LIGI Kuu Bara imefikia tamati Julai 18 ambapo bingwa alishapatikana mapema ambaye ni Simba na amefanikiwa kuuchukua uchampioni huo kwa mara ya nne mfululizo, hongera sana kwao.
Kutokana na kumaliza nafasi ya kwanza,Simba sasa watashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Yanga wakati kule kwenye Kombe la Shirikisho kuna wawakilishi wetu ambao ni Azam FC na Biashara United, hawa ni wageni na huu ni msimu wao wa tatu ligi kuu, wanastahili pongezi.
Wakati ligi ikimalizika, sasa timu zinaingia kwenye vita ya usajili japokuwa tayari kuna nyingine zilishaanza kusajili mapema tu na hii ni kutokana na ligi ya msimu huu kuchelewa kuisha kutokana na kuchelewa kuanza kutokana na janga la Corona.
Tumeshaanza kuona viongozi wa timu kadhaa hapa nchini wakisafiri kwenda nje ya nchi kufuatilia wachezaji na shughuli nyingine za kitimu, pengine msimu ujao wa 2021/22 utakuwa wa kipekee sana.
Wakati timu zinaenda kwenye vita ya usajili zinapaswa kukumbushwa kuwa, zinapaswa kusajili kulingana na upungufu na siyo kusajili kwa sifa kisa zimeona timu zingine zinafanya hivyo.
Msimu uliopita tulishuhudia sajili nyingi sana na wachezaji baadhi walikuwa wakipokelewa kwa makundi makubwa ya mashabiki wa timu husika hivyo basi,viongozi wayaachie kazi mabenchi ya ufundi yafanye kazi yao na wao wabaki kwenye suala la kutoa fedha ili kukamilisha usajili.
Hiki kitu nimekuwa nikikizungumza mara kwa mara kwamba makocha wasiingiliwe linapokuja suala la kiufundi maana ndiyo kazi waliyosomea na viongozi wadili na suala la kiutawala na kuingilia majukumu yasiyomuhusu.
Muacheni kocha asajili wachezaji anaowataka na hata ikitokea wakashindwa kufanya vizuri basi mnapomtimua kazi basi iwe kwa haki kwamba kwa kuwa mlimpa kila alichokihitaji na yeye akashindwa kuwapa furaha basi hakuna budi kumuondoa, hapo hamna dhambi kabisa maana kila upande umetenda haki.
Viongozi msisajili wachezaji ambao mwisho wa siku wanaishia kukaa benchi au jukwaani. Tumeona wachezaji wakali wakitoka huko timu za kawaida wanaenda timu kubwa wakiwa na viwango vya juu lakini huko wanakutana na wakubwa zaidi yao hapo maana yake unakuwa umeimaliza na timu ya taifa kwani unaua kipaji cha mchezaji ambaye pengine ni tegemeo la kesho la taifa.
Au kiongozi utaona anasajili tu mchezaji ilimradi anajua anapata asilimia kumi wao huita ‘ten percent’ sasa hii inakuwa inaharibu soka, sawa inawezekana wakati mwingine kamali inakubali kwa mchezaji kuwika kwa kuwa msaada lakini mara nyingi huwa wanafeli.
Wachezaji najua sasa hivi wengi wanaangalia fedha lakini labda niwaambie ni bora ukakaa sehemu ambayo unafanya kazi yako kwa amani bila presha na unalipwa kama kawaida hata kama ni fedha ya kawaida kuliko kwenda sehemu ambayo unalipwa sana, huchezi hata benchi hukai unaishia jukwaani, hapa unaua kipaji.
Ili soko liweze kuonekana inatakiwa uonekane unacheza sasa kama umekubali kulipwa fedha nyingi na unaenda kuishia kukaa jukwaani ni kazi bure. Tulia fanya maamuzi sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment