KUMEKUWA na kasumba ya mashabiki, makocha pamoja na wachezaji kuwageukia waamuzi na kuwabebesha zigo la lawama pale wanapokwama kupata matokeo ama wakati mwingine wanaposhinda.
Kwa kuwa
kelele kwa waamuzi kwa sasa zimekuwa zikizidi kila leo ni muhimu kwa mamlaka
kuweza kulichukulia hili suala kwa uzito wa kipekee kwani linatibua utamu wa
ligi.
Wengi wanaokwenda
uwanjani hawapendi kuona makosa ya kizembe yakitokea na kwa waamuzi inabidi
watambue kwamba pale ambapo wanaamua hakuna anayeweza kufanya mabadiliko hapo
baadaye.
Kutokana na
kasi ya mechi kuwa kubwa kwa sasa nadhani kuna umuhimu wa Shirikisho la Soka
Tanzania,(TFF) kuangalia namna ya kufanya kuweza kuliondoa kabisa hili tatizo
la kelele za waamuzi.
Ipo wazi
waamuzi wanafanya kazi yao vizuri kwa kufuata sheria 17 ila kuna wakati
wanapata kigugumizi kwa kutaka kuweka usawa kwa sababu ya makosa ambayo
yamepita ama kushindwa kuelewana ndani ya uwanja hili sio sawa.
Kwa wale
ambao watapewa jukumu la kusimamia mechi zote itapendeza wakifuata sheria 17.
Ikiwa mchezaji anastahili kupewa kadi nyekundu kwa mujibu wa sheria na apewe
hata kama itakuwa ni kwa timu nzima haki itendeke.
Pia sehemu
ya penalti hata kama ikitokea timu ikapata penalti tatu hata saba zifunikwe na
zipigwe tu hakuna haja ya kuhofia eti manenomaneno ama presha ya mchezo hiyo
hakuna.
Wapo waamuzi
ambao wanafanya kazi zao vizuri sasa hawa kazi yao nzuri inapotezwa na baadhi
ambao wanavurunda kwa kukusudia ama bahati mbaya.
Wachezaji
wakiwa ndani ya uwanja wana kazi kubwa ya kutafuta matokeo ila inapotokea
wanakwamishwa na juhudi za mwamuzi haileti picha nzuri.
Wakati
uliopo na kwa mechi zinazofuata itakuwa vizuri waamuzi wakafanya kazi yao bila
presha ama shinikizo katika maamuzi yao ndani ya uwanja.
Ipo wazi na
inaonekana kwamba msimu huu kwa kuwa timu ni chache ushindani utakuwa mkubwa.
Hivyo waamuzi nao pia wajipange kwenda sawa na kasi ambayo ipo ndani ya uwanja.
Mzunguko wa
pili umeanza kwa utofauti ndani ya ligi ambapo kila timu imekuwa ikipambana
kusaka ushindi kwenye mechi ambazo itacheza.
Kutokana na
ushindani huo ni muhimu kwa timu pamoja na wachezaji kuendelea kujipanga
vizuri. Hakuna timu ambayo inaweza kukubali kupoteza mchezo ilihali inahitaji
ushindi.
Inahitajika
umakini mkubwa kwa waamuzi katika kutoa maamuzi yao. Ni wazi kwamba kwa sasa
kila mchezaji amekuwa akitafuta sababu pale timu inapokwama kushinda.
Wengine
wamekuwa wakiangukia kuwapa lawama waamuzi huku wengine wakidai ni kutokana na
miundombinu kutokuwa rafiki.
Jambo la
msingi kwa sasa ni kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa usahihi uwanjani hilo
litafanya zile kelele na lawama kupungua.
Waamuzi kwa
nafasi ambao wanapewa kufanya kazi ni muhimu kufanya kazi kwa juhudi na kutimiza
zile sheria 17 za mpira na itafanya ligi izidi kuwa imara.
Uimara wa
ligi utafanya maendeleo ya soka letu kuzidi kupanda kila wakati na hilo ni
faida kwa taifa letu kiujumla kwa kuwa mafanikio yanatuhusu sisi wenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment