KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema licha ya timu yake kushindwa kupata mchezo wa kirafiki lakini anaamini kuwa maandalizi waliyoyafanya yanatosha kuifanya timu hiyo kufanya vyema katika mchezo wao dhidi ya DR Congo.
Tanzania wakiwa ugenini wanatarajiwa kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo utakaofanyika Septemba 2 nchini Congo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, kocha Kim alisema kuwa hali ya kikosi chake ipo vizuri japo alihitaji kupata mchezo wa kirafiki jambo ambalo limeshindikana huku akiweka wazi kuwa wana imani ya kufanya vizuri kuelekea mchezo huo.
Kocha huyo amesema, wachezaji Saimon Msuva na Mbwana Samatta wataingia kambini wikiendi hii.
“Tumebakiza siku chache kabla ya kwenda Congo kwa ajili ya mechi za Kombe la Dunia, wachezaji wawili wa kimataifa, Simon Msuva na Mbwana Samatta watajiunga kikosini wikiendi hii.
“Hali ya kikosi ipo vizuri na wachezaji wameanza mazoezi, nilitamani kuwa na mechi ya kirafiki mwisho wa wiki hii kabla ya kwenda Congo ila imekuwa ngumu hivyo tutaendelea kujiandaa kila wakati kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri kuelekea mchezo huo,” alisema kocha huyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment