January 13, 2021


 TAYARI ipo wazi kwa sasa fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Uwanja wa Amaan ni kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga.

Kwa kiasi fulani mashindano ya msimu huu wa 2021 yamekuwa na ushindani mkubwa kwa timu ambazo zilikuwa zinashiriki.

Tunaona kwamba kila timu ndani ya dakika 90 ilikua inapambana kusaka ushindi. Hili ni jambo ambalo linahitaji pongezi kwa washiriki wote ambao wameweza kuishia njiani kwenye mashindano haya.

Bado kwa wenyeji kama ambavyo awali nilisema kuwa wamekuwa na mwendo wa kusuasua kutafuta ushindi imezidi kuendelea ambapo na msimu huu pia wameishia njiani mapema kwenye hatua za mwanzo.

Kwa haya ambayo yametokea ni somo kwa wenyeji kwa ajili ya msimu ujao ili kufanya kazi vizuri na kupata matokeo chanya kwenye mechi ambazo watashiriki.

Mabigwa watetezi Mtibwa Sugar nao watakuwa kwenye makochi kutazama mtifuano wa leo wa nani atakuwa mrithi wa kombe lao.

Haikuwa kazi nyepesi kwa Mtibwa Sugar kuweza kufikia mafanikio ambayo waliweza kufikia msimu uliopita wa 2020 baada ya kuwafunga Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.

Msimu huu wametolewa na Simba kwenye hatua za mwanzo kwa kufungwa mabao 2-0 hii inamaanisha kwamba msimu huu walikuwa kwenye mwendo mbovu.

Timu tisa ambazo zilishiriki na makundi yao matatu kila timu ilionekana kwamba ina jambo ambalo inahitaji kulifanya awali ila dakika 90 ziliamua matokeo yatakuaje.

Mwisho wa siku matokeo ambayo yametokea ni haya ambayo wapo nayo kwa sasa kwa kuwa matokeo ya dakika 90 hayawezi kubadilika kwa namna yoyote ile.

Wapo wachezaji ambao waliweza kupata nafasi kwenye vikosi vyao na kufanya kweli wanastahili pongezi kwa kuwa kazi ni muhimu kufanyika muda wote ndani ya uwanja.

Wakati huu kwa wachezaji wenye akili hutumia kuonyesha uwezo wao wote ili kulishawishi benchi la ufundi liweze kuwapa nafasi kwenye timu zao pale mashindano yatakapofika ukingoni.

Makocha pia nina amini kwamba kwa mechi ambazo wameshuhudia ndani ya uwanja wamepata aina ya kikosi ambacho wanakihitaji ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na mashindano mengine ambayo yanatarajiwa kuendelea.

Na ningependa niwakumbushe wachezaji kwamba kwa wakati huu bado dirisha dogo lipo wazi wanaweza kupata sehemu ya kutokea ikiwa watapambana.

Fainali itakuwa na ushindani mkubwa ila tunapenda kuona kwamba inachezwa kwa haki na sheria zote zinafuatwa kuanzia kwa waamuzi na wachezaji pia kufanya vizuri.

Ikumbukwe kuwa mashindano haya yanarushwa duniani na kufanya iwe ni sehemu ya kutangaza vipaji vyao nje na ndani ya Zanzibar. Hivyo wale wajanja watakuwa kazini kwenye kazi nyingine.

Nina amini kwamba wachezaji kwenye jezi zao kuna majina yao pamoja na namba zao jambo linalofungua njia kwa upande wa kujitangaza.

Wakala akikubali uwezo wa mchezaji fulani hatatakuwa na wasiwasi kuanza kumfuatilia mchezaji anayemtaka bali atakaa chini na kuanza kufuatilia rekodi za mchezaji huyo.

Muhimu kwa wachezaji ambao watakuwa kwenye fainali leo kupambana kwa hali na mali kusaka ushindi kwa ajili ya timu zao.

Nina amini kwamba ushindani utakuwa mkubwa na kila timu inahitaji kupata taji hilo.

Kwa waandaaji pia ni muhimu kuzidi kuboresha mashindano haya ili yazidi kuwa na mvuto kwa kuwa mwanzoni ilikuwa na mvuto mkubwa.

Uwepo wa timu kutoka nje ya Bongo ambazo zilikuwa zinakuja kushiriki na kuleta ushindani lilikuwa ni moja ya jambo ambalo linazidisha uzuri wa mashindano.

Ila kibaya ilikuwa ni kwamba pale wageni wanapofanye kweli na kusepa na kombe wakiwa ugenini hili pia nalo linapaswa litazamwe kwa wakati ujao ili wenyeji waweze kubaki na taji la mapinduzi.

Mashabiki pia ni wakati wenu wa kujitokeza ndani ya uwanja kuona burudani. Kila timu inaonekana kujipanga kusaka ushindi.

Ni wakati wa benchi la ufundi pia kutazama mapungufu na kuyafanyia kazi ili pale ligi itakapoanza kila kitu kitakuwa sawa.

Fainali pia itoe picha kwamba ushindani upo na kila timu inaweza kupata ushindi ndani ya dakika 90. Tunahitaji kumpata bingwa wa haki uwanjani.

Kuanzia waamuzi na wachezaji wanajukumu la kujituma na kufanya kazi kwa juhudi kusaka ushindi ndani ya uwanja na inawezekana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic