May 13, 2021


SOKA letu lina mtindo wake wa maisha kila siku lazima liibuke jambo jipya na ukifuatilia wapi linatokea kabla halijapata ufumbuzi linakuja lingine maisha yanaendelea.

Ilikuwa ni wimbo mkubwa kwa waamuzi kufanya maamuzi mengi ya hovyo uwanjani kisha kabla hilo halijapatiwa ufumbuzi, ikawa ni ubabe kwa wachezaji.

Wachezaji wanakuwa wababe kwa wachezaji wenyewe mpaka kwa waamuzi nako wanapeleka ubabe ilimradi mambo yaendelee kwenda kama ambavyo wanahitaji iwe.

Kumbuka ubabe wa kijana wa Simba, Ibrahim Ame sambamba na kiungo mkongwe, Jonas Mkude kwa mwamuzi wa pembeni wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Gwambina na Simba.

Yalipokuja maamuzi, Ame kapigwa rugu la laki tano na mechi tatu kafungiwa kutocheza huku Mkude yeye akisubiri maelekezo mapya, hili ni soka letu acha tuendelee kupambania mafanikio tutayakuta yanatusubiri.

Kwa sasa tunaambiwa kwamba ni maelekezo ambayo yaliyeyusha ule mchezo ambao ulikuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa na wadau kati ya Simba na Yanga.

Mchezo huo ulipaswa kuchezwa Mei 8, Uwanja wa Mkapa ila uliahirishwa kwa kuwa Yanga waligomea mabadiliko ya muda kwa kuweka bayana kwamba kanuni ya ligi haikufuatwa.

Simba nao wakaja na tamko lao refu kabisa la kurasa mbili wao ombi lao Yanga ishushwe madaraja ila hawajaweka bayana kwa kanuni ipi na kifungu gani, hili ni soka letu.



Wakati mashabiki na wadau wakifikiria kuhusu gharama zao, Serikali nayo ilitoa maelekezo kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni kuja na majibu ya maswali ambayo yanaulizwa na wadau wengi, bado tunasubiri ili tuone mambo yatakwendaje.

Habari ambayo imetolewa na Serikali kupitia wizara pamoja na TFF, kupitia Bodi ya Ligi Tanzania ni kwamba mchezo huo utapangiwa tarehe na kuhusu gharama za waliotoa viingilio, watatumia kwa ajili ya mchezo ujao tiketi zao.

Ukifikiria kuhusu ubabe wa wachezaji wa ligi, sio wa Simba pekee hata Yanga pia wapo nadhani unakumbuka kwamba Carlos Carlinhos aliwahi kumpiga ngumi mchezaji baada ya kupaniki kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, ukigusa kwenye Ligi Daraja la Kwanza huku acha kabisa.

Basi kwa kuwa haya yote lazima yatokee na maisha yaendelee basi tusisahau kwamba Mei 15 kutakuwa na mechi zilizoshikilia maamuzi kwa timu moja kupanda moja kwa moja ndani ya Ligi Kuu Bara na moja kusaka nafasi ya kucheza mchezo wa play offs.

Ni kundi B ambalo vita yake sio ya kusubiri maelekezo ni lazima ifuate kanuni na utaratibu ambao upo ikiwa kutakuwa na maelekezo tutashuhudia hasara kubwa nyingine tena.

Tofauti yao ni pointi moja tu, Geita wao watamenyana na Fountain Gate, Pamba wao wanakutana na Transti Camp hapo Pamba wapo nyumbani na Geita wapo ugenini patamu hapo.

Kikubwa katika mechi hizi yasiwepo maelekezo ya timu fulani kupata ushindi ama ule ujanjaunja ambao umekuwa ukitajwa kufanyika katika mechi hizi, hapana inatosha, soka letu lisimamiwe katika misingi imara ili washindi wawe wa haki.

Pamba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 33 na wapinzani wao kwa sasa kwenye vita ya kupanda ni Geita Gold wenye pointi 34 wote wamecheza jumla ya mechi 15.

Hili kundi linaushindani mkubwa katika kuona nani anapanda kwani mshindi wa moja kwa moja anapeta ila ikitokea wote wakashinda basi nafasi ni ya kinara wa kundi huku yule wa nafasi ya pili ataangukia kucheza play offs.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic