UONGOZI wa Simba umesema kuwa upo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo na wanatambua kwamba utakuwa na ushindani mkubwa ila hawana hofu kwa kuwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi lipo tayari.
Simba itamenyana na Klabu ya AS Vita leo kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes.
Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa utachezwa Uwanja wa Des Martyrs,Congo, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa wachezaji wapo tayari kimwili na kiakili kwa ajili ya mchezo wa leo na wameahidi kupambana kuleta heshima kwa Tanzania na kuomba dua kutoka kwa mashabiki.
"Watanzania ninapenda kuwaambia kwamba kila kitu kipo sawa, wachezaji wanajua kwamba wanatakiwa kufanya nini kwenye mchezo wa leo na tunakwenda kufanya kazi kwa kujituma mwanzo mwisho.
"Wachezaji wapo tayari kiakili,wapo tayari kimwili na kwa msafara ambao tupo nao huku wote wapo tayari na wametuahidi kuweza kupambana ndani ya uwanja kusaka ushindi.
"Kwa mashabiki wetu tunaomba dua zenu kwani huu mchezo wetu wa leo ni mgumu na una ushindani mkubwa ila niwatoe hofu kwamba tunajiamini na wachezaji wana morali kubwa ukizingatia ni mchezo mkubwa siku ya leo," amesema.
Barbara Gonzalez, Mtendaji Mkuu wa Simba,(CEO) amesema kuwa wamekaa na wachezaji na kuzungumza nao ambapo wamewaahidi kuwapa zawadi nzuri ikiwa wataanza na ushindi kwenye mchezo wa leo.
Kila la kheri MNYAMA. MUNGU atujalie matokeo chanya
ReplyDelete