BADO dunia ipo kwenye giza nene
kutokana na ugonjwa wa COVID19 wa Virusi vya Corona ambao
unaendelea kuitikisa dunia kwa kasi na nchi zikipoteza maelfu ya watu kila
kukicha na wengine bado hali mbaya wapo vitandani wakipigania maisha yao
kutokana na janga hili.
Hakuna asiyejua
nini kinaendelea kwa dunia ya sasa Virusi vya Corona vimekuwa
vikimaliza watu bila kuchagua huyu ni nani wala yule ni nani ukipata unakwenda
hasa kama utashindwa kujitokeza kwa ajili ya kupewa huduma za afya.
Kwenye soka tayari
tumeshuhudia viongozi wa klabu za soka hasa huko Ulaya wamefariki na
Virusi vya Corona ambavyo ni tishio kila kona ya dunia
hata hapa Tanzania.
Tanzania ni nchi kubwa ambayo
ina wakazi wengi waliopo mjini na vijijini lakini licha ya janga hili la Virusi
vya Corona baadhi ya maeneo bado hawajapata elimu
kuhusu janga hili.
Kama inavyofahamika
soka ni burudani wakati huu ni muafaka kabisa kwa wachezaji na klabu
kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanakuwa wa kwanza kutoa
elimu kwa jamii zinazowazunguka kuhusiana na virusi vya Corona.
Tunaamini wao ni watu ambao
wanafahamika na kuwa karibu na jamii kupitipia vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii kipindi kama hiki wanatakiwa kutoa elimu na wakati mwingine
hata kuzunguka kwa tahadhari na kuwaelimisha watu juu janga hili ili kuepusha
vifo kama ilivyo Ulaya.
Kutokana na hali
ilivyo kuna ambao watakuwa na uwezo wa kuichangia jamii vifaa kwa ajili ya
wagonjwa na wengine watakuwa hawana uwezo huo, lakini elimu ni bure mnaweza
kutoa elimu hiyo kwa jamii ambayo imekuwa ikiwazunguka kwa wakati wote.
Hakika hakuna
kinachoshindikana naamini wale mastaa wa Simba, Yanga, Azam, Ndanda, Mtibwa,
Mbeya na Namungo na wengine hasa walioko mjini watatakiwa
kupita hata vijijini kuendelea kuielemisha jamii kuhusu Virusi vya
Corona kwa asilimia 50 elimu mjini imetolewa zaidi.
Hivyo
wachezaji naomba mjitokeze katika hili kwa kurudisha fadhila kwa
jamii ambayo inawazunguka kwa kutoa elimu juu ya Virusi vya Corona kwa
manufaa ya vizazi vyetu pamoja na uchumi wa nchi kwani Virusi hivi
vikisambaa kwa kasi vitapoteza nguvu kazi ya watu.
0 COMMENTS:
Post a Comment