June 22, 2021


 UNAKUMBUKA ule mchezo kati ya Simba na Plateau wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar? Basi kuna viungo wawili wa Plateau United kutoka Nigeria walikichafua kweli pale katikati ya uwanja ambao ni Issa Ndala na Ochewechi Oche.

Kati ya hao basi fahamu kuwa kiungo mshambuliaji Ochewechi Oche amefunguka kuwa yupo katika mazungumzo ya awali na Klabu ya Simba ambao wameonyesha nia ya kumhitaji kiungo huyo.

 

Katika mchezo huo Simba ililazimishwa suluhu dhidi ya Plateau ambao ulikuwa mchezo wa mtoano wa awali kwa ajili ya kufuzu makundi na Simba kusonga mbele mara baada ya kuwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 waliupata wakiwa ugenini nchini Nigeria.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi moja kwa moja kutoka nchini Nigeria, Ochewechi Oche aliweka wazi kuwa yupo katika mazungumzo na Simba ambao walianza kuongea naye tangu kumalizika kwa mchezo wao walipokutana katika michuano ya kimataifa.

 

“Simba walinitafuta tangu tulipomaliza mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa kule Tanzania, waliniambia msimu ukimalizika tutafanya mazungumzo na tayari kila kitu kuhusu mimi anakifahamu meneja wangu ambaye aliniambia kuwa wapo katika mazungumzo.

 

"Kwangu haina shida kujiunga Simba kwani ni timu nzuri na kubwa kwa Afrika, hivyo kama kila kitu kitakuwa sawa nipo tayari kujiunga na Simba,” alisema mchezaji huyo.

 

Naye meneja wa mchezaji huyo, Kunle Soname alithibitisha kuwa katika mazungumzo na Simba huku akiweka wazi kuwa viongozi wa Simba wapo siriazi na mchezaji huyo.

 

“Nipo katika mazungumzo na Simba ambao viongozi wameniambia kuwa wapo tayari kumsajili mchezaji wangu ila wameniambia wanasubiri mpaka msimu wa ligi yao umalizike, kwangu mimi pamoja na mchezaji ni jambo jema kuwa katika mazungumzo na moja kati ya timu kubwa Afrika na tutafurahi tukikamilisha dili hili,” alisema meneja huyo.

 

Kwa upande wake, msemaji wa timu hiyo, Albert Dakup alisema kuwa wamekuwa wakifuatilia Ligi ya Tanzania kwa karibu kwa kuwa wamepokea ofa ya kiungo wao kutakiwa na timu kubwa za Tanzania ikiwemo Simba.

 

“Najua ligi haijamalizika huko, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu ligi ya Tanzania kwa sababu imekuwa na ushindani mkubwa hasa kwa timu ambazo zinakamata nafasi ya juu hasa Simba, Yanga na Azam.


“Kuhusu suala la Ochowechi ninachokijua ni kwamba tumepokea ofa kutoka kwa timu za huko licha ya kwamba Simba ndiyo imekuwa ikitajwa sana lakini zipo klabu nyingi ambazo zinahitaji kumpata, siwezi kukueleza ofa ya Simba ipoje ila inatajwa maana uongozi wa juu ndiyo unafahamu kila kitu ila bado hawajaweka wazi,” alisema Dakup.

 

Kutokana na ubora wa uchezeshaji wa Ochewechi Oche kama atafanikisha usajili wake wa kujiunga na Simba basi atacheza sambamba na kiungo mkabaji wa timu Thadeo Lwanga lakini atakumbana na upinzani mkali wa namba na wachezaji kama Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Jonas Mkude ambao hucheza katika nafasi anayocheza yeye.

1 COMMENTS:

  1. Haya basi matopolo mambo hayo na ikiwa kweli ipo hela na kuweni mkono mmoja muipinduwe Meza kumkabili Mnyama peke yake bila ya kushirikisha au kuwategemea wengine

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic