October 17, 2020


RAUNDI ya sita kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara inazidi kurindima ambapo timu zimekuwa zikipambana kusaka pointi tatu ndani ya uwanja.

 

Ipo wazi kabisa ushindani wa msimu huu wa 2020/21 ni tofauti kabisakabisa na ule uliopita wa 2019/20 kwa namna ambavyo timu zinaingia kupata matokeo ndani ya uwanja.

 

 

Kila timu imejipanga kwa namna yake na mwisho wa siku inapata matokeo chanya. Tunaona kwamba kwa upande wa Yanga wao wameweka nguvu kubwa upande wa ulinzi huku Simba, Azam  FC wao nguvu zao zikiwa kwenye upande wa ushambuliaji.

 

Katika hili kila timu imekuwa ikipambana kusaka ushindi na inapata kile ambacho imekipanda. Hilo ni jambo la kwanza na jambo la pili ni kuona namna gani matokeo yanapatikana.

 

Ninasema hivyo kwa sababu kuna timu ambazo zimekuwa na matokeo mabovu kwenye mechi zaidi ya mbili mfululizo na bado hazijashtuka kufanya maamuzi.

 

Hii ni mbaya kwa kuwa mwanzo wa ligi hesabu za wale wanaosaka ubingwa huanza kupangwa na kwa wale ambao wanajiandaa kushuka pia hesabu zao huanza kuhesabiwa.

 

Kwa wale wajanja wamekuwa wakishinda mechi za mwanzo ili kujiongezea hali ya kujiamini. Wapo wale wengine ambao wanahitaji kushinda lakini wanashindwa kutokana na mbinu ambazo wanatumia.

 

 

Ni muhimu kufanya marekebisho makubwa wakati huu kabla ya wakati ule wa mzunguko wa pili ambao  hali huwa ngumu zaidi. Ninasema hivyo kwa sababu ninakumbuka msimu uliopita timu nyingi zilizinduka mzunguko wa pili.

 

Makosa ambayo yamefanyika msimu uliopita ni mbaya kurudiwa tena kwani kutafanya timu zicheze kwa presha kubwa kutafuta ushindi.

 

Tukiachana na masuala ya maandalizi ya ligi kwa mechi hizi za mzunguko wa kwanza ninapenda pia nizungumzie suala la timu yetu ya Taifa ya Tanzania pamoja na mashabiki.

 

Imekuwa ni ajabu kuona kwamba kuna mashabiki ambao wanajipanga kuizomea timu ya Taifa ya Tanzania uwanjani ikicheza na timu ya Tunisia.

 

Hili limenipa mshtuko mkubwa na kunifanya nijiulize mara mbili inawezekanaje Mtanzania unamzomea Mtanzania mwenzako tena akiwa kwenye majukumu ya kuijenga Tanzania?

 

Nilipojaribu kufuatilia ukweli na sababu ni ipi eti inaelezwa maneno ya kocha siyo ya kizalendo anaonesha upendeleo katika kazi yake. Hii ni mbaya na inapaswa isipewa sapoti kwa kuwa sisi ni Watanzania na timu yetu ni Taifa Stars.

 

Makosa ambayo ameyafanya kocha adhabu yake haihusiani na timu ya Taifa ya Tanzania. Ikiwa maneno yake ni mabaya kwa mashabiki bado kuna uhuru wa kuzungumza na kuangalia uzito wa maneno ambayo aliyasema.

 

Ikiwa kuna ukweli katika hayo hakuna haja ya kulalamika, sisi sote ni binadamu makosa yapo lazima kusamehe sasa shabiki unapoamua kuikomoa timu yako ya Tanzania haileti picha nzuri.

 

Ni wazi kwamba kila Mtanzania ana haki ya kusikilizwa na kutoa maoni yake kwa mujibu wa katiba ya Tanzania lakini hapaswi kuleta vurugu na kuvuruga kwa kuwa sio asili ya Mtanzania.

 

Rai yangu kwa mashabiki wote kwa sasa ni kuziweka kando tofauti zao na kuungana kufanya kazi moja kuipa sapoti timu ya Taifa ya Tanzania, masuala ya kuzomea na kugoma kwenda uwanjani muda wake umeisha hayo ni mawazo mgando.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic