TAYARI mbivu na mbichi kwa timu ambazo zitashiriki Ligi Daraja la Kwanza zimetambulika na ni wakati mwingine kwa ajili ya msimu ujao wa 2021/22.
Timu nne zitakazoshiriki michuano ya kimataifa kwa
maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika na
Kombe la Shirikisho zinajulikana na yote imetokana na matokeo ambayo wameyapata uwanjani.
Majibu yaliyokuwa yanasubiriwa ni kwa timu ambazo zilikuwa chini na idadi yao ilikuwa kubwa zaidi na hizi ndizo zilizokuwa zikipambania roho au uhai wao ili kubaki katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Tayari Mwadui “margea”, hawa “walishapoteza uhai” katika ligi hiyo, zilikuwa zinatafutwa nyingine tatu za
kuteremka kwa maana ya kujipanga kuanzia nafasi ya tano. Halafu zilitafutwa nyingine mbili katika nafasi ya 14 na 13 kwa ajili ya kucheza play off na nyingine mbili za Ligi Daraja la Kwanza.
Mtiti wa mkiani haukuwa mwepesi kwa kuwa kazi ilikuwa ngumu si mchezo, maana ni kama timu nane zilikuwa zinapambana kujiokoa ingawa hapa kuna jambo kubwa la kujifunza katika timu hizi.
Timu ambazo zilikuwa katika hali mbaya zaidi na kuokoka kwao ni kugumu sana ni sita hadi saba na timu hizi zinatokea katika mikoa sita ya Shinyanga, Tanga, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Morogoro.
Katika mikoa hii, ipo baadhi ambayo ni sugu sana katika suala la kuwa na timu ambazo kila mwisho wa msimu zinakuwa zinapambana kujiokoa kuteremka daraja na hii imekuwa ni kasumba kwa kuwa hata kama timu hiyo itateremka, itakayopanda msimu unaofuata, nayo huingia huko huko.
Dodoma unaweza kusema ni wageni katika
hili, tokea walipotamba na CDA na Kurugenzi, walipotea lakini timu inayotokea mkoani hapo ya Dodoma Jiji, wao wako vizuri na wamebaki. Shida imekwenda kwa wahamiaji wa mkoa huo JKT Tanzania. Ndio maana nataka kwa kuanza kuwakumbusha Dodoma wanatakiwa kuwa mfano tofauti na wengine.
Morogoro sasa imekuwa ni tabia, tokea
kuteremka kwa Moro United ambayo baadaye ilipotea, Mtibwa Sugar imekuwa ikitamba sana na uliona timu kadhaa kama Polisi ikitamba na kupotea.
Sasa ni misimu minne, Mtibwa Sugar na ukubwa wake imekuwa ikipigania kuepuka kuteremka daraja. Imekuwa ni timu haina hata uhakika tu wa kubaki na hili linaonyesha ndani ya Mtibwa yenyewe au mkoa huo unashindwa kutoa ushirikiano kuirejesha timu hiyo kwenye mstari na kuwa imara kabisa.
Morogoro wamekuwa na uhakika na Mtibwa Sugar muda wote lakini sasa mambo si hivyo tena. Inaonekana kuna wakati watakuwa hawana timu ligi kuu na hasa kama mwendo wa Mtibwa ndio huu ambao wanaonekana wameshindwa kurejea katika kiti cha ubora cha wao kuwa timu bora au moja ya timu kubwa.
Hili ni deni kwa Wanamorogoro nao inabidi wajiulize, maana siku chache zijazo, ligi kuu inaweza kuwa ni kwenye runinga tu.
Katika mikoa iliyobaki, hii mitatu sasa ni sugu na mambo yamekuwa magumu sana. Miwili kutoka Kanda ya Ziwa kwa maana ya Mwanza na Shinyanga na mmoja wa Nyanda za Juu, Kusini yaani Mbeya.
Ihefu ilikuwa inapambana kubaki ila imeshuka, Mbeya City ilikuwa inapambana kubaki na imefanikiwa na hizi zote zinatokea mkoa huo. Lakini kwa Mwanza, Gwambina msimu mmoja tu wako katika wakati mgumu na angalia pia Shinyanga wao ndio mapemaa wameumaliza kabisa mwendo maana Mwadui imeweka rekodi ya kuteremka ikiwa na mechi zaidi ya tano mkononi.
Kuna jambo la kujifunza katika mkoa hii kama ilivyo kwa Tanga ambayo inaonekana timu zake huweza kuhimili angalau msimu mmoja bila kuwa na hofu ya kuteremka daraja lakini baada ya hapo, hakuna namna.
Wakati mwingine Tanga hawakupenda kukumbushwa hili na ukweli, wao na mikoa ya Kanda ya Ziwa, waliongoza kuzishusha timu zao kwa majungu, kutopendana na kuelewana na hili wanapaswa kubadilika kwa kuwa msimamo wa ligi, unawashitaki kwamba wana walakini na mwisho wanapaswa kurekebisha mambo yabadilike au wataendelea kupandisha msimu huu na kushusha msimu.
Coastal na Mtibwa Sugar sasa zitacheza mchezo wa mtoano kusaka nafasi ya kubaki ndani ya ligi ama kushiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Sidhani kama GWAMBINA inatoka mkoa wa Mwanza
ReplyDeleteWanatoka wilaya ya misungwi mkoa wa mwanza
Delete