May 25, 2021


OKTOBA 25, 2018 Kampuni maarufu ya michezo ya kubeti nchini ya SportPesa iliwashitua wadau baada ya kutangaza kuingia kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa na kumwaga mamilioni ya fedha kwa bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo.

 

Mwezi huu, SportPesa imetimiza miaka minne tokea ianze kufanya kazi nchini, lakini ina mengi ya kusimulia kama chachu ya maendeleo ya michezo na ushiriki mkubwa kwa jamii hapa nchini.

Mwakinyo kutoka mjini Tanga ni bondia ambaye tayari alishaanza kuwavutia Watanzania wengi kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa akioonyesha.

Tayari ilionekana ni kijana ambaye anairudisha Tanga katika ramani ya ubora katika ngumi za kulipwa baada ya mabondia kadhaa maarufu kutokea katika mkoa huo lakini baadaye ukatawaliwa na ukimya.

 

Mkataba wa miaka mitatu kati ya SportPesa na Mwakinyo, ulisifiwa sana na Serikali kupitia Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wakati huo, Dk Harrison Mwakyembe kwa kuwa wadau na hata Serikali iliamini SportPesa zaidi walijikita zaidi katika mchezo wa soka.

Katika mkataba huo, SportPesa ilimpeleka Mwakinyo nchini Uingereza ambako aliongozana na bondia mwanamama Mkenya, Fatuma Zarika kwa ajili ya maandalizi ya pambano lililofanyika nchini Kenya huku Mwakinyo akiandika rekodi ya kuwa Mtanzania anayecheza pambano kubwa la ugenini.

Mwezi mmoja nchini Uingereza haukuwa haba, lakini haukuwa mchache kwani Mwakinyo alikuwa akifanya mazoezi chini ya bondia nyota wa Uingereza, Tonny Bellew ambaye amekuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya bondia huyo.

Bondia huyo Mtanzania alielezea mengi kuhusiana na ubora wa kambi aliyopewa na SportPesa jijini Liverpool, England lakini mafunzo bora kutoka kwa Bellew yaliyomfanya kubwa bora maradufu na hadi sasa anaendelea kuwa mmoja wa mabondia bora kabisa barani Afrika.

Hii ilikuwa siku chache baada ya Mwakinyo kumchakaza Samm Egginton kwao Uingereza. Wakati huo alikuwa ndani ya 10 bora ya dunia kwa ubora.

 SportPesa hawakutaka Mwakinyo apotee wala ashuke, wakampa nafasi ya kuendelea na mazoezi Uingereza katika kiwango cha juu na mkataba huo wa miaka mitatu, ulikuwa kama chachu ya maendeleo kwake akienda kushinda Night in Nairobi.

 


Aina ya uchezaji wa Mwakinyo ulibadilika kwa kiasi kikubwa sana. Hadi leo unaweza kusema moja ya maendeleo ya bondia huyo ambaye anaendelea kutamba si Tanzania au Afrika Mashariki pekee bali Afrika ni mafunzo mazuri aliyopata akiwa Uingereza na baadaye akaenda Kenya na kushinda dhidi ya Mfilipino.

Kama unakumbuka, Mwakinyo alirejea tena nchini na kushinda pambano akionekana kuwa na tofauti kubwa katika upiganaji licha ya ubora wa mpinzani wake.

Mwakinyo aliishukuru SportPesa kwa kukitambua kipaji chake lakini kukiwezesha kupiga hatua kubwa baada ya mafunzo bora nchini Uingereza. Kama haitoshi, alirejea nchini akiwa amepata faida kubwa ya vifaa vya kisasa vilivyomsaidia kuendelea kujifua katika kiwango bora naye akaendelea kung’ara kama sehemu ya mmoja wa mabondia bora.

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa, Abbas Tarimba alieleza namna wamekuwa wakijitanua katika ukuzaji na maendeleo ya michezo na mfano mzuri ukawa ni huo namna walivyoingia katika mchezo huo mkubwa na maarufu wa pili hapa nchini baada ya soka.

 

Katika soka, tayari SportPesa walionyesha ubora wa kiwango cha juu wakiingia mkataba mkubwa na Yanga na Simba unaowafanya kila mwaka kumwaga zaidi ya Sh bilioni 2 na kuandika rekodi ya kuwa na mkataba mkubwa zaidi katika mchezo wa soka na michezo kwa ujumla kuwahi kusainiwa na hasa kwa ngazi ya klabu.

Pamoja na soka, upande wa ndondi, tayari SportPesa wameweka alama yao kupitia Mwakinyo na hakuna ubishi, wakati wanatimiza miaka minne ya kazi bora nchini, tayari wameonyesha mafanikio makubwa katika kusaidia michezo kuliko kampuni nyingine yoyote ya michezo ya kubahatisha.

 

Ukiachana na soka na bondia, bado SportPesa wakaendelea kurudisha katika jamii kupitia vitu mbalimbali. Uwanja waliotumia mamilioni ya fedha kuutengeneza wakiweka nyasi za kisasa kabisa kwenye Uwanja wa Taifa (sasa kwa Mkapa) lakini katika eneo la Kizimkazi, wakajenga nyumba mbili kwa ajili ya madaktari.

 

Mamilioni ya fedha walimwaga katika nyumba mbili za familia za madaktari zilizokarabatiwa na kuwa na mwonekano wa kisasa kabisa, kuwafanya madaktari wawe vizuri, wenye furaha na tayari kufanya kazi zao ngumu kwa ubora unaotakiwa. Hii ikiwa ni sehemu ya kuonyesha kweli wamelenga kurudisha kwenye jamii na wakati mwingine si lazima kupitia katika michezo pekee.

Pia kumbuka ile project yao ya Kit For Africa ambayo wamekuwa wakigawa vifaa vya michezo kama jezi, mipira na kadhalika ili wafanye mazoezi kwa ubora zaidi.

Katika hili, wanagawa vifaa baada ya Yanga au Simba ambao wanafanya nao kazi wamekuwa wakipewa kazi ya kupendekeza timu gani ya mtaani isaidiwe vifaa hivyo.


Wakati fulani, Kit for Africa ilifanyika nchini Kenya wakati nyota Yakubu Aiyegbeni wa Nigeria na Everton alipotembelea Nakuru, Kenya. Lakini baadaye imefanyika kwa miaka mitatu mfululizo jijini Dar es Salaam na timu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam zikafaidika kwa kiwango kikubwa sana.


 Hadi leo, watoto na vijana wamekuwa wakitumia vifaa vya Kit For Afrika kutoka SportPesa kuendeleza vipaji vyao na baadaye huenda wakawa ndio mashujaa wa taifa letu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic