MSHAURI Mkuu wa Klabu ya Yanga kuelekea kwenye mabadiliko,Senzo Mazingisa raia wa Afrika Kusini, amefunguka kwa kuwafuta hofu mashabiki wa timu hiyo akiwaambia watulie kwani kikosi hicho kitakuwa hatari kadiri muda unavyooenda.
Senzo ameongeza kwamba kwa sasa mashabiki wa timu hiyo watulie kwani kikosi ndiyo kinazidi kujijenga kwa ajili ya kufanya makubwa kwenye Ligi Kuu Bara na michuano mingine msimu huu.
Yanga katika usajili wa msimu huu, imesajili wachezaji 12 katika kukiimarisha kikosi hicho kinacholisaka taji la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo bila ya mafanikio.
Senzo ameliambia Spoti Xtra kuwa, kikosi hicho kwa sasa kinaendelea kujijenga taratibu ambapo mashabiki wake wanatakiwa watulie kwani watakuja kupata kitu ambacho wanakitaka wakikaa sawa.
“Japo tumepata pointi kwenye mechi zote mbili lakini bado mashabiki wanatakiwa kutulia kwa sababu kikosi bado kinaendelea kujijenga taratibu.
“Benchi la ufundi linafanya kazi hiyo na tunaamini baada ya muda kila kitu kitakaa sawa, ila watupe muda kwa kipindi hiki, wasubirie baada ya muda mambo yakikaa sawa watapata kile ambacho wanakitaka,” alimaliza Senzo.
Kwa sasa kikosi cha Yanga kipo Bukoba kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, unaotarajiwa kuchezwa Septemba 19, Uwanja wa Kaitaba.
0 COMMENTS:
Post a Comment