July 8, 2021

 


ASIKWAMBIE mtu, kumfunga Mtani kuna raha yake, huku mitaani kwetu kuna watu tangu Jumamosi wameendelea kuvaa jezi zao za kijani na njano, huku wengine wakiwa wanaogopa hata kuzigusa jezi zao za rangi nyekundu na nyeupe.

Yote hii ni baada ya Mbungi kali iliyopigwa siku ya Jumamosi kati ya wababe wawili wa mitaa ya Kariakoo, yaani klabu za Simba na Yanga. Ndiyo nazungumzia Kariakoo Dabi, mchezo ambao unatajwa katika nafasi ya tano kwenye ubora wa dabi za bara la Afrika.

Kwenye mchezo huo ambao hapo awali ulipigwa danadana katika nyakati mbili tofauti, yaani Fenbruari 20 na Mei 8, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara klabu ya Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 mchezo ukipigwa katika dimba la Mkapa, Dar es Salaam.

Nawapongeza Yanga kwa mafanikio hayo makubwa dhidi ya Mtani wao, na kwa kuendeleza ubabe mbele ya Simba tena uwanjani akiwepo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Ushindi huo si tu umewapa nafasi Yanga kutembea kifua mbele ya Simba, bali umezidi kuwaongezea nafasi ya kumaliza katika nafasi ya pili ya msimamo kwenye Ligi Kuu Bara, nafasi ambayo imekuwa ikiwania kwa karibu na klabu ya Azam.

Yanga wana kila sababu ya kujimwambafai mitaani kutokana na ushindi walioupata Jumamosi iliyopita, lakini ushindi huo dhidi ya Mtani haupaswi kuchukuliwa kama kushinda kombe, bali wakumbuke wana kazi kubwa ya kuirekebisha timu yao kwa kumaliza mapungufu ambayo wanaonekana kuwa nayo.

Msimu ujao Yanga wanatarajiwa kuwa na michuano mingi zaidi kwani watakuwa sehemu ya klabu nne kutoka Tanzania ambazo zinatarajiwa kushiriki michuano ya kimataifa.

Katika hili Yanga wanahitaji angalau pointi moja katika michezo yao miwili ya Ligi Kuu ambayo wamesaliwa nayo, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ina maanisha kuwa Uongozi unapaswa kuweka nguvu kubwa katika usajili wa kuzidi kukifanya kikosi hicho kiwe kipana na bora zaidi, hii itawasaidia kuwa washindani na sio washiriki katika michuano watakayoshiriki msimu ujao.

Kufanya vizuri kwa Yanga hasa katika michuano ya Afrika ni hitaji la kitaifa, ili tusije kurudia makosa tuliyoyafanya msimu wa mwaka juzi kwa timu zote nne zilizokuwa zikituwakilisha kuondolewa katika hatua za awali hali ambayo ilitupunguzia pointi nyingi.

Kwa Simba kwanza nawapa pole kutokana na maumivu ya kihisia waliyoyapata kutokana na kipigo walichopewa Jumamosi na Mtani wao, muhimu wawe wapole na kuangalia wapi walikosea ili kurekebisha mapungufu yao.

Kama alivyosema msemaji wao Haji Manara kuwa hawana haja ya kuanza kulalamikia Penalti wala kumtafuta mchawi bali wajipange kwa ajili ya michezo ijayo, ni wazi kufungwa na mtani ni jambo kubwa, lakini hakuna namna imekwishatokea na hawawezi kubadilisha.

Wengine nawasikia wamekuwa wakitaja kuamini kuwa labda kipigo walichopewa kinahusiana na imani za kishirikina, hasa kutokana na utani na maneno yanaondelea kumhusu Mjumbe wa Baraza la wazee wa Yanga, Mzee Mpili.

Katika hili nadhani kila mtu ana imani yake na kama ni kufanyiana mambo, kila upande wa wababe hawa wa kariakoo umekuwa ukitajwa kufanya jambo hasa katika michezo kama hii.

Hivyo kwangu nisingependa kulichukulia katika mtazamo huo bali naamini Yanga walikuwa bora zaidi kimbinu uwanjani, kulinganisha na wapinzani wao Simba na ndiyo maana walipata matokeo.

Kipigo cha Jumamosi kimeandikisha mchezo wa nne ambao Simba wameshindwa kuibuka na matokeo ya ushindi dhidi ya Yanga katika michezo ya Ligi Kuu Bara. Ambapo Yanga imeshinda michezo miwili huku michezo miwili iliyosalia ikiisha kwa matokeo ya sare.

Hii haileti tafsiri nzuri kwa Simba klabu ambayo kwa sasa inatajwa kuwa miongoni mwa klabu bora Afrika, lazima wakae chini na kumaliza changamoto hii kwa afya ya mashabiki wao kwani mashabiki wa Simba na Yanga kwao ushindi dhidi ya Mtani ni kila kitu.

Maneno ya mzee mpili kuwa kama Simba watakaa vibaya kwenye michezo yao miwili ijayo mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho, na ule wa ngao ya hisani atawapiga tena, uwakumbushe Simba kwenye maandalizi yao, na waache kujiamini kupita kiasi.


Uchambuzi wa Vuvuzela unaopatikana kwenye gazeti la Championi Jumatano.

 

 

 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic