BAADA ya kumalizana na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi inaelezwa kuwa Uongozi wa kikosi cha klabu ya Simba umemficha kipa huyo Dar es Salaam, huku Prisons wao wakijua kuwa kipa huyo anashughulikia matatizo ya kifamilia.
Taarifa kutoka ndani ya kikosi cha klabu ya Simba zinaeleza kuwa tayari Kisubi amefikia makubaliano na Uongozi wa klabu hiyo, na kusaini mkataba wa miaka mitatu, ambapo mchezaji huyo amejiunga na Simba kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Tanzania Prisons.
Akizungumzia ishu hiyo, Meneja
wa Prisons, Prosper Mtevu amesema: “Ni kweli kipa wetu Jeremia
Kisubi hayupo na timu tangu Juni 18, mwaka huu kutokana na ruhusa maalum ambayo
alipewa ya kwenda kushughulikia matatizo ya kifamilia.
“Kuhusiana na ishu ya kusaini Simba, inawezekana akawa tayari amesaini au sivyo kwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, na kiutaratibu ana nafasi ya kusaini kwenye timu nyingine kama mchezaji huru, hivyo tutasubiri kuthibitisha hilo atakapokuja kutuaga.”
Ulipotafutwa uongozi wa Simba kuzungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema: “Ni kweli kama Uongozi malengo yetu ni kuhakikisha tunazidi kuwa bora kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye viwango bora.
“Lakini siwezi kusema chochote kuhusiana
na mipango ya usajili kwa sasa kwa kuwa bado tunasubiri ripoti ya kocha kujua
mapungufu yapi ya kuyafanyia kazi, hivyo kuhusiana na hilo tunaomba muda zaidi
wa kulifanyia kazi kabla hatujatoa taarifa.”
0 COMMENTS:
Post a Comment