November 5, 2020

 


BADO fungiafungia ya viwanja kwenye ardhi ya Bongo inaendelea jambo ambalo linazidi kuleta hisia mpya kila iitwapo leo kwamba awali wakati vinaanza kutumia nani aliruhusu viweze kutumika?


Kwa kinachofanywa na Bodi ya Ligi Tanzania,(TPLB) kufungia vile viwanja ambavyo havina ubora ninawapa pongezi kwa kuwa ili wachezaji wafanye kweli ni lazima pia hata sehemu wanayochezea nayo iwe rafiki.


Wengi walikuwa wanafuatilia sehemu za kukaa wachezaji wa akiba pamoja na mashabiki huku sehemu ya kuchezea ambayo ndiyo inaleta matokeo chanya ilikuwa ikipewa kisogo


Tumeshuhudia kwamba baadhi ya viwanja ambavyo awali vilifungiwa na TPLB kuweza kutumika vimefanyiwa maboresho na kwa sasa angalau vinaleta picha nzuri kwa kuwa muonekano wake umekuwa bora.


Karume wa Mara ambao unatumiwa na Klabu ya Biashara United, Gwambina Complex wa Mwanza ambao unatumiwa na Gwambina wenyewe ni miongoni mwa viwanja ambavyo vimefanyiwa maboresho.


Kikubwa ambacho kinatakiwa kwenye viwanja ambavyo vimeboresha ni kuendelea kuongeza juhudi na kuvifanya viwanja hivyo vizidi kuwa bora muda wote ili viendelee kutumika kwenye matumizi mengine.


Tunaona kwamba taratibu kuna mabaoresho ambayo yameanza kuonekana na wachezaji nao wameanza kuonyesha kwamba mabadiliko hayo yana faida kwao hasa katika suala la kupambana ndani ya uwanja.


Ile fungiafungia iwe somo kwa timu nyingine ambazo zinamiliki viwanja kwa kufanya maboresho kwenye sehemu ambazo hazipo sawa ili kuepuka adhabu.


Niliweka wazi siku moja hapa juu ya ugumu wa Uwanja wa Mkwakani katika kusaka matokeo pamoja na Uwanja wa Jamhuri, Dodoma mambo yalikuwa ni magumu kwa wakati wake.


Kwa kuwa wakati huu vimefungiwa ni fursa kwa wamiliki kuweza kuuboresha ili uweze kutumika kwa wakati ujao pindi utakapokuwa umekamilika.


Itakuwa ngumu ikiwa hakutakuwa na maboresho kuweza kuruhusiwa kutumika tena kwa kuwa mamlaka imeeleza kuwa itafanyia ukaguzi kabla ya kuruhusu uwanja kutumika.


Gharama za uendeshaji kwa timu ambazo zimeshazoea kutumia viwanja vyao ambavyo vimefungiwa hapo lazima itaongezeka hivyo ili kupunguza gharama ni lazima kwa timu husika kufanya ukarabati kwa upesi.


Msimu huu wa 2020/21 tunaona kwamba viwanja vingi vinakutana na adhabu kwa kufungiwa ili kufanyiwa maboresho ni muhimu kufuatilia pia namna ya kuboresha viwanja na sehemu za kukaa watazamaji kwa ajili ya kuona kwamba msimu unamalizka kwa aina ya kipekee.


Ndani ya uwanja ushindani umekuwa mkubwa na kila timu inapambana kupata matokeo hilo ni jambo la msingi kwa kila mmoja.


Pongezi kubwa kwa wachezaji wa timu zote ambao wanapambana kwa wakati huu ni kuona kwamba wanaweza kufikia malengo ambayo wamejwekeea.


Mashabiki wengi wanazidi kujitokeza uwanjani na wameona ushindani na soka tamu ambalo wengi wanapenda kuliona siku zote hicho ndicho kikubwa tunachohitaji kwenye soka.


Kikubwa ambacho kinahitajika ndani ya uwanja ni kuweza kutafuta ushindi kwa juhudi zote ili kuweza kufikia malengo ya timu ambayo imejiwekea.


Ikitokea tofauti na hapo na kuanza kuleta porojo na maneno kushindwa ni karibu kwa timu ambayo itashindwa kujiandaa vizuri na kuleta maneno mengi.


Sasa hapo ndipo utagundua kwamba mpira ni uwanjani maneno maneno hayasaidii kukuza soka letu, kila mmoja kwa wakati wake anapaswa kutimiza majukumu yake.


Kosa moja likalofanywa na timu litawagharimu na kuacha pointi tatu ziende kwa wapinzani. Haya ndiyo maisha ya mpira kila mmoja anapambana kutumia makosa ya mpinzani wake.


Muda wote wachezaji mnapaswa kuwa makini na wapinzani wenu ili kulinda matokeo na pia katika kupata matokeo ni lazima kila mmoja atumie kosa la mpinzani kupata ushindi.


Benchi la ufundi lina kazi la kutengeneza timu imara na yenye ushirikiano ambayo inaweza kutoa matokeo kwenye mechi zote ndani ya ligi.


Ule uzembe wa wachezaji pamoja na kushindwa kuheshimu mechi zilizo mbele ni chanzo cha kushindwa kupata matokeo mazuri.


Kila kipindi kina mbinu zake, wapo ambao wamekuwa wakifanikiwa kipindi cha kwanza na kufeli kipindi cha pili na wapo ambao wanafeli vipindi vyote viwili kikubwa ni maandalizi.


Ukitazama kuna timu ambazo kipindi cha kwanza huboronga na kuna timu ambazo huweza kufanya vizuri. Zipo ambazo zinafanya vizuri mwanzo kisha zinapotea jumla.


Kuna ushindani mkubwa kwa sasa kwenye ligi na wachezaji wanapaswa wajitambue wasibweteke na mafanikio ya muda wanayopata ama kuvunjika moyo kwa matokeo mabaya.


Mpira hautabiriki kila mmoja ana nafasi ya kupata matokeo bila kujali yupo vipi jambo la msingi tu awe amejiandaa sawasawa.


Kwa timu ambazo zimekuwa na mwenendo mbovu benchi la ufundi lifanye kazi ya kurekebisha makosa na kutumia mbinu mpya kupata matokeo.


Wakati wa kufanya hayo mabadiliko ni sasa na 
mashabiki pia sapoti yenu ndani ya uwanja ni muhimu kwani kwa kufanya hivyo kunaongeza morali kwa wachezaji.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic