April 4, 2016


Na Saleh Ally
ULISIKIA namna ambavyo karibu kila kona ya dunia walivyokuwa wakiamini Real Madrid inakwenda kwenye Uwanja wa Camp Nou jijini Barcelona kuchota aibu katika mechi yake ya pili ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ msimu huu.

Si Ulaya tu, Tanzania na Afrika kote, wengi waliamini lazima Madrid ingefungwa katika mechi hiyo ya juzi usiku kwa kuwa Barcelona inayoongoza La Liga ina kikosi bora kabisa, tena watendaji kazi ya ufungaji watatu sasa ni kama ndugu na hawakamatiki.

Lionel Messi, Luis Suarez na Messi walipachikwa jina la MSN walionekana watafanya yao na hakuwa wa kuwazuia huku wale wapinzani wao Karim Benzema, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo maarufu kama BBC wakionekana kuwa wamedoda kwani hata timu yao iko katika nafasi ya tatu na ilikuwa na tofauti ya pointi 10 dhidi ya Barcelona.

Safari ya Camp Nou, kwa maana ya mtazamo haikuwa inaonekana ni nzuri kwa Madrid. Lakini wengi wakiwemo wachambuzi hawakuwa na subira kuona kocha mpya wa Real Madrid ambaye alikuwa anaiongoza timu yake katika El Clasico ya kwanza akiwa mwalimu, atafanya nini.


Kocha huyo amefanikiwa kuiongoza Madrid kuitwanga Barcelona kwa mabao 2-1, mabao ya Karim Benzema na Cristiano Ronaldo na bado ikaonyesha soka safi la kitabuni.

 Zinedine Yazid Zidane si mgeni wa El Clasico, amecheza tokea enzi za Kocha wa Barcelona, Luis Enrique lakini hata mshambuliaji nyota wa Barcelona, Messi pia amepambana naye.

Kwa Zidane, El Clasico ni kitu anachokijua kwa undani. Anaujua ukali na ubora wa Barcelona kwa vitendo kwa kuwa amecheza. Si rahisi kumlinganisha na Rafa Benitez au Carlo Ancelotti hata kama wao ni makocha wakubwa.
 Kuijua El Clasico, haina maana Zidane hatofungwa lakini kwa kuwa ni El Clasico yake ya kwanza, lazima ilikuwa afanye kitu tofauti, hicho ndicho kilichoimaliza Barcelona juzi usiku.

Kwa namna Madrid ilivyocheza, hesabu ya kwanza ilikuwa ni kuwaweka mfukoni MSN ambao utaona walikuwa ‘likizo’, utafikiri hawapo. Walijaribu lakini mtego wa Zidane ukawamaliza.

Mbili ilikuwa kuziba mianya ya mipira inayopitishwa katikati ya uwanja, kama ambavyo wamekuwa wakifanya Barcelona wakimtumia Messi au Iniesta. Tatu ni kupokonya mipira kwa haraka na kushambulia kwa mtindo wa kuvuruga.


Lakini mwisho, utaona mwanzo hadi mwisho wa mchezo, wachezaji wanne hawakuondoka kabisa nyuma ya mpira. Unaweza kusema Madrid walipaki angalau basi dogo aina ya Hiace lakini kila waliposhambuliwa, likawa basi kubwa kabisa kama Ngorika kwa kuwa wote walirejea na kuacha watu wawili tu mbele.

Uchezaji wa Barcelona na Madrid kimfumo umekuwa ni  4-3-3. Lakini Zidane akarejea kwenye mfumo mama wa 4-4-2 ambao ulionekana kuwazima kabisa Barcelona.

Chanzo cha kwanza cha uzimaji wa jaribio la MSN ilikuwa ni kumtumia kiungo mkabaji Carlos Casimiro maarufu kama Casemiro ambaye hata katika upangaji wa timu kabla ya mchezo ni 9% ndiyo walitabiri huenda angecheza, lakini akawa chaguo la kwanza la Zidane.

CASMIRO VS SUAREZ

Lakini unaona Zidane anawachanganya zaidi Barcelona kwa kuwa anawatumia viungo wote ambao hucheza, yaani Luca Modric na Toni Kroos. Maana yake Casemiro anakuwa kiungo wa tatu.

Utaona safu ya kiungo ya Madrid ilikuwa bora katika ukabaji kwa kuwa kwa wakati mmoja, Casemiro na Kroos walishuka chini na Modric aliyekuwa namba saba akaingia kati kucheza kama namba nane. Hivyo katikati hasa Madrid inaposhambuliwa, palikuwa pamejaa na hapakuruhusu mipango ya upenyezaji mipira.

 Kweli utaona mara kadhaa, Madrid walikosea, lakini si zaidi ya asilimia 20. Ndiyo maana hata baada ya nahodha wa Madrid, Ramos alipolambwa kadi nyekundu, Madrid hawakuwa na haraka ya kufanya mabadiliko kwa kuwa ilikuwa katika mpango sahihi wa ulinzi.

Lakini mfumo wa ushambulizi pia, wakati Madrid inatoka nyuma kwenda mbele, kwanza ilikuwa ni mchezaji mmoja au wawili kukimbia na mpira kwa kasi kama ambavyo Neymar na Messi hufanya. Utaona bao la kwanza namna Modric alivyokimbia na mpira, akampa Marcelo naye akafanya sawa, naye kabla ya kumpa Kroos tayari alibadilishana na Modric na kuingia namba saba aliyepiga krosi safi kwa Benzema.


Madrid wangeweza kufunga mabao mengi zaidi kama wangekuwa makini. Barcelona hawakuwa na mpango B wa maana kwa kuwa walilazimika kutoka katika mchezo wa mipango ya uhakika na kulazimisha bao la kona kwa kuwa Pepe alifanya uzembe, Gerard Pique akamtoroka.

Wakati Barcelona wakiwa nyumbani wanaonekana ni wakali sana, mpango mpya wa Zidane unaonekana kumvuruga hata Kocha wa Barcelona, Enrique ambaye haraka hakuwa amejiandaa kuuvunja, ndiyo maana Madrid ikiwa ugenini ikacheza vizuri zaidi na kufunga mabao mazuri likiwemo lile lililokataliwa alilofunga Bale ambalo halikuwa na tatizo kama mwamuzi angekuwa makini.

Kitu kidogo sana kinaweza kubadilisha jambo katika mechi moja kubwa. Licha ya kutokuwa na uzoefu kama kocha mkubwa, Zidane ametumia uzoefu wake wa kucheza La Liga na El Clasico, kuishangaza Barcelona.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic