KASI ya mshambuliaji wa Azam FC ambaye ni kinara wa kucheka na nyavu imeongezewa na benchi la ufundi hilo linaloongozwa na Kocha Mkuu, George Lwandamina akisaidiana na Kocha Msaidizi Vivier Bahati.
Ndani ya Ligi Kuu Bara, Prince Dube ni namba moja kwa kucheka na nyavu akiwa ametupia mabao 12 anafuatiwa na Meddie Kagere mwenye mabao 11 na John Bocco mwenye mabao 10 hawa ni wa Simba.
Akizungumza na Spoti Xtra, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier alisema kuwa kwa sasa wachezaji wote wana kazi ya kumtegenezea nafasi nyota huyo ili aongeze kasi katika ufungaji wake.
“Ili timu ipate ushindi ni lazima wawepo wafungaji ambao wanafunga, kwa sasa tunaye Dube ambaye anafunga tumewaambia wachezaji wote kwa sasa wanapaswa kumtengenezea nafasi za kufunga ili aongeze kasi yake.
“Mbali na yeye kuwa na uwezo wa kutengeneza mipango timu inacheza kwa kushirkiana ndio maana unaona kwamba mabeki nao wanatengeneza nafasi za kufunga pamoja na viungo ambao hawa wanapeleka mipira kwa washambuliaji,” alisema Vivier.
Dube ndani ya Azam FC iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo pia ametengeneza jumla ya pasi tano za mabao.
Mkononi ana tuzo moja ya mchezaji bora wa mwezi Septemba inayotolewa na Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu Tanzania Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment