July 8, 2020


UONGOZI wa Klabu ya Simba inatajwa kuwa upo kwenye mazungumzo na straika wa timu ya Kiyovu ya Rwanda, Mnigeria, Samson Babuwa.

Simba baada ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara na kujikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, inapambana kuhakikisha inaimarisha safu yake ya ushambuliaji ili ifanye vizuri kwenye michuano hiyo ya kimataifa pamoja na ya ndani.

Licha ya kudaiwa Simba kufanya mazungumzo na baadhi ya washambuliaji kutoka nchini Rwanda akiwemo aliyekuwa mshambuliaji wa Rayon Sport, Mghana, Michael Sarpong na Mrundi, Jules Ulimwengu, lakini bado haijaridhika, sasa imegeuzia nguvu zake kwa Mnigeria huyo.

Kwa mujibu wa taarifa ilizozipata Spoti Xtra kutoka nchini Rwanda, Simba inapambana kuhakikisha wanafanikiwa kunasa saini ya straika huyo aliyevunja rekodi za kutosha ndani ya timu yake tangu ajiunge nayo msimu huu.

“Suala la Babuwa kutakiwa na Simba ni la kweli, wamekuwa wakifanya mazungumzo kwa siri kubwa sana.

“Mwenyewe amekuwa mgumu kusema, lakini ni kweli Simba wanamtaka na wamekuwa wakitumia baadhi ya watu wao waliopo hapa Rwanda kumshawishi hasa kutokana mkataba wake na Kiyovu kubaki miezi sita.

“Jamaa ni straika mzuri kwa sababu ndani ya msimu huu amekuwa mfungaji bora kwenye timu yake, lakini amekuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kufunga mabao 15 msimu huu katika mechi 23 alizocheza.

“Pia ametoa pasi za mwisho kumi, hivyo siyo mchezaji wa kawaida. Ukiangalia pia amewafunga APR kwenye mechi zote mbili msimu huu,” kilisema chanzo chetu.

Spoti Xtra lilimtafuta straika huyo ambaye kwa upande wake hakutaka kuweka wazi mipango yake zaidi ya kusema:

“Nilisaini mkataba wa mwaka mmoja kuchezea Kiyovu na kwa sasa naruhusiwa kuzungumza na timu yoyote kutokana na kubaki miezi sita, lakini nisingependa kuweka wazi kwenye vyombo vya habari kwa kuwa mambo yana kawaida ya kubadilika.

”Hivi karibuni, Katibu wa Simba, Arnold Kashembe, alisema: “Hivi sasa Simba tunafanya usajili makini kwa ajili ya michuano ya kimataifa pamoja na ile ya ndani.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic