UONGOZI wa DStv Tanzania Januari 8, 2021, umeikabidhi timu ya Global FC jezi za nyumbani na ugenini kwa ajili ya michezo ya kirafiki na mashindano mengine ambayo itashiriki kwa msimu wa 2021.
Makabidhiano hayo yamefanyikafika katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam ambapo zitatumika rasmi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya DStv Tanzania unaotarajiwa kuchezwa Januari 31,2021.
Mkuu wa Masoko wa DStv Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo, amesema kuwa lengo kubwa la mchezo huo ni kuongeza ushirikiano zaidi kwa mwaka 2021.
Akizungumza na wafanyakazi wa Global Group wakati wa makabidhiano, Shelukindo alisema kazi kubwa ya DStv ni kuendelea kuwa karibu na wale ambao wanafanya nao kazi kila siku.
“Tumekuwa tukifanya kazi na Global Publisher kwa muda mrefu, siyo kwa kuwa tuna mchezo nao wa kirafiki tu mwishoni mwa mwezi huu, Januari, hapana ni muda mrefu kwa kuwa kazi zetu na kile ambacho wanakifanya wao vinategemeana.
“Huwezi kuzungumzia masuala ya michezo kwa sasa bila kuitaja DStv kwa kuwa inabeba kila kitu mpaka masuala ya movie na kila mtu anafurahia huduma zetu, hivyo mchezo tutacheza nao na tukiwafunga wataendelea kufurahia huduma zetu. Wateja wetu wazidi kutupa sapoti mwaka huu mpya wa 2021 tunakuja kivingine,” alisema.
Naye Mhariri Mtendaji wa Global Publisher, Saleh Ally alisema kuwa watazidi kuongeza ushirikiano na DStv kwa kuwa wamekuwa nao kwa muda mrefu, jambo ambalo limewafanya wamekuwa ni familia.
“Kwa sapoti ambayo tunapeana na DStv ni kubwa na inatufanya nasi tunazidi kuongeza nguvu katika kuboresha familia hii ambayo ni bora na yenye furaha, ninaona wametuletea jezi ilhali wanajua kwamba timu yetu inakwenda kuwafunga, ila yote kwa yote huu ni mwanzo ndani ya 2021,” alisema Ally.
Wakati huohuo, nahodha wa Global FC, Wilbert Molandi, amesema sapoti waliyoipata kutoka DStv ni kubwa na wanaamini kwamba wataendelea kushirikiana.
“Tutazidi kushirikiana na DStv kwa kuwa wamekuwa bega kwa bega katika kazi ambazo tunazifanya, ni familia moja, hivyo lazima tuzidi kuongeza nguvu ukizingatia kwamba mwaka 2021 unaanza. Kwenye mchezo wetu wachezaji wetu wapo vizuri kutakuwa na burudani,” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment