MASHINDANO ya Mapinduzi Cup kwa sasa yapo
karibu kuweza kuanza kurindima visiwani Zanzibar ambapo kuna timu zinazoshiriki
Ligi Kuu Bara zinakwenda kushiriki.
Mtibwa Sugar ambao ni mabingwa watetezi
wapo ndani ya timu ambazo zitakuwa na kazi ya kusaka ubingwa kwa msimu wa
2020/21.
Mbali na Mtibwa Sugar kuna Yanga, Simba,
Azam FC, Namungo FC zote hizi zimejumuishwa kwenye orodha ya timu zitakazokuwa
na kazi ya kusaka ushindi.
Mbali na hawa wageni wenyeji wao ni pamoja
na Chipukizi, Jamhuri,Malindi,Mlandege hawa nao pia watakuwa na kazi ya
kulisaka taji hili la heshima.
Uzuri ni kwamba kila timu ina nafasi ya
kutwaa taji hili hivyo kikubwa ni kuweka mipango makini ambayo itaipa nafasi
timu husika kutwaa taji hili la heshima.
Kwa waandaaji nina amini kwamba changamoto
ambazo walizipata msimu uliopita zitakuwa zimefanyiwa kazi na kuyaandaa
mashindano katika hali ya utofauti zaidi.
Kwa sasa mambo mengi yamebadalika na mipango
pia inabidi ibadilike ili kwenda sawa na ushindani uliopo kwenye uwanja wa
mpira kiujumla bila kumuacha hata mmoja nyuma.
Nasema hivyo kwa sababu miaka ya nyuma
ushindani ulikuwa ni mkubwa na timu nyingi ambazo zilikuwa zinashiriki zilikuwa
zinanguvu kubwa hali ambayo ilikuwa ni ngumu kuweza kumtambua mshindi.
Kila mmoja alikuwa anapiga hesabu za kuwa
bingwa hali ambayo ilifanya kila mchezo kuwa na msisimko wa kipekee.
Tofauti kabisa na msimu uliopita ambapo ni
timu moja tu ambayo ilikuwa inasema hadharani kwamba inahitaji kupata ubingwa
huku wengine wakishiriki bila kuonyesha nia ya kutwaa ubingwa.
Hivyo ipo wazi kwamba ushindani kwa msimu
uliopita mambo hayakuwa mazuri kwa mashabiki pamoja na timu ambazo ziliingia
ndani ya uwanja.
Timu shiriki zote zilikuwa zimebwana na
ratiba ya Ligi Kuu huku nyingine zikiwa zinashiriki mashindano ya kimataifa.
Hata wakati huu pia mambo yanaonekana kuwa
hivyo kwa sababu tayari kuna mashindano ya kimataifa na zipo timu ambazo zina
kibarua cha kufanya na zinashiriki Kombe la Mapinduzi.
Simba na Namungo FC wana kibarua kimataifa
kwenye mechi zao za marudio hivyo kazi kubwa kwao itakuwa ni kujipanga vizuri
namna gani wanaweza kufanya vizuri kwenye haya mashindano.
Kila timu inapenda kufanya vizuri ila ratiba
muda mwingine huwa zinakuwa si rafiki kutokana na wachezaji kutakiwa kushiriki
kwenye mashindano mengine.
Somo jipya kwa waandaaji ni kwamba
wanapaswa waangalie namna mpya itakayowasaidia waweze kuibuka na mvuto mpya
hasa kwa kuanzia na maboresho ya ratiba.
Wakifanikwa kucheza na ratiba itawafanya
wawe na uwanda mpana kwa washiriki kuwa huru kucheza kwa ushindani bila kuwa na
hofu yoyote kitaifa na kimataifa.
Hapa pia inapaswa iwe somo kwa wenyeji nao
waweze kuonyesha ushindani mwanzo mwisho kwenye haya mashindano.
Imekuwa kawaida kwao kushuhudia taji
likirejea Bara na kuwaacha wenyeji wakiishia njiani jambo ambalo halipendezi.
Ni wakati kwa wenyeji nao kufungua njia na
kuleta ushindani wa kweli wakiwa ni wenyeji.Inawezekana na kila kitu kipo wazi
maandalizi ni muhimu.
Nina amini kwamba utakuwa ni mwaka mpya wa
2021 na kila timu itakuwa na mipango mipya tofauti na msimu uliopita wa 2020.
Kila mmoja kwa sasa ana kazi ya kuweza
kuweka mipango yake sawa. Kuanzia ndani ya Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Pili na
la Kwanza.
Pia Ligi ya Wanawake nayo pia inapaswa
ipewe kipaumbele ili kupata bingwa halali jambo litakaloleta furaha kwa
mashabiki na viongozi wa timu.
Kwa zile ambazo zilikuwa zinakwama kupata
matokeo ndani ya mechi zao ambazo wamecheza ni wakati wao wa kujipanga upya na
kuanza kwa namna nyingine.
Ni muda wa kumaliza hesabu kwa kuwa
mzunguko wa pili ushindani wake huwa unakuwa tofauti zaidi ya mzunguko wa
kwanza.
Hesabu ambazo zimekwama kukamilika mzunguko
wa kwanza inapaswa zimaliziwe mzunguko huu wa pili ambao huwa unakuwa na
ushindani mwanzo mwisho.
Wakati huu mbivu na mbichi zitajulikana kwa
zile ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja na kwa zile ambazo zinawania
taji la Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili ni muda wa mavuno.
0 COMMENTS:
Post a Comment