BERNARD Morrison, kiungo wa Yanga amesema kuwa yupo fiti leo kumalizana na Simba Uwanja wa Taifa kwa kuwa ndizo mechi ambazo amezizoea tofauti na nyingine anazocheza kwenye viwanja vya nje ya dar pamoja na wapinzani wengine.
Leo Simba inamenyana na Yanga, kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga ambapo mshindi atakutana na Namungo fainali itakayopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga.
Habari za kuaminika kutoka kwa mtu wa karibu wa Morrison zimeeleza kuwa Morrison amepania kufanya makubwa leo kwenye mechi dhidi ya Simba mara mbili zaidi ya alichofanya Machi 8, Uwanja wa Taifa.
Kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Morison aliwafunga Simba bao moja lililowapa pointi tatu jumla ila hivi karibuni alikuwa kwenye mvutano na klabu kuhusu suala la mkataba na inaelezwa kuwa wameyamaliza mambo hayo.
"Ujue Morrison anafurahi sana anapoona kwamba leo anakutana na Simba, amesema kuwa mashabiki wa Yanga wasiwe na hofu kuhusu yeye atatimiza majukumu yake na atawafunga akipata nafasi.
"Sababu kubwa za kujiamini ni kwamba anasema hizi mechi ndizo ambazo amezizoea hasa kucheza na wachezaji wenye uwezo mkubwa na mzuri jambo ambalo halimpi presha kwa kuwa mechi kubwa yeye ni zake na uzoefu unambeba.
"Hana majeraha hana ugonjwa wowote na amepanga kufanya maajabu kweli leo uwanjani mbele ya Simba hata kambini amekuwa na vitukovituko lengo ni kuwaweka wachezaji katika hali ya umoja," alisema mtu wake wa karibu.
Luc Eymael, Kocha Mkuu wa Yanga alisema kuwa kufunga bao kwa Morrison kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar kumemuongeza hali ya kujiamini hivyo hana mashaka naye leo kwenye mchezo dhidi ya Simba.
Morrison mwenye amesema kuwa:"Kazi yangu ni mpira na Yanga ndio timu yangu nitapambana kuipa ushindi,".
0 COMMENTS:
Post a Comment