MIPANGO mingi iliyokuwa imepangwa kufanyika ndani ya mwaka 2020 inaweza kuwa imekamilika kwa asilimia kubwa na inaweza kuwa haijakamilika pia kwa asilimia kubwa.
Yote ni matokeo ya hesabu ambazo zilikuwa
zinafanyika. Kuanzia ndani ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Wanawake, Ligi Daraja la
Kwanza hata lile la pili bila kusahau na ligi ya mkoa.
Yapo mengi ambayo yamekuwa yakiendelea ila
kwa sasa ni muda wa kumaliza tathimini kwa yale ambayo yalikuwa yamepangwa
kufanyika ndani ya mwaka uliopita ambao unabaki kwenye rekodi.
Kushindwa kufikia malengo ambayo timu
ilikuwa imejiwekea, mchezaji mmojammoja pamoja na uongozi kiujumla sio mwisho
wa mipango.
Bado maisha ya soka lazima yaendelee na
ushindani pia unapaswa kuedelea kuwa mkali bila kupungua ndani ya Bongo.
Pongezi kwa wale ambao wameweza kufanya nusu ya kile ambacho walihitaji kukifanya. Wapo pia ambao wameweza kufanikisha kwa asilimia 100 mipango yao.
Achana na hao pia wapo ambao hawaelewi ikiwa kama
wameweza kutimiza yale ambayo waliyapanga ama la kwa kuwa bado wanapambana.
Jambo la msingi ni kuanza kujipanga kwa
ajili ya mwaka huu ili kuweza kuweka mambo sawa na kuomba Mungu azidi kutoongoza
katika yale ambayo tumepanga kuyafanya.
Ukweli ni kwamba binadamu anapanga na Mungu
anapanga pia juu yetu hivyo ni lazima kuwa watulivu katika kila jambo.
Ukiachana na hayo sasa twende kwenye mada
ya leo ambapo ningependa kuzungumzia kuhusu Ligi ya Wanawake Tanzania.
Wengi wanapenda kuiita Serengeti Lite
Premier League kutokana na mdhamini wao mkuu kuwa bega kwa bega na klabu hivyo
wadau wengine ni muhimu kujitokeza.
Msimu huu wa 2020/21 kumekuwa na ushindani
wa kipekee huku kwenye Ligi ya Wanawake ambapo kila timu inaonekana kujipanga
kufanya vizuri.
Licha ya uimara uliopo kwenye ligi hii bado
kuna matatizo kwa upande wa timu nyingi kushindwa kumudu gharama jambo ambalo
linaleta maumivu kwa wachezaji pamoja na viongozi.
Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF)
wanapaswa wajipange sawasawa kulidhibiti hili kwani kwa kuanza kuvurunda mwanzo
kutafanya ule msisimko ambao umeanza kuishia njiani.
Jambo lingine pia la kuzingatia ni ubora wa
viwanja ambavyo vitakuwa vinatumika katika kusaka matokeo ndani ya uwanja.
Timu zote 12 zinazoshiriki Ligi zina nafasi
ya kufanya vizuri ikiwa zitazingatia maandalizi mazuri kila kitu ni maandalizi
na wakati wa kufanya maandalizi ni sasa kupitia makosa ambayo yanafanyika.
Benchi la ufundi pamoja na vongozi
wanapaswa waangalie kwa umakini ni wapi wanapokosea ili wafanikiwe kusonga
mbele na kupata matokeo katika michezo yao ijayo.
Kikubwa ambacho wachezaji wanapaswa
wakifanye ni kujitambua na kubeba nguvu ya kujiamini kwamba wanaweza kupata
matokeo uwanjani kwa kupambana bila kutegemea kubebwa.
Kila baada ya kushinda mchezo mmoja iwe ni
mwanzo wa maandalizi kwa ajili ya mchezo unaofuata bila kubweteka.
Imani yangu ni kwamba ushindani ukiwa
mkubwa huku kwa Wanawake itaongeza nguvu ya kuwa na timu ya Taifa ya Tanzania
yenye nguvu.
Kama wachezaji mtaamua kujituma uwanjani
pasipo kumtegemea mchezaji mmoja maana yake ni kwamba mtapata matokeo chanya
ambayo mnayafikiria.
Ila kama kila mmoja atakuwa anajiona yeye
ni bora kuliko mwingine hapo ndipo tatizo linapoanzia hasa kwa kufanya
ushindani na ule ubora kupotea.
Uongozi wa timu zote kwa sasa una jukumu la
kutazama wapi ambapo walikuwa wanakwama kupata matokeo kwenye mechi zao
zilizopita.
Kila mmoja akubali kujitoa kwa ajili ya
timu na afanye kazi kwa juhudi akiwa uwanjani bila kujali anacheza na nani
uwanjani.
Tunaamini kwamba tunaweza kufanya mapinduzi
katika soka la Wanawake na kuipeperusha bendera ya taifa nje ya nchi.
Mpira kwa sasa ni biashara na ili ufanikiwe
kibiashara ni lazima ushindane na usikubali kushindwa ili uwe kwenye ushindani
siku zote.
Hivyo ni muhimu wachezaji wetu pia kuweka
kwenye akili kwamba wapo sokoni wanapoingia ndani ya uwanja na wanaweza kufikia
mafanikio na kucheza nje ya Bongo.
Nina amini kwamba mwaka mpya wa 2021
kutakuwa na ushindani mkubwa na matokeo tofauti kwa timu zile ambazo zilikuwa
hazifanyi vizuri.
0 COMMENTS:
Post a Comment