July 17, 2021


FAINALI ya Kombe la Azam Sports 
Federation inatarajiwa kupigwa mwisho wa reli Kigoma, jambo jema linapaswa pongezi.

Hapa kinachotakiwa kutazamwa kwa ukaribu ni namna ya kuwa na sehemu moja ambayo itakuwa inajulikana kwa fainali ila hatua ya nusu na robo itapendeza zikiwa zinachezwa sehemu tofauti.


Wazo la kuupeleka mpira kila kona ambalo linafanywa na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) sio baya ila kuna umuhimu wa kutazama namna ambayo itafanya kuwa bora kila wakati.


Kwa sasa tunaona kwamba mchezo wa fainali kati ya Simba na Yanga unatarajiwa kuchezwa Kigoma, Uwanja wa Lake Tanganyika, hamna tatizo kwa kuwa jambo la msingi ni kushuhudia fainali.

Jambo moja ambalo wahusika kwa sasa wanapaswa kuangalia ni namna ya kuboresha mazingira ya huko ambapo timu zinakwenda kucheza.


Tunaona kwamba mchezo ambao unawakutanisha watani wa jadi huwa hauwi mwepesi kila timu inahitaji ushindi hivyo suala la maandalizi kwa timu zote ni muhimu.


Jambo la msingi ambalo linahitajika ni kuona kwamba kila timu inashinda kwa kupambana kwenye kusaka ushindi kwenye mchezo huo.



Ikiwa ni mchezo wa fainali unapigwa Kigoma basi kuna umuhimu wa kuangalia baada ya fainali kuisha nini kitatokea baadaye kwa Uwanja wa Lake Tanganyika.


Hapa kuna jambo la kujifunza kupitia Uwanja wa Nelson Mandela ambao kwa sasa Tanzania Prisons wanautumia, je Kigoma nani atakwenda kuutunza?


Ngumu sana kufikia mafanikio ya soka ikiwa kuna gharama ambazo zinapotea kwa muda kisha baadaye mambo yakawa tofauti.


Nina amini kwamba watu wa Kigoma wanapenda maendeleo na soka pia wanalipenda basi iwe kupitia maboresho ambayo yatafanywa kwenye uwanja huo yalindwe daima.


Pia iwe chachu kwa timu ambazo zipo Kigoma kupambana ili kuweza kuibukia ndani ya Ligi Kuu Bara hilo litaongeza chachu ya ushindani na timu zitautunza vema uwanja huo.


Ipo wazi kwamba sheria namba moja ya mpira ni uwepo wa uwanja hivyo kuwa na uwanja ni fursa kwa timu za Kigoma kuongeza nguvu ili ziweze kupeperusha bendera katika sekta ya michezo.


Nilishauri pia wakati ujao mamlaka kama itaona vema basi kuwe na chaguo la sehemu ya kucheza fainali na hii itakuwa inaongeza ushindani kwa timu zote shiriki kupambania kufika hatua ya fainali.


Tukirudi kwenye ligi ni kweli kwamba timu nyingi zimebakiwa na mechi moja hapo zile mbichi na mbivu zinakwenda kujulikana.


Zile timu ambazo zinakwenda kushuka daraja sasa ni wakati wao kwenda kujua kile ambacho walikipanda huku wengine wakijua kama wameweza kufikia malengo yao ama ni hapana.


Pia kabla sijafika mbali ninapenda kutoa pole kwa familia ya michezo hasa Polisi Tanzania baada ya kupata ajali hivi karibuni wakitoka mazoezini.



Ni maumivu makubwa ambayo Polisi Tanzania wanapitia na hayo sio kwao pekee bali familia nzima ya mpira inapitia kwenye maumivu.


Ngumu kufikiria namna ambavyo kila mmoja ameguswa lakini nimeona kila timu kila mchezaji, mashabiki bado wamekuwa katika hali ya kuwaombea dua Polisi Tanzania.


Katika hili tunaomba Mungu azidi kuwa pamoja na kila mchezaji pamoja na timu zote kiujumla kwa kuwa usalama wetu yeye anajua bila kuwasahau mashabiki ambao nao husafiri.


Kipindi hiki kigumu kila mmoja anapaswa kuwa mtulivu na kuendelea kuomba ili kila kitu kiende sawa.

Wataalamu ambao ni madaktari nao tunawaombea katika kazi yao waweze kufanya vizuri.


Tuna amini kwamba ndugu zetu watarejea kwenye ubora wao na maisha yataendelea hivyo ni wakati wa kuzidi kuwa na subira.


Ikiwa ni lala salama basi wachezaji waendelee kupambana kutimiza majukumu yao pamoja na benchi la ufundi kuwapa majukumu vijana wao.


Tunahitaji kuona kwamba kila mechi ambayo inachezwa inakuwa na ushindani pamoja na matokeo  ambayo ni bora kwa kila timu.


Kikubwa ni maandalizi nakupanga mipango makini kwa ajili ya mechi ambazo zimebaki kwa sasa hatua hii ya mwisho.


Zile ambazo zitapata nafasi ya kushuka zinapaswa zikumbuke kwamba jukumu lao ni kusaka ushindi kwenye mechi zao ili waweze kurudi tena kwenye ushindani wa Ligi Kuu Bara.


Wakati huu ni wa kuchanga karata upya na kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya waweze kurudi kwenye ligi muda mwingine.


Kurudi kwenye ligi kwa timu ambazo zitashuka ni jukumu lao kufanya maandalizi. Inabidi watambue kuwa kurudi kutoka Ligi Daraja la Kwanza mpaka Ligi Kuu Bara sio kazi nyepesi.


Kazi kubwa kwa wachezaji iwe kutafuta ushindi katika mechi zao zijazo na kupambana kwa hali na mali kupata wanachostahili.


Timu ambayo itajipanga ina nafasi ya kushinda hivyo ni lazima kufanya hivyo kwenye mechi hizi za lala salama.


Tambo ni muhimu na tunaona kwamba kumekuwa na hamasa kubwa kwa wachezaji kuelekea hizi mechi za lala salama hivyo mipango inabidi iwepo kwa sasa.


Maneno na tambo zisiwatoe mchezoni jukumu lao ni kutimiza majukumu bila kuogopa mpira uwanjani, nje ni tambo kama tambo na inaruhusiwa kabisa.


Ni tayari Mbeya Kwanza ina uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao pamoja na Geita Gold hapa tunawaambia kwamba karibuni huku maisha yanaendelea.


Ninapenda kuwakumbusha kwamba zile jitihada ambazo zilitumika kwenu kupanda ligi basi huku pia ziendelee kwa kasi.


Ushindani wa huku kwenye ligi ni mkubwa na hilo lipo wazi hivyo ikiwa mtaanza kujipanga wakati huu mtapata matokoe mazuri.




2 COMMENTS:

  1. Ukiandika makala mbili hapo. FAINALI IKIPIGWA PATUNZWE NA POLENI POLISI TANZANIA

    ReplyDelete
  2. Kwani hujui kama uwanja wa Lake Tanganyika unatumiwa na timu ya Kigoma sisters iliyoko ligi kuu ya wanawake? Au unataka timu gani tena iutumie. Kama vilabu vya kiume hawawezi kuja Kigoma acheni dada zetu waendelee kuutumia na wanashangiliwa sana wanapochezea hapo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic