July 31, 2015

DIAMOND
Na Saleh Ally
KILA binadamu angependa kuwa na maendeleo ya chochote ambacho anakifanya. Lakini bado si vibaya kujivunia maendeleo ya ndugu au rafiki yako.


Inapofikia Mtanzania mwenzako akafanya vizuri, basi ni jambo la kujivunia. Jambo ambalo litakuwa ni la pamoja au utaifa.

Mfano unaposikia mwanamuziki Diamond ameshinda tuzo ya MTV au nyingine yoyote hasa nje ya Tanzania, hilo linakuwa ni jambo la Watanzania ingawa juhudi binafsi ni zake na timu yake.

Lakini unaposikia mchezaji wa Kitanzania kama Mbwana Samatta kuna timu inamtaka kwa kitita cha dola milioni 1 (zaidi ya Sh bilioni 2), lazima ujivunie kama Mtanzania.

Unakumbuka Simba ilipoing’oa Zamalek na kuivua ubingwa wa Afrika huku ikiwa ni timu bora ya Afrika mwaka 2003, Watanzania walifanya hadi maandamano.
Hali hiyo ilikuwa inatokana na ubora wa timu hiyo, ukubwa wa historia yake kuanzia Misri hadi kote Afrika. Lakini leo inamtaka mchezaji kutoka Tanzania tena kwa kitita kikubwa, naye amesema hapana, anataka kuendelea mbele zaidi.
Mimi kama Mtanzania naona ni jambo la kujivunia kama Mtanzania. Sidhani kama kuna sababu ya kununa au kusikia wivu kwa kuwa kila mtu kama Mtanzania ataiwakilisha nchi yetu kupitia sehemu yake.
SAMATTA
Umeona hata waandishi wenzangu wanaofanya vizuri ninawapongeza kwa kuwa kufanya kwangu vizuri ni sehemu ya changamoto kwao, nao wakifanya vizuri changamoto kwangu na mwisho tunakimbia haraka katika maendeleo.
Kuwa na watu kama Diamond na Samatta, hakukwepeki. Lakini kuwa nao katika wakati huu lazima tukubali ni bahati kwa kuwa kufanya kwao vizuri hakuwezi kuwa kwa nguvu za giza. Wanajituma, wanapambana na mambo yanakwenda.
Walipofikia lazima tukubali watu hao hawawezi wakawa wanalala usingizi wa pono na mambo yakawa vile au ikawa ni hewala Mungu saidia na mambo yakafikia hapo yalipo.
Ni watu wanaojituma, watu walio na nia ya kutimiza ndoto zao. Lazima tukubali Samatta ana juhudi uwanjani, anajituma mazoezini na msikivu kwa walimu wake. Ndiyo maana kawa nyota kuliko hata nyota waliokuwa kabla yake.
Diamond wakati anakuja, amewakuta wengi wakiwa maarufu. Wakiwa wameanza muziki na kujulikana sana. Lakini leo alipofikia yeye, ninaamini hata hao waliokuwa mastaa wakati ule wanaona hakuna nafasi ya kufikia. Lakini unafikiri Diamond huwa analala tu na mambo yanateremka kama mvua za masika na kufikia mafanikio? Jibu unalo.
Ndiyo maana nimekuwa sipendi kuingia kwenye siasa za “wewe team nani?” mimi ni timu Tanzania, ukipenda timu Saleh Ally”. Ukweli ni kwamba lazima tuwaunge mkono vijana wanaojitahidi na kuliletea taifa sifa.
Msikasirishwe na wao kupata mafanikio binafsi, maana pia hawawezi kupata mafanikio hadi kuliletea taifa sifa bila ya kufanikiwa binafsi.
Unaona Samatta anaendesha Range Rover Vogue yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 80, halikadhalika Diamond anasukuma BMW X6, haina tofauti ya thamani na ile ya Samatta.
Hawa vijana wanastahili, lakini nimekuwa nikijiuliza, baada ya wao nani anafuatia? Nani anaingia kwenye dimbwi hilo la mafanikio?
Najiuliza watu wanaona wanachokifanya? Wanaona walipofikia na kutafakari kwamba wanajituma, hawalali na wanapambana kwa nidhamu ya juu? Au wote tumenuna na kuwaangalia kwa jicho la husda?

Angalia kwenye Bongo Movie. Tokea pigo la kifo cha Steven åKanumba, unamuona nani tena anafanya vema? Unafikiri watu wa Bongo Movie walikuwa tayari kumuiga au kushindana na Kanumba kwa mafanikio au waliomuonea husda na wakajaa majungu. Kuondoka kwake nao wamebaki watupu hakuna hata anakaribia robo ya alivhofanya licha ya kwamba sasa hatunaye miaka zaidi ya mitatu?
Ndiyo nawauliza, baada ya Diamond na Samatta kwa maana ya mafanikio? Nani kajiandaa, maana nao ni binadamu, kesho wanaweza kushuka. Lakini walipofikia nani anaweza kufika? Tumejiandaa?



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic