki wakaungana kwa pamoja kuhakikisha ushindi unapatikana katika mechi hizo.
Ikienda kinyume na hapo, hamtakuwa na budi na kujiandaa na maisha ya Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
0 COMMENTS:
Post a Comment