Na Saleh Ally
HAKIKA maisha yanabadilika kwa kasi kubwa na ukitaka kuishi kwa
amani katika kipindi hiki lazima ukubaliane na hali halisi ilivyo.
Hakuna ubishi tena kwamba ni lazima uishi katika kipindi hiki
ukiamini Corona ni tatizo na lazima kuwe na tofauti ya maisha na yale kabla ya
kuibuka kwa Covid 19 ambayo sasa inaitikisa dunia.
Watanzania wapenda michezo, nao wanalazimika kuishi katika aina
mpya ya maisha ambayo bila shaka ni kero, maumivu na manung’uniko ya
kutofurahia hali.
Michezo yote ilisimamishwa, si Tanzania pekee au Afrika pekee
badala yake ni dunia nzima. Kawaida ya wanamichezo wanaishi dunia nzima, ndiyo
maana mara zote utasikia mtu anauliza hivi, hapa nyumbani unashabikia timu
gani, nje pia timu gani?
Maisha ya wapenda michezo au soka, ni hapa nyumbani na nje.
Hivyo kufungwa kwa michezo hapa nyumbani lakini hata huko nje kwao inakuwa ni
kama jela hivi. Hakuna kinachoendelea kawaida kwa maana ya viwanja vya hapa
nyumbani lakini hata viwanja vya nje ambako wangeweza kuangalia kupitia
runinga.
Wengi wamelipa ving’amuzi mbalimbali lengo likiwa ni kuangalia
mpira, wanaweza kuona hiyo ni sehemu ya hasara lakini hakuna namna kama
nilivyosema kuwa lazima kuishi kulingana na mazingira ya sasa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli
yeye amekuwa jasiri, pamoja na kuwa na hali hii ya hofu ameendelea kuwatia moyo
wananchi wake au anaowaongoza namna ambavyo inaweza kuendelea na mapambano
yanavyoweza kwisha kwa ushindi.
Serikali yake imeonyesha nia ya kurejesha michezo kwa kuanza na
soka na baadaye tumeona wizara husika ikieleza kwamba hilo limefanikiwa na
tayari linafanyiwa kazi kuhakikisha mambo yanafanyika kwa tahadhari kubwa.
Rais Magufuli amemaliza kazi kwa kuwa amefanya kitu kikubwa kwa
wanamichezo akianza na soka. Kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha zawadi hii
aliyoitoa haitumiki vibaya na wahusika kwa maana ya wadau, watende haki
kuonyesha kwamba walikuwa wanastahili kupewa nafasi hii ambayo nchi nyingine
nyingi bado hawajaipata.
Tumeona ligi chache kama Bundesliga ya Ujerumani ambayo imeanza
sambamba na ligi ya Korea Kusini. Tayari Premier League ya England tumeelezwa
itarejea Juni lakini kuna La Liga ya Hispania na Serie A ya Italia ambako nao
wameamua kurejea.
Kwa Afrika, Tanzania inaonekana kuwa ya kwanza kabisa kuruhusu
michezo kurejea, jambo ambalo wahusika wanapaswa kulitumia vizuri kuunga mkono
uamuzi huo wa Rais Magufuli.
Kutumia vizuri hapa nawagusa wachezaji wenyewe, makocha, waamuzi
na hata viongozi wa klabu na mashirikisho. Kuwa wafuate masharti ya wataalamu
wanaeleza nini ili kuhakikisha wanamaliza ligi hiyo au nyingine
zitakazoendeshwa wakiwa salama.
Nasisitiza usalama kwa kuwa inawezekana. Mfano mchezaji amepimwa
na kuonekana yuko salama, hivyo anapitishwa kuwa sasa yuko tayari kushiriki
katika mechi za ligi akiwa na wenzake dhidi ya timu nyingine, basi ni lazima
awe mweledi kwa vitendo.
Mchezaji huyo kama amejua ameshapimwa na usalama wake ni usalama
wa wenzake atakaokutana nao dhidi yake au wale wenzake wa timu moja anaofanya
nao mazoezi, basi lazima ajilinde.
Ninaamini kwa wale watakaokuwa wamefanyiwa vipimo na kukaa
sehemu sahihi, basi ni jambo jema kabisa kuwa makini badala ya kusikia au
kumuona mchezaji aliye katika timu inayoshiriki ligi akiwa katika makundi ya
watu wengine ambao hawajapimwa.
Ninaamini katika kipindi hicho wakati ligi zinachezwa hakutakuwa
na uhuru mkubwa wa kutosha kwa wachezaji wengi.
Badala yake kutakuwa na masharti mengi hasa kutoka kwa
wataalamu wa afya, lengo likiwa ni kumaliza ligi kukiwa na usalama au salama.
Sasa kwa wachezaji, makocha, viongozi na wengine ni lazima wawe wavumilivu ili
waweze kumaliza kipindi hicho cha mechi 10.
Kama watashindwa kufuata masharti, halafu wakasababisha
maambukizi, maana yake watafanya ionekane Serikali ilikuwa na haraka na
ilipaswa kusubiri. Au Serikali iliamua kuwapa dhamana watu wasiojielewa au
wasiojua thamani ya walichopewa, hili litakuwa jambo baya sana.
Bado ninaamini watu walio ndani ya michezo watakuwa wameelewa
alichokifanya Rais Magufuli kuwa si jambo dogo la kijasiri, hivyo si vizuri
kumuangusha.








0 COMMENTS:
Post a Comment