KIUNGO namba moja kwa kupiga mipira iliyokufa na kutengeneza pasi za mwisho ndani ya Yanga, Carlos Carlinhos kwa sasa anatibu jeraha lake alilopata ndani ya Yanga ambayo inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania.
Nyota huyo raia wa Angola aliumia jana Oktoba 19 kwenye mazoezi ya timu yaliyofanyika Kigamboni jambo lililopelekea apewe huduma ya kwanza akisubiri ripoti kutoka kwa dokta ili kujua maendeleo yake.
Ndani ya Yanga kiungo huyo ametoa jumla ya pasi mbili na kufunga bao moja kati ya mabao saba ambayo yaliyofungwa na timu hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kuwa nyota huyo hajaumia sana kwa kuwa alipata mshtuko kwenye mazoezi hivyo mashabiki wasiwe na mashaka.
"Kweli Carlos alipata majeraha lakini si makubwa sana kwa sasa hivyo mashabiki wasiwe na mashaka katika hili atarejea kwenye ubora wake.
"Kwa sasa kikosi kinaendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Polisi Tanzania, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yao," amesema.
Yanga itacheza na Polisi Tanzania mchezo wa sita ndani ya Ligi Kuu Bara, Oktoba 22, Uwanja wa Uhuru saa 10:00 jioni.
Yanga ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 inakutana na Polisi Tanzania iliyo nafasi ya tano na pointi 11 baada ya kucheza mechi sita.
0 COMMENTS:
Post a Comment