Wakongwe
wa Italia, usiku wa kuamkia leo wameonyesha ukubwa ni dawa baada ya kuitandika
Barcelona ya Hispania kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora
ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mechi
hiyo iliyokuwa ya kuvutia, pamoja na kasi ya Barcelona lakini wenyeji AC Milan
walionekana kucheza kwa kujiamini zaidi na kupanga mashambulizi taratibu na kwa
uhakika.
Hadi timu
hizo zinakwenda mapumziko, hakuna timu iliyokuwa imepata bao ingawa kulikuwa na
kosakosa kutoka kila upande.
Ingawa Barcelona
inaongoza La Liga kwa tofauti ya pointi 12 na AC Milan iko nafasi ya tatu
katika Serie A, mambo yalionekana kuwa tofauti hata walivyochambua wapembuzi wa
mambo ya soka kuhusiana na mchezo huo.
Mabao yote
mawili ya AC Milan yalifungwa na Waafrika raia wa Ghana, Prince Boateng na Sulley
Muntari, tena wote wakitikisa nyavu katika kipindi cha pili.
Kabla ya
mabao hayo katika dakika za 57 na 81, Muntari nusura aipatie bao Milan baada ya
shuti lake kali kugonga mwamba.
Philippe Mexes naye alifanya kazi ya ziada
kuokoa krosi ya Alba isimfikie Pedro ambaye alikuwa katika nafasi nzuri ya
kufunga.
Kinda
Stephane El Shaarawy nusura aipatie bao Milan lakini kushindwa kuupiga mpira
vizuri akapoteza nafasi na kipa wa Milan, Christian Abbiati akachupa kiufundi
kuokoa shuti kali la Xavi kutoka umbali wa mita 30.
Pamoja na
kuonyesha juhudi kubwa, lakini juhudi za mchezaji bora duniani, Lionel Messi
hazikufua dafu mbele ya ngome kongwe ya AC Milan.
Ushindi
huo unaifanya AC Milan iende katika mechi ya marudiano Camp Nou ikiwa mbele kwa
mabao mawili huku wenyeji wake Barca wakiwa na kazi ya kushinda mabao matatu au
zaidi huku wakilinda zaidi nyavu zao zisiguswe.
Kivutio
kingine uwanjani hapo ni mshambuliaji mpya wa AC Milan, Mario Balloteli
alipojitokeza uwanjani hapo na mpenzi wake mpya, Fanny Robert Neguesha ambaye
ni mwanamitindo.
0 COMMENTS:
Post a Comment