April 27, 2021


NGOMA inapigwa kwa kasi kwenye ligi kwa sasa ikiwa ni mzunguko wa pili na kila mmoja anapigania malengo yake ili kupata kile anachostahili.

Bado vita ya ubingwa ni mbichi kwa sasa ambapo zile zilizo tatu bora zinapewa nafasi ya kumtoa mbabe ambaye atasepa na taji hilo lenye thamani kubwa kwa timu.

Kuna Simba ambao ni vinara, wapo Yanga nafasi ya pili na Azam FC hapo wamejikita nafasi ya tatu bado wanazidi kutuniashana misuli kuona kwamba nani anasepa na ubingwa.

Ipo wazi kwamba bingwa mtetezi ambaye ni Simba naye malengo yake ni kuona anaweza kutetea taji hilo huku Yanga nao wakiweka wazi kwamba wanahitaji kulitwaa taji hilo baada ya kulikosa kwa muda mrefu.

Azam FC pia wao mdogomdogo wanasema kwamba wana jambo lao ambalo wanahitaji kutimiza hivyo kwa kuwa kila mmoja ana mechi mkononi ni suala la kusubiri na kuona.

Kama ilivyo ngumu kwenye ubingwa pia ni ngumu kwenye kushuka daraja pamoja na zile ambazo zitamaliza ndani ya 10 bora mchakato ni mkubwa na kila timu inahitaji ushindi.

Naona kwamba wengi wanashangaa imekuajekuaje Simba ikashinda bao 1-0 mbele ya Mwadui FC tena kwa mbinde ilihali timu hiyo ipo nafasi ya 18 ikiwa inapambana kubaki kwenye ligi msimu ujao?

Huu ni mpira na kila timu inastahili kushinda hivyo hakuna timu ambayo inapaswa kufungwa wala ambayo inapaswa kushinda muda wote.



Ikiwa hivyo basi isingekuwa na umuhimu wa kuwepo kwa mechi basi zile timu ambazo unadhani zinastahili kushinda zingekuwa zinakaa pembeni na kuziacha timu nyingine kushiriki. Kwa kuwa ni mpira basi ni lazima mchezo uchezwe.

Pongezi kwa Mwadui ila ninawapa neno kwamba walikuwa na kazi ya kuanza kwa gia hiyo tangu awali. Tunajua kwamba uchumi ni tatizo kubwa linalosumbua timu zetu ila kwani waliwezaje kucheza mbele ya Simba kwa kasi ile?

Kumbuka pia waliweza kucheza vizuri pia mbele ya Azam ambayo nayo ipo ndani ya tatu bora maana yake ni kwamba kila kitu kwenye soka kinawezekana.

Jambo kubwa ambalo ningependa lifanyike katika mechi hizi za mwisho ni lazima kuwe na usawa na mechi zichezwe kwa kufuata sheria 17 za mpira.

Mtu ashinde kwa kutumia nguvu zake mwenyewe na hakuna ujanjanja ambao utafanyika kwani tunahitaji kuona kwamba kila kitu kinakwenda sawa.

Lala salama kwa timu zote iwe ni ndani ya Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi Daraja la Kwanza ni muhimu kuweza kuona kwamba kila timu inashinda kwa haki.

Katika hili ipo wazi kwamba ni jambo la msingi kupata mshindi ambaye hatapata tabu akipanda ligi msimu ujao wa 2021/22 itasaidia kueleta ushindani mkubwa .

Kwa kuwa hizi ni mechi za mwisho na zina umuhimu mkubwa kwa kila timu kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya wafikie malengo waliyojiwekea.

Kikubwa kinachotakiwa kwa sasa ni kuona kwamba kila timu inafanya maandalizi mazuri ili kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja ambayo yatawapa kile ambacho wanakihitaji.

Wapo ambao wamekuwa wanapenda kuleta ugomvi ndani ya uwanja hayo yamepitwa na wakati ni muhimu kutulia na kufanya maamuzi kwa akili zaidi.

Hivyo wale wote ambao watakuwa uwanjani wapambane kutafuta matokeo ndani ya uwanja kupata matokeo chanya.

Kwenye Ligi Daraja la Kwanza tunataka kuona kwamba kila mechi inakuwa na mvuto pamoja na ushindani ule ambao unaonekana kwa kila mmoja kucheza na kupata ushindi.

Tunataka kuona kila timu inapata matokeo ambayo yanastahili kwao na wakimaliza kucheza wafurahi kile wanachokivuna na baada ya kushuka ama kupanda wasiwe na malalamiko.

Mechi za lala salama ni muhimu maandalizi yakawa mazuri katika kumalizia mechi hizi ambazo zimeshikilia maamuzi ya mechi za mwisho.

Tukija Ligi Kuu Bara ni muhimu kwa kila timu ikawa na uhakika wa kushinda mechi zote za nyumbani na ugenini bila mashaka yoyote.

Ipo nafasi ya kupata matokeo na kujinusuru kwa timu ambazo zina mechi mkononi ikiwa zitachanga vema karata zao kwa mechi ambazo zimebaki.

Ikiwa kila mmoja ataamua kufanya vizuri na akapata matokeo mazuri basi zitatimiza ndoto za kubaki kwenye ligi kwa ajili ya msimu ujao na ikishindikana basi zijipange kwa ajili ya maisha ya Ligi Daraja Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa zile ambazo zitapanda mpaka kufika ndani ya Ligi Kuu Bara ni lazima zijipange vizuri katika mechi zote ambazo watakutana nazo kwenye maisha mapya wakati ujao.

Tunataka kuona timu zenye ushindani ndani ya Ligi Kuu Bara na zile ambazo zitashuka daraja zikapambane pia ili kurudi huku ndani ya ligi.

Wasijisahau kwamba wanakwenda kwenye makazi mapya na wengine wanapanda kwenye makazi mapya ni lazima kujipanga vizuri hakuna namna.

Wachezaji wapambane ndani ya uwanja kwa hali na mali kwa ajili ya timu zao ambazo zinahitaji matokeo mazuri muda wote.

Itakuwa vizuri ikiwa kila mmoja atakuwa kwenye kutimiza majukumu yake na apambane kwelikweli kwani ndio kazi yake aifanye kwa ukamilifu bila ulegevu.

Imani yangu ni kwamba zile ambazo zitashuka zitakuwa zimejifunza na zitakuwa zimeshuka kwa haki huku zile ambazo zitapanda nazo zinapaswa kupanda kwa haki bila dhuluma.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic