DIAMOND |
Na Saleh Ally
KILA binadamu angependa kuwa na
maendeleo ya chochote ambacho anakifanya. Lakini bado si vibaya kujivunia
maendeleo ya ndugu au rafiki yako.
Inapofikia Mtanzania mwenzako
akafanya vizuri, basi ni jambo la kujivunia. Jambo ambalo litakuwa ni la pamoja
au utaifa.
Mfano unaposikia mwanamuziki Diamond
ameshinda tuzo ya MTV au nyingine yoyote hasa nje ya Tanzania, hilo linakuwa ni
jambo la Watanzania ingawa juhudi binafsi ni zake na timu yake.
Lakini unaposikia mchezaji wa
Kitanzania kama Mbwana Samatta kuna timu inamtaka kwa kitita cha dola milioni 1
(zaidi ya Sh bilioni 2), lazima ujivunie kama Mtanzania.
Unakumbuka Simba ilipoing’oa Zamalek
na kuivua ubingwa wa Afrika huku ikiwa ni timu bora ya Afrika mwaka 2003,
Watanzania walifanya hadi maandamano.
Hali hiyo ilikuwa inatokana na ubora
wa timu hiyo, ukubwa wa historia yake kuanzia Misri hadi kote Afrika. Lakini
leo inamtaka mchezaji kutoka Tanzania tena kwa kitita kikubwa, naye amesema
hapana, anataka kuendelea mbele zaidi.
Mimi kama Mtanzania naona ni jambo
la kujivunia kama Mtanzania. Sidhani kama kuna sababu ya kununa au kusikia wivu
kwa kuwa kila mtu kama Mtanzania ataiwakilisha nchi yetu kupitia sehemu yake.
SAMATTA |
Umeona hata waandishi wenzangu
wanaofanya vizuri ninawapongeza kwa kuwa kufanya kwangu vizuri ni sehemu ya
changamoto kwao, nao wakifanya vizuri changamoto kwangu na mwisho tunakimbia
haraka katika maendeleo.
Kuwa na watu kama Diamond na
Samatta, hakukwepeki. Lakini kuwa nao katika wakati huu lazima tukubali ni
bahati kwa kuwa kufanya kwao vizuri hakuwezi kuwa kwa nguvu za giza.
Wanajituma, wanapambana na mambo yanakwenda.
Walipofikia lazima tukubali watu hao
hawawezi wakawa wanalala usingizi wa pono na mambo yakawa vile au ikawa ni
hewala Mungu saidia na mambo yakafikia hapo yalipo.
Ni watu wanaojituma, watu walio na
nia ya kutimiza ndoto zao. Lazima tukubali Samatta ana juhudi uwanjani,
anajituma mazoezini na msikivu kwa walimu wake. Ndiyo maana kawa nyota kuliko
hata nyota waliokuwa kabla yake.
Diamond wakati anakuja, amewakuta
wengi wakiwa maarufu. Wakiwa wameanza muziki na kujulikana sana. Lakini leo
alipofikia yeye, ninaamini hata hao waliokuwa mastaa wakati ule wanaona hakuna
nafasi ya kufikia. Lakini unafikiri Diamond huwa analala tu na mambo
yanateremka kama mvua za masika na kufikia mafanikio? Jibu unalo.
Ndiyo maana nimekuwa sipendi kuingia
kwenye siasa za “wewe team nani?” mimi ni timu Tanzania, ukipenda timu Saleh
Ally”. Ukweli ni kwamba lazima tuwaunge mkono vijana wanaojitahidi na kuliletea
taifa sifa.
Msikasirishwe na wao kupata
mafanikio binafsi, maana pia hawawezi kupata mafanikio hadi kuliletea taifa
sifa bila ya kufanikiwa binafsi.
Unaona Samatta anaendesha Range
Rover Vogue yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 80, halikadhalika Diamond
anasukuma BMW X6, haina tofauti ya thamani na ile ya Samatta.
Hawa vijana wanastahili, lakini
nimekuwa nikijiuliza, baada ya wao nani anafuatia? Nani anaingia kwenye dimbwi
hilo la mafanikio?
Najiuliza watu wanaona
wanachokifanya? Wanaona walipofikia na kutafakari kwamba wanajituma, hawalali
na wanapambana kwa nidhamu ya juu? Au wote tumenuna na kuwaangalia kwa jicho la
husda?
Angalia kwenye Bongo Movie. Tokea
pigo la kifo cha Steven åKanumba, unamuona nani tena anafanya vema? Unafikiri
watu wa Bongo Movie walikuwa tayari kumuiga au kushindana na Kanumba kwa
mafanikio au waliomuonea husda na wakajaa majungu. Kuondoka kwake nao wamebaki
watupu hakuna hata anakaribia robo ya alivhofanya licha ya kwamba sasa hatunaye
miaka zaidi ya mitatu?
Ndiyo nawauliza, baada ya Diamond na
Samatta kwa maana ya mafanikio? Nani kajiandaa, maana nao ni binadamu, kesho
wanaweza kushuka. Lakini walipofikia nani anaweza kufika? Tumejiandaa?
0 COMMENTS:
Post a Comment