NA SALEH ALLY
KUNA malalamiko mengi sana katika soka la wanawake kuhusiana na aina ambavyo mambo yamekuwa yakiendeshwa, hili linapaswa kufanyiwa kazi.
Kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kufuatilia soka la wanawake na kukua kwake, nitawakumbusha kidogo kwamba ilikuwa ni kazi ngumu sana kufikia hapa lilipo.
Bahati mbaya sana, walioshiriki kulipambania wengi hawapo leo hii, mfano kwa makocha kama Juma Bomba aliyekuwa Sayari FC au wamiliki kama Marehemu Dk Maneno Tamba aliyekuwa mmiliki wa Mburahati FC, moja ya timu chache zilizowakuza wasichana kisoka.
Wakati huo ilikuwa Sayari FC na Mburahati FC, halafu baada ya hapo ni timu ya taifa. Lakini baadaye mambo yakaendelea kubadilika na timu zikaanza kuanzishwa na mwisho ikawa si Dar es Salaam tu, badala yake Mwanza, Arusha, Pwani na kadhalika na sasa unaona kuna timu imara hadi Kigoma, hili ni jambo bora sana.
Ndani ya historia hii, kuna watu wamejitolea na kuumia sana. Lengo lilikuwa ni kulikuza soka la wanawake kwa mapenzi yao, leo hii hawajulikani au kutajwa lakini wameifanya kazi yao vizuri.
Wakati hao walijitolea, wako ambao wanaendeleza leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeendelea kufanya vizuri katika maendeleo ya mpira wa miguu wa wanawake lakini ndani yake kuna matatizo mengi ambayo yamekuwa yakiendelea kimyakimya na huenda yanaonekana kama si sahihi hivi kuyazungumzia, jambo ambalo ni kosa kubwa.
Zaidi ya miezi minne, nilizungumza na moja ya wachezaji wa klabu moja ya wanawake ambao walielezea kuhusiana na kiongozi mmoja ambaye anasimamia timu yao kuwanyanyasa na wakati mwingine katika masuala ya kijinsia.
Walilalamika kuhusiana na kuwapendelea baadhi wakiwatuhumu ni wapenzi wake, lakini amekuwa akiwadhulumu hata haki zao za malipo na hawana uwezo wa kusema kokote kuhusiana na hofu.
Hivi karibuni tena, mchezaji mmoja kutoka Malawi ambaye aliletwa kufanya majaribio nchini, akaingia kwenye mgogoro mkubwa akidai alitapeliwa na mmoja wa viongozi wa timu hiyo ambaye alimlaghai kuvunja mkataba na timu yake kwao Malawi na alipofika hapa mambo yakawa tofauti na hata nauli ya kurejea kwao likawa jambo gumu tena.
Mgogoro huu uliingiliwa na waandishi ambao walilifikisha suala hili katika uongozi wa juu na baadaye kukawa na msaada wa kuhakikisha hili suala linapata mwafaka.
Kuna kiongozi mwingine pia nimesikia akilalamikiwa, huyu amekuwa akiwabagua wengine na wakati mwingine kumpa kocha wa timu wakati mgumu kutokana na uamuzi wake wa kutaka kuona anaowataka yeye wanacheza.
Soka la wanawake kwa hapa nchini linakua, kukua kwake hakuwezi kukafanya mambo yakaendelea kubaki kama ambavyo ilikuwa zamani. Mabadiliko yataanza kujitokeza, ugomvi wa kimaslahi, unyanyasaji na kadhalika lazima utaongezeka.
Huu ndiyo wakati mwafaka sasa kwa TFF kuanza kujiimarisha ikiwa ni pamoja na kutengeneza kanuni ambazo zitawabana viongozi wanaofanya kazi katika klabu hizi za wanawake kuhusiana na unyanyasaji na kadhalika.
Kumbuka wanaoshiriki huku ni wasichana au wanawake, mambo utakayoyasikia huku lazima yatapishana na soka la wanaume. Inawezekana wakati mwingine wahusika watakuwa wanayazidisha kutokana na walivyo hasa wanapokutana kinadada au wanawake. Lakini lazima kutakuwa na sehemu ambayo hawatendewi haki kwa manufaa ya wahusika hasa wenye vyeo.
Maana yake, ili mambo yaende vizuri, lazima kuwe na hofu kwa wale watendaji ambao watakuwa wanajua kama watatumbukia katika mambo hayo na kubainika, maana yake watakuwa katika matatizo makubwa. Hii itafanya mambo yaende kwa usahihi na haki, jambo ambalo litaongeza kasi ya kukua kwa mchezo huo badala ya kuutengenezea hofu kubwa zaidi katika makuzi yake.
We mwenyewe unatoa habar kwa kuficha ficha, unataka wasomaji tufanyeje sasa
ReplyDelete