September 12, 2020

 


HATIMAYE miamba 20 kunako Ligi Kuu England ‘Premier League’, leo inatarajia kuanza safari ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo kwa viwanja mbalimbali kuwaka moto huku kukiwa na Mtanzania mmoja tu, Mbwana Ally Samatta anayekipiga Aston Villa.

 

Ligi hiyo inakwenda kuanza ikiwa na makundi mbalimbali, zipo timu ambazo zinapewa nafasi ya kutwaa ubingwa, za kuwania kumaliza nafasi nne za juu na nyingine kubaki Premier msimu ujao.

 

Uwepo wa nyota wapya katika klabu mbalimbali, ni jambo lingine linalotia hamasa na hamu kwa mashabiki kutaka kuona msimu utakuwa na namna gani, ingawa bado viwanja vitakuwa tupu bila uwepo wa mashabiki kwa tahadhari ya Corona.


Kwa Tanzania, mashabiki wengi wana vitu vitatu katika vichwa vyao ambavyo vinapelekea kutaka kuona mambo yatakuwaje msimu huu, moja ni matarajio ya timu zao kufanya vizuri.

 

Mbili ni kushuhudia wachezaji wapya waliosajiliwa kwenye klabu zao wakitiki, lakini kubwa na la mwisho ni kuona nini atafanya Samatta akiwa na jezi yake namba 20 ya Villa.

 

Samatta alijiunga na Aston Villa Januari 20, 2020, akitokea KRC Genk ya Ubelgiji kwa mkataba wa miaka minne na nusu.Hadi ligi ya msimu uliopita inamalizika, Samatta alifunga bao moja katika michezo 14 ya Premier.


Sasa msimu huu inaonekana amepania kwelikweli kuhakikisha anawaziba mdomo wapinzani wake.Ikumbukwe kuwa Aston Villa imeongeza straika mwingine kutoka Brentford, Ollie Watkins, ambaye msimu uliopita aliweka kambani mabao 25 na asisti tatu kwenye Championship.

 

Sasa majibu ya maswali ya nini Samatta atakwenda kufanya, anayajibu baba yake mzazi, Mzee Ally Samatta, ambaye amekuwa bega kwa bega na kijana wake huyo katika makuzi yake kisoka mpaka sasa.

 

Mzee Samatta anasema: “Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa magazeti, kuna mwandishi mmoja wa Kiingereza alitabiri kwamba Samatta atakuwa mmoja kati ya wachezaji ambao watawania kiatu cha dhahabu katika msimu huu unaoanza.



“Usemi wake huo unaonekana utakuja kutimia, kwa sababu katika michezo miwili waliyocheza hivi karibuni amefanikiwa kufunga mabao mawili katika michezo yote hiyo, wakiwemo Arsenal ambao waliwachapa 3-2.

 

VIPI KUHUSU KUNYIMWA PASI?

“Hilo la kunyimwa pasi msimu huu halitakuwepo kwa sababu yeye mwenyewe ameniambia wachezaji wenzake wameshaanza kumjulia kuwa yeye ni mzuri juu, hivyo krosi zote wanazochonga anazifikia.


“Kwa hivyo wanampelekea mipira ya juu kwa ajili ya kichwa, zamani walikuwa hawamjui, lakini siku hizi wanapiga mipira ya juu na yeye anafunga kwa kichwa huko mazoezini.


ANAFANYA MAZOEZI GANI KWA KIPINDI HIKI?

“Alisema kwa sasa anafanya mazoezi makali sana kwa ajili ya kufanya vizuri, anapiga mashuti, anakimbia, anapiga vichwa ili kupambania namba kwenye kikosi cha kwanza.

 

ASTON VILLA IMESAJILI WASHAMBULIAJI WAPYA YEYE ANASEMAJE JUU YA HILO?

“Ameniambia kuwa yeye anafanya mazoezi kumshawishi mwalimu ili aweze kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.


SAMATTA MWENYEWE ANASEMAJE SASA KUELEKEA MSIMU MPYA?

“Anasema anataka kuchora na kuandika jina la Tanzania katika kuta za Aston Villa, ndoto na ahadi zake ni kufanya vizuri na kuwa mfalme ndani ya timu hiyo hili kuitangaza nchi na bendera yake.

 

“Anajua akifanya vizuri na kutajwa na mashabiki pamoja na vyombo vya habari, itakuwa ni sehemu nyingine ya kuifanya Tanzania ijulikane na kutangazika kama ambavyo ilitangazika wakati ambao alikuwa KRC Genk.

 

“Anataka aimbwe na kuandikwa kwenye jezi na midomo ya mashabiki wa Aston Villa, hilo atalipata ikiwa atafanya vizuri msimu huu ndiyo maana anaomba Watanzania wamuombee ili aweze kufanya vizuri.


“Anajua kuna ugumu wa kufikia huko, lakini kwa uwezo wake na sapoti ya Watanzania kwa dua na maombi anaamini atafanikiwa kufika huko ndani ya muda mfupi.Hiyo ndiyo tamaa yake kubwa na ahadi anayoitoa kwa Watanzania.

 

AMEKUAMBIA ANATAKA KUFUNGA MABAO MANGAPI MSIMU HUU?

“Idadi hajaniambia, ingawa amesema kuwa anataka kufunga mabao mengi kila atakapokuwa anapata nafasi ili kumshawishi mwalimu na kuisadia timu yake.

 

ULIMPA USHAURI GANI KAMA MZAZI?

“Unajua Samatta ni mtu wa kupambana, siku zote akisema nataka kufanya jambo fulani huwa anafanikiwa, hivyo nilichomuambia asiogope majina mapya, apambane kama kawaida yake.

 

“Ila nilimkumbusha kuwa, ukiona mchezaji analetwa kwenye nafasi unayocheza wewe, ujue kuwa umeletewa changamoto mpya kutokana na upungufu uliojitokeza hivyo unatakiwa kuonyesha kitu cha utofauti na mwenzako.“Lakini kubwa zaidi amtangulize Mungu kwenye kila hatua atakayopiga ndani ya msimu huu, maana akiboronga, inaweza ikawa mbaya kwake na akashindwa kutimiza malengo aliyojiwekea.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic