YALE mambo ambayo tulikuwa tumeyakumbuka kwa muda mrefu sasa yapo njiani kurejea huku msisitizo mkubwa ukiwa kwenye kuchukua tahadhari na kufanya mambo kwa weledi bila kubababisha.
Ni masuala ya michezo ambayo yalikuwa yamesimamishwa na Serikali kutokana na kuibuka kwa janga la Virusi vya Corona ambalo linaivurugavuruga dunia kwa sasa.
Ilikuwa Machi 17 nikukumbushe kwamba Serikali iliamua kusimamisha masuala ya michezo na sababu kubwa ilikuwa ni kuzuia zaidi maambukizi ya Corona ambayo ni hatari kwa afya.
Kurejea kwenye ulimwengu wa soka baada ya kimya cha muda mrefu ambacho kilikuwa kina maswali mengi kwa familia ya michezo ni kitu cha kukipokea kwa mikono miwili huku tukikumbuka tahadhari dhidi ya Corona ni muhimu kuchukuliwa.
Mambo mengi yalikuwa yamesimama duniani kote na kwenye upande wa soka ndani ya ardhi ya Tanzania pia shughuli zilikuwa zimesimama ili kutoa muda wa kufanya tathimini na kupambana kwa nguvu kumshinda adui.
Furaha ya mashabiki na familia ya michezo kiujumla haikuwa ile ya siku zote kwani kukaa muda mrefu bila kushuhudia mechi za ushindani ilikuwa inaumiza.
Tayari ipo wazi Serikali imeruhusu masuala ya michezo kurejea baada ya kujiridhisha kwamba maambukizi yameanza kupunguua ingawa Corona ipo hilo lipo wazi na Serikali yenyewe inatambua hilo.
Tunapaswa kuendelea kuchukua tahadhari tusijisahau tukafikiri tumemshinda adui Corona ilihali bado yupo kwenye ardhi ya Tanzania na dunia kiujumla.
Ni kweli tulikuwa kwenye hali ya upweke bila kushuhudia mpira wa ushindani na kuona zile burudani ambazo tulikuwa tumezizoea kwa muda mrefu ila kwa sasa furaha inarejea kikubwa ni kuendelea kuchukua tahadhari.
Kila mmoja kwenye ulimwengu wa soka kuna kitu ambacho anakikumbuka kwani alikikosa kwa muda wa miezi miwili hivyo kurejea kwake ni furaha kwa familia kiujumla.
Haikuwa kazi rahisi lakini hatukuwa na namna ya kufanya kwa kuwa afya ni jambo la msingi na ilikuwa ni dharula imetokea nasi tukawa hatuna njia ya kufanya zaidi ya kukubali kwamba lazima tuingie vitani kupambana.
Kuanza kwa masuala ya michezo kusitufanye tusahau kwamba kuna Corona na kuendelea kufanya mambo kama kawaida kabla ya Corona hapana tutaharibu mambo kwa mtindo huo.
Mipango makini inabidi ipangwe na kila mmoja kwa sasa kuanzia mchezaji mmojammoja kwani ishawekwa wazi kwamba Juni 13 mambo yanarejea uwanjani.
Kauli ya Serikali ya hivi karibuni kwamba maisha yataendelea kwenye ulimwengu wa soka kama ilivyokuwa mwanzo ni furaha kwa kila mmoja.
Serikali imeridhia kuendelea na soka kwa kucheza mechi za nyumbani na ugenini yaani kuendelea na maisha kabla ya Corona.
Hivyo tunaendelea palepale ambapo tuliishia na kila mmoja atavuna kile ambacho amekipanda kwani awali ilionekana kuwa kuna hali ya malalamiko kwa baadhi ya timu.
Ikumbukwe kuwa awali Serikali ilisema kuwa kutakuwa na vituo viwili ambavyo ni pale Mwanza na Dar es Salaam na mechi zingechezwa kwa kasi ili kumaliza msimu ila mambo yamebadilika.
Awali ilipangwa kuanzia Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, hawa kituo chao kingekuwa Mwanza hivyo watu wa Mwanza wangekuwa na ugeni mkubwa wa mashabiki pamoja na timu ambazo zingetia timu kambini.
Ligi ya Wanawake pamoja na ligi nyingine zote Serikali imeruhusu ikiziachia mamlaka husika ikiwa ni pamoja na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kujua namna gani wao watafanya ila kanuni ni zilezile za kufuata.
Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho hawa kituo chao kingekuwa Dar hivyo kuna baadhi ambazo zilianza kujipanga kwa hili ila upepo umebadilika.
Mamlaka inayosimamia michezo Tanzania, Shirikisho la Soka (TFF) ni wakati mwingine wa kutazama namna bora katika kusimamia msimu huu wa 2019/20 pamoja na muongozo ambao umetolewa kwa wadau wote wa michezo.
Kurejea kwa mechi za nyumbani na ugenini kunamaanisha kwamba kila mmoja atashinda mechi zake kwa mtindo ambao anaujua yeye lakini cha msingi kwanza ninapenda kuwakumbusha wadau, tahadhari ni muhimu.
Wakati huu uliopo kwa sasa ni kuanza kujiandaa kwa timu zote hasa baada ya Serikali kutoa muongozo wa kufanya wakati wa kumaliza mechi hizi kwa kipindi hiki ambapo kuna janga la Corona.
Bado tusijisahau kwamba janga la Corona lipo na tahadhari zinatakiwa ziendelee kuchukuliwa kwani afya ni utajiri namba moja.
Mashabiki wasikasirike kwa kuwa wameambiwa kwamba lazima waingie uwanjani wakiwa wamevaa barakoa hili ni jambo jema ni muda sasa kujipanga kupata barakoa yako maisha yaendelee.
Ingizo kubwa la mashabiki kwenye mechi ambayo itakuwa na ushindani pia imepigwa panga kwamba lazima waingie mashabiki nusu ya idadi.
Katika hili mashabiki mnapaswa kuwa waelewa na pale itakapotokea labda mmetangaziwa kwamba ni nusu ya mashabiki basi msisahau kuwahi tiketi zenu mapema ili yule mjanja atakayewahi atakuwa ndani ya uwanja atakayechelewa basi asikasirike akae nyumbani.
Hii yote ni tahadhari kwani Corona bado ipo pia wasijisahau kwamba wanatakiwa kunawa na maji tiririka, kukaa umbali wa mita moja hili nalo ni la msingi kuzingatia kuelekea kurejea kwa ligi.
Ushangiliaji wa makelele pia kwa sasa hautaruhusiwa tunapaswa kubadili mbinu katika kile ambacho tunakifanya na kuwa wastaarabu kwa muda wote wa uwanjani.
Kinga ni bora kuliko tiba kwa wakati uliopo kwa sasa ni muhimu kuchukua tahadhari kila wakati bila kuchoka afya ni kitu muhimu.
Katika hili ni muhimu kufuata utaratibu unaotolewa na Serikali kwa kuzingatia bila kupuuzia maagizo ambayo yanatolewa na wataalamu wetu.
Kitu kikubwa kwa timu na wadau kufuata muongozo ambao umetolewa na Serikali ili kuutimiza kwa uhakika bila kukosea.
Ikumbukwe kuwa kwa timu ambayo itashindwa kufuata utaratibu inapewa adhabu ya moja kwa moja na Serikali yenyewe kwa kushirikiana na TFF.
Ugonjwa huu upo kweli hilo tusijisahau kwa kuendelea kuishi maisha yale ambayo tuliyazoea zamani ni muda wa kubadilika na kuongeza umakini zaidi.
Ni muhimu kufuata maelekezo ya Serikali na kufuata kanuni za afya ili kujilinda sisi wenyewe hii vita tumeanza ni lazima tuimalize kwa ushindi inawezekana.
Vita ni yetu hatupo sehemu mbaya kwa sasa tupo katika kuelekea kupata ushindi hivyo ni lazima tuendelee kuchukua tahadhari ili kuishinda kabisa Corona.
Wachezaji wakati wenu wa kurejea uwanjani tayari umeshafika na nina amini kwamba muda ambao mnafanya mazoezi na timu ni lazima mtarejea kwenye ubora wenu.
Kila mchezaji asijisahau kwa kufikiri kwamba atakuwa na nafasi ya kujitetea kwa sasa hapana ni muhimu kuonyesha kwamba alikuwa anafanya kile ambacho alielezwa.
Tunaamini kwamba kwa sasa kazi kubwa itakuwa ndani ya uwanja kupambana na kutafuta matokeo kwa ajili ya timu zao ndani ya uwanja bila kuchoka.
Dakika tisini kwa sasa ndio atakuwa mwamuzi wa kile ambacho mlielekezwa kufanya mkiwa kwenye mapumziko na inapaswa iwe katika umakini mkubwa kutimiza majukumu yenu.
Mechi zinazofuata kwa sasa ni za lala salama na kila mmoja ni lazima apambane kutafuta matokeo chanya jambo ambalo litafanya kila timu iwe kamili.
Ilikuwa ngumu kumfuatilia mchezaji mmojammoja ila kwa kuwa mazoezi yameruhisiwa basi kila mchezaji atavuna kile ambacho alikipanda wakati ule wa mapumziko ya Corona.
Kazi iliyopo kwa kila mmoja ni kupambana kuona namna gani wachezaji watakuwa kwenye ubora na kupambana kwa hali na mali kupata matokeo chanya.
Hakuna ambaye anaweza kuamini kwamba Juni 13 kazi itaanza lakini mambo yameshaanza kwenda kasi ni lazima kila mmoja apambane kutafuta matokeo.
Muda hautakuwa rafiki wa kuanza kujipanga tena kwa wakati ambao umebaki ni kuona kwamba kila timu inamaliza mechi zake na kuanza kujipanga kwa wakati ujao.
Muda upo kwa sasa kuanza kujipanga upya na kufuta yale makosa ambayo yalifanyika awali kwa kuzembea ama kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa mchezaji mwenyewe.
Wachezaji ambao walikuwa na nidhamu nje ya uwanja binafsi nina amini matunda yao watayaona ndani ya uwanja kwa kuonyesha uwezo wao kwa vitendo.
Uvivu na uzembe ni hasara kwa timu na mchezaji mwenyewe kwani kunarudisha nyuma maendeleo ya timu jambo ambalo halitakiwi kufanyika.
Wakati wa kuendelea kutoa burudani kwa mashabiki unakuja kwa wachezaji lakini cha msingi ni kukumbuka kwamba Corona ipo.
0 COMMENTS:
Post a Comment