KUELEKEA mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa Septemba 25, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amelazimika kuwapa dozi nzito ya mazoezi mastaa wa timu hiyo ambapo sasa nyota hao wanafanya mazoezi mara mbili, hadi tatu kwa siku kwenye kambi yao nchini Morocco.
Simba waliondoka nchini Agosti 11, mwaka huu kuelekea Morocco kwa ajili ya kambi yao ya wiki mbili, yenye dhumuni la kukiandaa kikosi hicho kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22.
Baada ya kambi hiyo Simba itarejea nchini kwa ajili ya tamasha lao la Simba Day linalotarajiwa kufanyika Agosti 28, mwaka huu. Mara baada ya kumaliza tamasha hilo, Simba wataanza maandalizi ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa Septemba 25, kama sehemu ya ufunguzi wa msimu mpya.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake kwenye kambi yao Morocco, Gomes alisema: “Tumekuwa na wakati mzuri wa maandalizi tangu tumefika hapa, kwa kuwa tuna kazi kubwa ya kutetea mataji yote tuliyoshinda msimu uliopita, tuna kazi kubwa ya kufanya tukiwa hapa.
“Vijana wanajituma sana licha ya kwamba tumewaandalia ratiba ngumu ya mazoezi, ambapo tunafanya mazoezi mara mbili hadi tatu kwa siku, ili kuhakikisha tunarejea tukiwa bora zaidi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment