USIRUHUSU mwili wako ukachoka ilihali una nguvu ya kupambana katika tatizo ambalo upo nalo kwa wakati huo lazima utafute njia nzuri ya kukutoa kwenye tatizo ambalo unalipitia.
Najua kuna mbinu nyingi za kutatua matatizo kwa namna ambavyo watu wanaamua kupambana nayo inategemea na mazingira ambayo unakuwa upo kwa wakati huo.
Kila mmoja ana mbinu zake ambazo anazijua wakati wa kupambana na matatizo hilo lipo wazi lakini hata ukiwa na njia mia mbili jambo la kwanza la muhimu ni kutokukata tamaa
Mengi yanatokea na kuna magumu ninakubali kwamba kwa binadamu haya yote lazima yamkute lakini jambo la msingi ni kuona namna gani anaweza kupambana na kujitoa katika tatizo ambalo yupo.
Tunaona kwamba miongoni mwa njia ya kupambana na tatizo ni kulitambua kwanza hilo tatizo kisha kuanza kutafuta mbinu ya kujiengua taratibu kwenye hilo janga ambalo tunakuwa tupo kwa wakati huo.
Nimeanza hivyo nikimaanisha kwamba giza ambalo lilikuwa limetanda kwenye ulimwengu wa mpira kutokana na janga la Corona limeanza kuondoka taratibu.
Kumeshapambazuka kwa sasa kwenye maisha ya soka lile giza ambalo lilikuwepo awali kwa sasa limeanza kukatika taratibu kwa kuwa mwanga umeanza kuonekana.
Kwa kuwa tayari kila kitu kipo vizuri kwa upande wa maandalizi basi wadau tusiangushane katika kufuata utaratibu ambao unawekwa na Serikali.
Ikumbukwe kwamba licha ya kwamba maisha ya soka yanaendelea bado kuna umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwani hili janga lipo bado.
Mapambano yanapaswa yaendelee mchana hata usiku ili hali wakati ujao iwe sharwi zaidi ya hapa ambapo tumefikia kwani bado ugonjwa upo tusichukulie poa.
Wakati Rais wa Jamhuri ta Muungano wa Tanzania, John Magufuli anaruhusu masuala ya michezo alikuwa akisisitiza kwamba lazima tahadhari ifuatwe ili kuwalinda zaidi watanzania.
Wadau tusimuangushe Rais wetu ambaye anapenda kuona michezo ikiendelea na watu wake wakifurahi huku wakijilinda kwa kuchukua tahadhari ambazo zinafaa.
Wachache sana ambao wanaweza kuelewa ni namna gani Rais ameamua kufanya maamuzi magumu na ya kishujaa ila yote amefanya kwa kuwa anaamini kwamba watu wake ni wasikivu na wanajua kuchukua tahadhari.
Kwa hatua ambayo Serikali imeamua kufanya inapaswa ipongezwa kwani imerejesha burudani kwa familia ya michezo na kuona namna gani burudani itaendelea.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari na kufuata yale maagizo ambayo yametolewa kwa wadau.
Jambo la msingi kuhusu afya yetu ni kuona kwamba kitu kitakachotufanya tuendelee kuwa salama ni kuchukua tahadhari wakati wote bila kujali maambukizi yamepungua haina maana kwamba Corona imeisha.
Isijirudie tena mambo yale kama Azam FC ilivyokuwa ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Transit Camp ambapo mashabiki walitaka kuendelea mazoea yao ya kukaa kama kawaida.
Katika hilo wote tunapaswa kuwa makini tusisumbue mamlaka ambazo zipo na zinatekeleza kazi zao basi ni bora kutii kuliko kuzilazimisha mamlaka kutumia nguvu kubwa.
Nimeona kwamba kuna mambo ambayo yameanza kufuatwa ikiwa ni barakoa kwa mashabiki wanapoingia uwanjani pamoja na waandishi wa habari pia kwani hapa vita ni ya wote.
Kwa namna ambavyo tumeanza licha ya changamoto kidogo hatupo vibaya muhimu ni kuona kwamba maandalizi yanaendelea kwa kila timu kujizatiti ili kutimiza muongozo kwa ufasaha.
Mashabiki pia kazi ni kubwa kuendelea kufuata ule utaratibu ambao umewekwa bila kupuuzia kwani kwa kufanya hivyo itafanya Serikali ifikirie kutoa adhabu jambo ambalo sio iwapo kutakuwa na udanganyifu.
Hapa tunakumbushana kwani afya ni muhimu ndugu yangu msomaji ndio maana leo tunaendelea kuwa wazima kwa kuwa tuna utajiri wa afya ambayo tumepewa na Mungu.
Ukweli ni kwamba iwapo mtu yoyote atakuwa anafanya kinyume na utaratibu ili awe salama kwa kupuuzia ni rahisi kutokuwa salama yeye na jamii nzima kiujumla.
Chaguo la shabiki ambaye hawezi kufuata utaratibu ni yeye mwenyewe kuamua kubaki nyumbani ama kwenda kutazama kwa jirani kwenye vibanda umiza.
Kikubwa ambacho wengi walikuwa wanasubiri ni kuona idadi ya wachezaji 10 iliyotolewa awali ingeendelea ila kutokana na Serikali kuona kwamba hali imeanza kuwa shwari kwa upande wa maambukizi imeamua kuruhusu mashabiki.
Hata kwenye vibanda umiza bado Serikali ipo kwani mamlaka husika ambazo ni Serikali za mtaa zimepewa jukumu la kufuatilia kia kibanda umiza.
Kwako wewe ambaye haujali ikufikie kwamba hata ukiwa kwenye vibanda umiza bado Serikali ipo na unatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa kwenda na barakoa yako na kunawa kwa maji tiririka.
Ninarudia tena kwamba afya za mashabiki ni muhimu hivyo ni lazima ule muongozo uliotolewa na Serikali ukafuatwa bila kupinga kwa kuwa atakayekiuka atapewa adhabu.
Wizara ya afya na Serikali inatambua kwamba nguvu kazi za watu zinategemea afya bora ambayo ni muhimu kulindwa kwa sasa hivyo nasi pia lazima tujali.
Mambo ni mengi ya kufanya kwa sasa ikiwa ni pamoja na kupambana kufikia malengo ila hautaweza kuyafikia ikiwa hautakuwa na afya njema.
Muda ambao umebaki kwa sasa timu wenyeji kazi ni kwenu kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya kucheza ili kusiwe na yule atakayepata adhabu.
Serikali inamaanisha kwamba kwa sasa inafuatilia kila hatua na ipo macho kuona kwamba hakuna uvunjifu wa utaratibu uliowekwa pale mikikimikiki ya ligi ikianza.
Nina amini kwamba katika hili wadau wa michezo tutaungana kama hali ilivyokuwa mwanzo hakuna ambaye alijitenga bali mapambano yalikuwa kwa kushirikiana basi na sasa kwenye unafuu tuwe kitu kimoja.
Ninarudia kusema kwamba Corona ipo tusijidanganye kwamba vita imekwisha hapana ni muhimu kuchukua tahadhari hivyo kwa upande wa mashabiki timu zinapaswa ziangaliwe.
Tusisahau kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona ndugu zangu hili janga bado tupo nalo ni muhimu kujilinda kwa kuchukua tahadhari na kufuata kanuni za afya.
Tayari imewekwa wazi kuwa ni lazima kila mmoja anakazi ya kuchukua tahadhari yeye pamoja na jamii inayomzunguka ili abaki kuwa salama.
Lazima mashabiki wasijisahau pale watakapoingia uwanjani kunawa mikono kwa maji tiririka ikiwa ni mwendelezo wa kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
Vita tuliianza kwa kushirikiana ninaona kabisa kuna mwanga unakuja ila ili uweze kuonekana ni lazima kila mmoja awe tayari kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
0 COMMENTS:
Post a Comment