BAADA ya takribani miezi miwili kupita, hatimaye Jumamosi iliyopita kikosi cha klabu ya Yanga, kilifanikiwa kupata tena tabasamu la matokeo ya ushindi baada ya kuwafunga Biashara United bao 1-0.
Kabla ya mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa mwisho Februari 20, mwaka huu pale walipoifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 katika dimba la Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam. Baada ya ushindi huo dhidi ya Mtibwa Yanga ilipoteza mchezo mmoja na kupata sare mbili mfululizo.
Kwa namna ambavyo Yanga walicheza Jumamosi, watu wengi wameona kuna kitu kimeongezeka ndani ya klabu hiyo kulinganisha na namna walivyocheza michezo yao iliyopita.
Bila shaka nyongeza hiyo ya kiuchezaji imetokana na mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa na Mwambusi ndani ya kikosi hicho, ambapo sura mpya ambazo hazikuwa zikipata nafasi ya kucheza mara kwa mara zimeanza kuonekana tena uwanjani.
Mashabiki wa Yanga wameonekana kuridhishwa sana na mabadiliko hayo hasa katika safu ya ulinzi, ambapo utawala wa muda mrefu wa pacha ya Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto imeanza kupotea, na sasa pacha mpya ya Dickson Job na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ imeanza kuchukua nafasi.
Ni mapema sana kusema pacha hiyo itaweza kuhimili vishindo vya mwishoni mwa Ligi lakini kuna tumaini kubwa unaliona kwa kocha Juma Mwambusi juu ya hilo.
Yanga imesaliwa na michezo tisa pekee ili kukamilisha hesabu zao kwenye ligi msimu huu, na bila shaka haipaswi kuruhusu kufanya makosa hata kidogo kama kweli wanataka kulinda matumaini yao ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Ushindi dhidi ya Biashara kwa kiasi fulani umepelekea kupungua kwa manung’uniko na lawama kutoka kwa mashabiki, ambao wamekuwa wakitafuta mchawi kila timu yao inapoonekana kufanya vibaya.
Angalau zile kelele za Waamuzi, viongozi na wachezaji kuhujumu timu zimeyeyuka kwa muda.
Hivi sasa viongozi na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kushikilia hapohapo, na kuzidi kuipa sapoti timu yao ili izidi kurejesha hali ya kujiamini na kupambana kwa ajili ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo yao iliyosalia.
Ukiangalia ratiba ya Yanga utagundua kuwa timu hiyo ina kibarua kigumu cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye michezo mitatu ijayo, ambapo Yanga watacheza na Gwambina Aprili 20, Azam Aprili 25, na kukutana na Simba Mei 8, kwenye dabi ya Kariakoo.
Hivyo ni wazi wadau wa klabu hiyo wanapaswa kushikamana sana ili kukamilisha ratiba hii kwani kama, watayumba kabla ya mchezo wao wa dabi na kuanza kulaumiana basi wajiandae kisaikolojia watakapokutana na Simba.
Yanga inaonekana kuanza na kheri
kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, na bila shaka Mwambusi na Yanga ya mwezi
mtukufu imeanza upya kama ilivyo kwa Arsenal ya kule Jijini London, England.
Uchambuzi wa Edibly Lunyamila.
Kwa uchambuzi huu na mwingineo usikose kufuatilia gazeti la Championi kila Jumatatu.
Naona UTO mnakujakuja kwa mbali kidogo
ReplyDelete