UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa leo kwenye kilele cha Tamasha la Azam Festival mbali na kuwatambulisha wachezaji wapya kutakuwa na burudani mbalimbali pamoja na surprise za kutosha.
Leo Uwanja wa Azam Complex, Azam FC itatambulisha wachezaji wake wapya pamoja na wale wa zamani kwa mashabiki wake pamoja na uzi mpya ambao watautumia msimu wa 2020/21.
Mgeni rasmi wa leo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Azam FC Zakaria Thabit, alisema kuwa malengo makubwa ya timu hiyo ni kuwa bora na yenye ushindani kwa kuwa inaongozwa na watu makini hivyo mashabiki waipe sapoti.
“Azam FC ni timu kubwa na bora hivyo malengo makubwa ni kuifanya izidi kuwa imara, mashabiki ni timu yao waendelee kuipa sapoti, na kujitokeza kwa wingi kilele cha Azam Festival” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin alisema kuwa watafanya mambo mengi mazuri huku burudani ikitolewa pia kutoka kwa msanii maarufu wa muziki, Ali Kiba na Msaga Sumu pia amethibitisha uwepo wake.
Kiba alisema: ”Nimefurahi sana kupata nafasi ya kutumbuiza mbele ya mashabiki, mimi ni mwanamichezo. Ninapenda kuwaambia watu kwamba waje kwa wingi Azam ni sehemu ambayo ina vitu vingi vya kufanya kwa watu wa mwanzo kabisa watakaonunua jezi kwa shilingi 20,000 nitasaini na kupiga nao picha.
“Nipo tofauti kwa sasa siwezi kuzungumza kama nitatoa wimbo wa Azam ama la, ninajua kutakuwa na surprise nyingi, hivyo watu wasishangae wakanikuta nipo uwanjani mimi ni mchezaji,” alisema Kiba.
Mechi ya kirafiki leo kwa Azam FC itakuwa dhidi ya Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Hitimana Thiery na miongoni mwa wachezaji wapya watakaotambulishwa ni pamoja na Awesu Awesu (Kagera Sugar), Ally Niyonzima, (Rayorn Sports), Ayoub Lyanga,(Coastal Union),Ismail Kada,(Tanzania Prisons),David Kissu,(Gor Mahia),Emmanuel Charlse,(Mbao), Prince Dube (Highlanders FC).
0 COMMENTS:
Post a Comment