MOHAMED Badru, Kocha Mkuu wa Gwambina FC amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.
Majira ya saa 1:00 usiku kutakuwa na kazi ya wanaume 22 kusaka pointi tatu muhimu kwa ajili ya kuweza kufikia malengo yao.
Walipokutana Uwanja wa Gwambina Complex, ubao ulisoma Gwambina 0-0 Yanga hivyo leo kila timu inahitaji kusepa na pointi tatu, Uwanja wa Mkapa.
Gwambina inakumbuka kwamba imetoka kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya KMC, Uwanja wa Uhuru jambo ambalo Badru amesema kuwa makosa yaliyopita wameyafanyia kazi.
"Tunacheza na vinara wa ligi, hilo tunalijua na tunatambua kwamba utakuwa mchezo mgumu ila tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo.
"Kikubwa ni kwamba wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu na tunaamini kwamba tutapata matokeo chanya, mashabiki wajitokeze kutupa sapoti," amesema.
Kwenye msimamo wa ligi, Gwambina ipo nafasi ya 12 na ina pointi 30 inakutana na Yanga iliyo nafasi ya kwanza na pointi 54.
0 COMMENTS:
Post a Comment