WAKATI mwingine wachezaji wa mpira huzitazama rekodi zao walizoziweka na kuishia kucheka kwa kuwa wanakosa chaguo la kufanya kutokana na muda kuwakimbia.
Ligi ilipoanza kabla ya kusimamishwa kwa sasa kutokana na janga la Virusi vya Corona kuna wachezaji ambao walijiunga kwenye timu mpya wakiwa na matarajio ya kufanya vizuri lakini ghafla mambo kwao yamekuwa magumu.
Wanapitia kipindi kigumu katika kuweka rekodi mpya kwenye kazi zao pamoja na kuzivunja zile ambazo waliziandika walipokuwa na timu zao za zamani.
Huenda watakuwa wamepata somo kwa kuwa tayari masuala ya michezo yanarejea na Juni 13 ratiba inaanza kusoma rasmi.
Hii hapa orodha ya wachezaji ambao mashabiki walitarajia kuona mambo makubwa kwao lakini ghafla mambo yamekuwa magumu kwao namna hii:-
Ajibu
Ibrahim Ajibu, kiungo mshambuliaji wa Simba alikuwa na wakati mzuri alipokuwa ndani ya Yanga msimu wa 2018/19. Usajili wake ulitikisa Bongo kutokana na dili lake la kujiunga TP Mazembe kuja wakati wa usajili ila danadana zikawa nyingi akaibukia Simba.
Wakati akiwa Yanga alitupia mabao sita na alikuwa ni namba moja kwa kutengeneza pasi za mwisho alitoa 17. Mambo yamekuwa magumu kwa sasa ndani ya Simba amecheza mechi 16 kati ya 26 na ametumia dakika 948 ana pasi nne za mwisho na bao moja alililowafunga Polisi Tanzania, Uwanja wa Taifa.
Erick Kabamba
Nyota huyu hana bahati ndani ya Yanga, alisajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo Januari ambapo mpaka sasa hajawa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza.
Yanga ikiwa imecheza mechi 15 baada ya kutua kwake Bongo amecheza mechi tatu pekee ambazo ni sawa na dakika 270.
Raia huyu wa Zambia mechi zake zilikuwa mbele ya Singida United Uwanja wa Namfua ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1, Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani 0-0 na Alliance FC Uwanja wa Taifa, Yanga ilishinda mabao 2-0.
Gadiel
Gadiel Michael, uwezo wake ulimkosha Kocha Mkuu Patrick Ausems kabla ya kuchimbishwa na lengo kubwa ilikuwa kumpa ushindani Mohamed Hussein,’Tshabalala’ ila mambo yamekuwa magumu ghafla.
Simba ikiwa imecheza mechi 28 yeye amecheza mechi nane ambazo ni dakika 720 huku akikimbizwa na Tshabalala ambaye amecheza mechi 18 za Ligi Kuu Bara na ametupia mabao mawili na pasi mbili za mabao jambo linalompa ugumu Gadiel kupenya kikosi cha kwanza kwani hajafunga bao wala kutoa pasi pia.
Rojas Gabriel
Beki huyu anayekipiga Namungo kwa sasa alianza msimu wa 2019/20 akiwa ndani ya Mwadui ambapo alikuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza licha ya kuwa beki alitoa pasi moja ya bao.
Maisha yake ndani ya Namungo aliyojiunga nayo kwenye usajili wa dirisha dogo Januari yamekuwa tofauti amecheza mechi tano sawa na dakika 450 hajafurukuta kwenye kikosi kilicho chini ya Kocha Mkuu Hitimana Thiery.
Shiza Kichuya
Alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na uwezo wake mkubwa ndani ya uwanja akiwa ni zao la Mtibwa Sugar. Alijiunga na Simba msimu wa 2016/17 aliuzwa msimu wa 2018/19 kwenye Klabu ya ENPPI ya Misri.
Bao lake la kona goli la msimu 2016/17 mbele ya Yanga lilimpandisha chati na kumfanya apendwe, mchezo huo ulichezwa Oktoba Mosi, Uwanja wa Taifa kwenye sare ya kufungana bao 1-1.
Amerejeshwa Simba kwenye usajili wa dirisha dogo kwa sasa ni kama zama zake zimeisha kwani amecheza mechi moja ya ligi akitumia dakika 45 mbele ya JKT Tanzania na Simba ilinyooshwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru.
Yikpe Gnamien
Jamaa alikuja kwa mkwara mzito ambapo aligoma kufanya majaribio baada ya kuachana na Gor Mahia ya Kenya.
Yikpe mwili jumba raia wa Ivory Coast amekuwa hana nafasi kikosi cha kwanza amefunga bao moja huku akitumia dakika 258 uwanjani akicheza mechi 10.
Mechi zake hizi hapa:-Simba (29), Kagera Sugar (20), Azam FC (15), Singida (23), Mtibwa (22), Lipuli (61), Ruvu Shooting (24), Prisons (60) na Polisi Tanzania (26), Namungo (2)
Kassim Khamis
Simba na Yanga zilikuwa kwenye mvutano mkubwa wa kuinasa saini ya jamaa huyu wa Zanzibar ila mabosi wa Azam FC wakawazidi ujanja na kuipata saini ya nyota huyu aliyekuwa akikipiga Kagera Sugar.
Amepita mikono ya makocha wawili alianza na Etienne Ndayiragije ambaye kwa sasa yupo na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kisha sasa Azam ipo chini ya Arstica Cioaba ila hana nafasi kikosi cha kwanza.
Alitupia mabao saba akiwa Kagera Sugar msimu wa 2018/19 alipata nafasi ya kuitwa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania lakini kwa sasa anaishi dunia nyingine hafurukuti kikosi cha kwanza anaishia kusugua benchi.
Aiyee
Salim Aiyee, akiwa Mwadui FC alitupia mabao 18 ambapo alikuwa ni mzawa wa kwanza kutupia mabao mengi kinara alikuwa Meddie Kagere aliyetupia mabao 23 msimu wa 2018/19.
Mambo yamekuwa tofauti kwake msimu huu akiwa KMC ikiwa imecheza mechi 29 na kutupia mabao 26 amefunga bao moja ilikuwa mbele ya Yanga wakati KMC ikishinda bao 1-0.
Deogratius Munish
Alijiunga na Lipuli akiwa ni mchezaji huru kwenye dirisha dogo baada ya kumalizana na Simba.Mechi 8 amefungwa mabao 16 huku Lipuli ikifunga mabao nane.
Mechi zake :-Ruvu Shooting 3-1 Lipuli, Februari 20, Yanga 2-1 Lipuli, Februari 5, Lipuli 1-1 JKT Tanzania Februari 11,Mbeya City 2-1 Lipuli, Februari 18, Tanzania Prisons 2-0 Lipuli, Februari 23, Lipuli 1-2 Namungo , Februari 29, Lipuli 3-3 Ndanda, Machi 3, Machi 10, Lipuli 0-1 Kagera Sugar.
Kuhusu Ajib na Gadwel Mitchel ni kuwa huko Yanga hawakuwepo wenye viwango vya kuwa weka Benchi wachezaji Hao jambo ambalo kwa Simba ni tofauti na hilo ni hakika
ReplyDeleteTrue
Delete