JERAHA la mbavu alilolipata mshambuliaji wa Klabu ya Yanga, Yacouba Songne, limeendelea kuipa hofu Yanga juu ya uwezekano wa kukosa huduma za nyota huyo kwenye michezo ijayo.
Yacouba aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Yanga, ambapo mpaka sasa amehusika kwenye mabao nane, akifunga mabao manne na kuasisti mara nne.
Meneja wa kikosi cha Yanga, Hafidh Saleh, amesema raia huyo wa Burkina Faso anaendelea na matibabu ya jeraha la mbavu na ndiyo sababu ya kukosekana kwenye mchezo wa Desemba 31 dhidi ya Tanzania Prisons.
"Mshambuliaji wetu Yacouba bado anasumbuliwa na jeraha la mbavu alilolipata kwenye mchezo dhidi ya Ihefu na licha ya kwamba hali yake siyo mbaya, lakini bado anaendelea na matibabu na ndiyo maana kocha aliamua kumpa mapumziko maalum yaliyomfanya akosekane kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.
“Lakini timu yetu ya matabibu inaendelea kufanya kila jitihada za kuhakikisha hali yake inarejea kama kawaida na anarudi uwanjani mapema iwezekanavyo ili kuendelea kutumikia kikosi,” amesema Saleh.
0 COMMENTS:
Post a Comment