May 6, 2021


KUELEKEA kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi unaotarajiwa kuchezwa Mei 8, Uwanja wa Mkapa, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, raia wa Ufaransa amekuwa akiwahimiza wachezaji wake kucheza mpira wa pasi fupifupi na kufunga pale wanapokaribia kwenye lango la wapinzani.

Simba imekuwa na mtindo wa kucheza pasi nyingi pale ambapo inawakabiri wapinzani wake katika uwanja, rekodi zinaonyesha kwamba walipocheza na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Mkapa na kufunga jumla ya mabao 5-0 walikuwa wakipigiana pasi 10 mpaka 15 pale wanapopata mpira mpaka kufika lilipo lango la wapinzani.

Mchezo wao wa mwisho kucheza Uwanja wa Mkapa kabla ya kuvaana na Yanga, Simba ilicheza na Kagera Sugar na ilishinda mabao 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho hatua ya 16 bora.

Ikumbukwe kuwa watani hao wa jadi walipokutana kwenye mzunguko wa kwanza Uwanja wa Mkapa, waligawana pointi mojamoja baada ya ubao kusoma Yanga 1-1 Simba.

Kwenye mchezo huo mbinu za Simba zilikuwa mikononi mwa Kagera Sugar kipindi cha kwanza kwa kuwa zile pasi zao zilikuwa zinakwama kupena kwenye ngome ya David Luhende.

Gomes amesema:"Nahitaji kuona wachezaji wanaweza kuwa kwenye kasi na kujiamini kwani mchezo wetu dhidi ya Yanga hautakuwa mwepesi kutokana na ushindani uliopo pamoja na nafasi.

"Kikubwa ambacho ninakiona kwamba kwenye mechi zetu ambazo zimepita tumepata matokeo mazuri hivyo inaongeza kwetu hali ya kujiamini na mpira wa pasi pamoja na kushambulia ni mbinu ambayo ipo kwa walimu wote," amesema.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza ya Gomes kuiongoza Simba na kukutana na Yanga kwenye Kariakoo Dabi kwa kuwa ile ya mzunguko wa kwanza, Kocha Mkuu alikuwa ni Sven Vandenbroeck.

Pia hata Nassredine Nabi naye itakuwa ni mara ya kwanza kumenyana na Simba kwenye Kariakoo Dabi kwa kuwa ule mchezo wa kwanza alikuwa yupo Mrundi, Cedric Kaze.

1 COMMENTS:

  1. Yani luhende peke yake ndo alizuia Simba isipige pasi kipindi cha kwanza?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic